Jumatatu, 26 Februari 2018

NDG.CATHERINE AANZA ZIARA KATIKA VYOMBO VYA HABARI ZANZIBAR

KATIBU wa  Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao (kushoto)  akikaribishwa katika Ofisi za Kituo Cha Radio ya Hits FM Radio katika ziara yake ya kutembelea Vyombo vya Habari Zanzibar.
 KATIBU wa  Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Ndugu
Catherine Peter Nao (kushoto)  akiwa pamoja na Katibu msaidizi Mkuu wa Idara hiyo , Ndugu Daud Ismail Juma.VIONGOZI wa Hits FM Radio wakibadilishana mawazo na viongozi wa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kutoka Idara ya Itikadi na Uenezi waliotembelea kituo hicho.

 MENEJA Mkuu wa Hits FM Radio Hafidh Kassim pamoja na Mkuu wa Utawala wa Kituo hicho wakifuatilia kwa makini mazungumzo na viongozi wa CCM waliofika katika kituo hicho kwa lengo la mazungumzo.

 MKUU wa Vipindi Hits FM Radio Bi.Zuhura Hussein(kushoto) akiwa pamoja na Mhariri Mkuu wa Kituo hicho Bi. Moza Saleh(kulia) wakifuatilia kwa makini kikao hicho.

 MKUU wa Vipindi Zuhura Hussein (kushoto  wa kwanza aliyevaa miwani) akieleza kazi mbali mbali zinazofanyika katika Studio ya Hits FM Radio ambapo Katibu wa NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Bi. Catherine Peter Nao( wa kwanza kulia) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa vipindi.

 MKUFUNZI wa mafunzo na utafti kwa watendaji wa Hits FM Radio Bi. Kudra Mawazo akiwa katika Chuma Cha Habari cha Kituo hicho mara baada ya kutembelewa na watendaji hao wa CCM.

 MHARIRI Mkuu wa Mwenge FM Radio Bw. Haji Ramadhan Suwed akizungumza mara baada ya kutembelewa na KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao, aliyefika katika Kituo hicho kwa lengo kujitambulisha na kubadilishana mawazo.

 MKURUGENZI wa Mwenge FM Radio  Bi. Badria Atai Masoud (wa kwanza kushoto) akizungumza na kuwatambulisha watendaji wake kwa Ujumbe uliowatembelea Kutoka Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar.

 WATENDAJI mbali mbali wa Mwenge FM Radio wakiwa katika Kikao hicho.

WATENDAJI wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar wakiwa katika Studio za Mwenge FM Radio.

 PICHA ya pamoja na viongozi na Watendaji wa Mwenge FM Radio na  Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar.


 MKURUGENZI wa Bahari FM Radio Yussuf Omar Chunda (wa pili kushoto aliyevaa chati nyeupe yenye mistari) akizungumza na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine Peter Nao na watendaji wengine waliotembelea  Kituo hicho cha Habari Kinachomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi

 Mkuu wa Utawala wa Kituo hicho Bw. Ali Ndota(kulia aliyesimama) akiwasilisha masuala mbali mbali ya utawala katika Radio hiyo, kwa Katibu wa NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar.

 BAADHI ya Wafanyakazi wa Bahari FM Radio wakiwa katika kikao cha pamoja na ujumbe wa Idara ya Itikadi na Uenezi waliotembelea Radio hiyo.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Catherine Peter Nao (katikati) akizungumza na wafanyakazi na Kituo hicho.


 MTANGAZAJI wa Kipindi Cha Michezo wa Kituo hicho Bi. Donisya Thomas akizuingumzia masuala mbali mbali ya kiutendaji ndani ya Radio hiyo.


VYOMBO vya Habari nchini vimeshauriwa kufuatilia na kuwahoji viongozi mbali mbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani ili kujua ni kwa kiwango gani Chama kimeisimamia Serikali kutekeleza iIlani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Bi. Catherine Peter Nao katika ziara yake ya mwanzo kwa Vyombo vya habari Zanzibar  toka ateuliwe kuongoza Idara hiyo.

Akizungumza viongozi na watendaji wa Vyombo hivyo ambavyo ni Bahari Fm Radio, Hits Fm Radio iliyopo Migombani pamoja na Mwenge FM Radio, alisema Serikali ya Awamu ya Saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein inatekeleza kwa ufanisi na kwa kasi kubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Katibu huyo aliendelea kufafanua kwa kueleza kuwa licha ya utekelezaji huo bado baadhi ya Vyombo vya Habari vimekuwa  haviandiki wala kuripoti utekelezaji huo hasa uimarishaji wa Huduma za msingi za kijamii zikiwemo Afya, Elimu, Kilimo, Uvuvi, ujenzi wa mitandao ya kisasa ya Barabara, uimarishaji wa miundombinu ya Anga pamoja na miundombinu ya Baharini.

Ameeleza kuwa CCM inathamini sana mchango wa Vyombo vya Habari nchini vinavyotoa habari na taarifa muhimu za Chama na Serikali bila upendeleo na ubaguzi huku vikifuata maadili kwa mujibu wa miongozo ya Tasnia ya Habari.

Alisema lengo la ziara hiyo ni kubadilishana mawazo na kujenga mahusiano endelevu baina ya Chama na Taasisi hizo za Kihabari nchini ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi zinazohusu CCM.

Pamoja na hayo amesema CCM ili iweze kuendelea kufanya vizuri katika medali za kisiasa,  ni lazima iwe karibu na vyombo vya Habari ambavyo ni wadau wakubwa wa kuhabarisha, kuelimisha na kuibua kero na changamoto zinazoikabili jamii.

“ Leo nimefurahi sana kukutana na waandishi wa habari tukaweza kubadilishana mawazo na uzoefu, lakini pia wito wangu kwenu fuatilieni utekelezaji wa Ilani ya CCM ili muweze kuwambia wananchi uhalisia juu ya mambo yaliyotekelezwa na Serikali chini ya usimamizi wa CCM.

Pia suala la kulinda maadili na miiko yenu ya Kitaaluma ni jambo muhimu kwa maendeleo ya taasisi zetu na taifa kwa ujumla”, amesema Catherine.

Pamoja na hayo aliahidi kuendelea kushirikiana na waandishi wa Habari kwa lengo la kuwarahisishia kazi zao na kupata taarifa za CCM kwa wakati mwafaka.

Akitoa ufafanuzi juu ya baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na watendaji wa vyombo vya Habari kwa kutopewa ushirikiano na baadhi ya Watumishi wa umma wenye dhamana ya kutoa taarifa kwa jamii, alisema changamoto hiyo ataitafutia ufumbuzi wa haraka ili viongozi wenye tabia hizo kujirekebisha na kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka1984.

Nao baadhi ya viongozi wa Vituo hivyo vya Radio wameeleza masikitiko yao kwa Katibu huyo, kwa kile walichodai kuwa baadhi ya Mawaziri ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na baadhi ya viongozi wa Chama hawatoi ushirikiano pale wanapotakiwa na Vyombo hivyo na kupelekea Habari kutokuwa na uwiano sawa wa Vyanzo vya Kihabari.

Akizungumza Meneja wa Hits FM Radio iliyopo Migombani Unguja, Hafidh Kassim amesema licha ya Vyombo vya Habari nchini kukabiliwa na changamoto mbali mbali bado wanaendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kutoa habari sahihi na zilizofanyiwa utafti wa kina kwa jamii.
Naye Mhariri Mkuu wa Mwenge FM Radio, Haji Ramadhan Souwed alizitaja changamoto zinazowakabili katika Kituo hicho kuwa ni pamoja na ukosefu wa baadhi ya vifaa vya kurusha matangazo yao ili yafike katika masafa ya mbali kama zilivyo Radio zingine na kuwaomba wadau, wafanyabishara na watu wenye uwezo kuwasaidia ununuzi wa vifaa hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bahari FM Radio iliyopo Migombani Unguja , Yussuf Omar  Chunda alisema changamoto waliyonayo ni ukosefu wa matangazo ya biashara hali inayopelekea kituo hicho vyanzo vya mapato vya uhakika.

Ziara hiyo inaendelea kesho katika vyombo mbali mbali vya habari vilivyopo nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni