Alhamisi, 8 Februari 2018

TABIA-AKANUSHA TAARIFA ZA CUF, ATOA ONYO KALI KWA CHAMA HICHO

NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Tabia Maulid Mwita akizungumza na Waandishi wa Habari  katika Afisi Kuu ya UVCCM Gymkhana Zanzibar.

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar umesema Chama Cha Wananchi CUF Visiwani humo kinaendelea kupoteza mvuto na uaminifu wa kisiasa kwa wananchi kutokana na viongozi wake kutawaliwa na ulaghai, chuki ubinafsi, visasi pamoja na uchu wa madaraka.

Pia umesema baada ya Chama hicho kufutika katika historia ya ushindani wa kisiasa, hivi sasa kimeibuka na mbinu mpya za kudandia Sera za CCM huku wakipotosha na kuhujumu maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na Vyombo vya Habari Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita uliofanyika katika Afisi Kuu ya UVCCM Gymkhana Zanzibar.

Amesema Umoja huo unakanusha taarifa za upotoshaji zilizotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani  aliyedai kuwa baada ya  kongamano la miaka 41 ya kuzaliwa kwa CCM lililofanyika Februari 1,2018, Vijana wa Vyuo na Vyuo Vikuu wa CCM walimfuata na kumtaka atoe ufafanuzi juu ya mada zilizowasilishwa katika kongamano hilo kwani zilikuwa za uchochezi.

Makamu Mwenyekiti huyo amesema kwa Vijana hao wapo  makini hawawezi kuomba ufafanuzi wa jambo lolote kwa viongozi wa CUF, kwani wana uongozi wao na wanapokuwa na jambo lolote wanaomba ufafanuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017.

“UVCCM ipo imara haitishwi wala kuyumbishwa na porojo na hoja dhaifu za viongozi wa CUF, tunawajua kuwa wao ni mabingwa wa kuzua uongo na fitna za kuwagawa wananchi na hizo ndio misingi ya Sera zao.

Lakini pia tunatoa Onyo kwa kiongozi yeyote wa upinzani atakayejaribu kufanya siasa Chafu za zinazohatarisha amani na usalama wa  nchi,  UVCCM tutamshughulia yeye na vibaraka wake kwa lengo la kulinda heshima ya Taifa letu.”, amefafanua Makamu Mwenyekiti huyo.

Akijibu hoja za waandishi wa habari juu ya moja ya tuhuma za CUF kuwa mada zilizotolewa katika kongamano hilo zilikuwa za uchochezi, Ndugu Tabia amefafanua kuwa CCM ni Chama kinachothamini na kuheshimu haki Umoja, mshikamano na utu, na maisha ya Wananchi wote.

Amesema tuhuma hizo hazina hata chembe ya ukweli kwani CCM imekuwa ni Chama pekee chenye sera na misimamo ya kuwaunganisha wananchi na sio kufanya uchochezi na migogoro kwa vyama vingine.

Ametaja lengo la kongamano hilo pamoja na mada zilizotolewa zililenga kuwajengea uwezo Vijana kupitia historia ya Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, historia ya Zanzibar toka ASP hadi CCM sambamba na mchango wa CCM katika Mapinduzi  ya Viwanda.

Pia aliendelea kueleza kuwa katika mada hizo kama  ipo mada iliyowagusa CUF na wakaifahamu vizuri walitakiwa kupongeza juhudi za CCM na sio kudai kuwa ni uchochezi.

Kupitia Mkutano huo wa vyombo vya habari Makamu Mwenyekiti huyo alipongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha sekta muhimu za kijamii zikiwemo Elimu, Afya na pencheni ya kila mwezi ya shilingi 20,000 kwa Wazee wote waliotimiza umri wa miaka 70.

Amesema ni aibu kubwa katika zama za siasa za sasa kuona bado kuna jamii ya wanasiasa wenye fikra mgando wasiokuwa na hata chembe ya kushauri na kuielekeza serikali ni kwa namna gani itaimarisha mipango ya maendeleo ya nchi, bali wao kazi yao ni kukosoa na kuponda kila jambo jema linalofanywa na Serikali.

Hata hivyo amesema CUF imekuwa ni kinara wa migogoro ya kugombea madaraka ndani ya Chama chao  na kusababisha mpasuko, hivyo ni lazima wanachama na wafuasi wa Chama hicho waanze mapema kurudi ndani ya CCM ili wanufaike na Demokrasia iliyotukuka kwani Chama chao hakina tena dhamana ya kisiasa ya kulinda na kutetea maslahi ya wanachama wake bali kila kiongozi anapambana na hali yake kupata madaraka ya juu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni