Alhamisi, 1 Februari 2018

WASOMI, WANASIASA WAKONGWE NA MAKADA WA CCM WACHAMBUA MIAKA 41 YA KUZALIWA KWA TAASISI HIYO

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Zubeir Ali Maulid akifungua Kongamano la sherehe za maadhimisho ya miaka 41 ya kuzaliwa kwa CCM lililofanyika Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni.

MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema katika kuadhimisha miaka 41 tangu kuanzishwa kwa Chama baadhi ya mafanikio yaliopatikana ni kuwa CCM imefanikiwa kuvumilia misukosuko ya kisiasa na kuidhibiti kwa maslahi ya wananchi wote.

Wamedai kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa demokrasia ya kweli ndani ya chama ambapo CCM imekuwa na utaratibu makini wa kuidhibiti hali hiyo ikiwemo vikao vya kimaadili.

Akizungumza katika Kongamano la kuadhimisha miaka 41 ya kuundwa kwa CCM, visiwani humu,miongoni mwa makada hao ambae ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa, Stephen Masato  Wasira amesema CCM imepita katika misukosuko na mawimbi ya kisiasa kwa miaka yote 41.

Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya Chama, ameeleza kuwa CCM inazingatia misingi yote ya demokrasia na kwamba hadi kuidhibiti hali hiyo ni kuwa muundo wake umeanzia katika ngazi ya shina.

"Sisi sote tunafahamu kuwa kuongoza lazima uanzie kwenye sehemu hii ya shina yaani kwa maneno mengine ni uongozi wa chini kabisa hivyo kwa miaka yote hii 41 ambapo CCM inadhimisha tangu kuundwa kwake hakuna chama cha kukifafananisha nacho zaidi ya ANC kutoka Afrika Kusini, kwa upande wa Afrika,"anasema Wasira

katika maelezo yake hayo wakati akitoa mada ya kongamano hilo, amesema siri ya mafanikio ya CCM katika kuvuka mawimbi hayo ya kisiasa kwenye miaka 41 tangu kuwepo kwakwe ni kwamba imeendelea kutekeleza demokrasia ambapo bado viongozi wake wanaendeleza mfumo wa shirikishi kwa wanachama wake.

Wasira ameongeza  kuwa uimara wa CCM tangu kuanzishwa kwake na kufanikiwa kudhibiti na kuimili misukosuko hiyo ya kisiasa ni kwamba tangu kuanzishwa kwake chama kimendelea kuzingatia muundo wake wa mamlaka ya chama kuelekeza wanachama.

"CCM imeendelea kuhakikisha kuwa maamuzi ya chama yanazingatiwa na wanachama hivyo mfumo wa chama ni kuwa wanachama ndio wenye kutoa maamuzi na kauli ya mwisho dhidi ya chama chao hivi ndivyo ilivyofanikiwa CCM kuwa imara katika kudhibiti misukosuko ya kisiasa tangu kaunzishwa Februari 5,mwaka 1977,"alisema

Amesema uimara wa Chama katika kudhibiti hali ya misukosuko hiyo ya kisiasa katika kipindi cha miaka 41 ya kuanzishwa kwake ni kutokana na muundo wake ambapo maamuzi ya wanachama wengi ndani ya CCM yanazingatiwa huku waliokuwa wachache wakisikilizwa na kwamba hali hiyo ndio mfumo wa demokrasia ndani ya chama.

"Wengi wanauliza kwani CCM imevuka na kudhibiti mawimbi ya kisiasa hususan katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba hali hii inatokana na kuwa chama chetu kinasimamia usawa,sera na sheria kwa mfano katika historia ya CCM viongozi wake wameendelea kupokezana mamlaka bila ya kuwepo shida yeyote hivyo ni ukweli kuwa hakuna wakufananisha chama chetu na kingine kwa kulingana na mfumo na muundo wa katiba yetu bado CCM itaendelea kuvuka mawimbi ya kisiasa,"alisema Wasira

Amefafanua kwamba  muundo wa chama ni kwamba endapo hali ya misukosuko hiyo ya kisiasa ikianza kujitokeza ndani ya CCM hivyo mfumo wa chama unatoa fursa ya kuwepo na vikao vya ndani vya maadili kujadili suala hilo na hatimae maamuzi yanatolewa kwa ajili ya kukilinda chama.

Mbali na hilo, Wasira amezitaja baadhi ya changamoto ambazo zilichangia kutaka kukiyumbisha chama licha ya kuwepo kwa uimara na huodari wa kudhibiti hali ya misukosuko ya kisiasa yakijitokeza ndani ya chama katika kipindi cha miaka 41 tangu kuanzishwa kwake.

"Unajua CCM inajuvunia kuwa na hali ya uvumilivu wa kisiasa katika kipindi chote cha miaka 41 ya kuanzishwa kwake lakini tumejifunza kuwa changamoto ya kuwepo na rushwa katika uchaguzi wa chama inachangia kudhofisha chama chetu na kinachotokea ni kuwa chama kinapata viongozi wasio kuwa waadilifu na wasiofahamu wajibu wao ndani ya chama,"alisema Mjumbe huyo wa NEC.

Kwa upande wake aliyewaikuwa Katibu wa Sekretarieti Organizesheni, Dk.Muhammed Seif Khatib, amesema  wakati CCM ikiadhimisha miaka 41 tangu kaunzishwa kwake chama kimefanikiwa kutimiza malengo yake ikiwemo ya TANU na ASP.

Amesema kuwa awali malengo hayo ya CCM yanatokana yalitokana na ASP na TANU ikiwemo kuondoa mfumo wa dhalimu wa utawala na kudai uhuru kamili, kuondoa matabaka, kuleta haki katika upatikanaji wa huduma za kijamii.

"Hivyo wakati tukitimiza miaka 41 ya CCM basi ni wazi kuwa malengo ya CCM ambayo yanatokana na TANU na ASP yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo leo hii bila ya CCM kusingekuwepo na hali ya kujitawala wenye kwa uhuru kamili na kwamba tunajivunia kutokuwepo kwa hali ya matabaka, ukabila na udini hii yote inatokana na Chama chetu,"amesema

Mapema Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Zubeir  Ali Maulid amefungua kongamano hilo na kuwataka vijana kulinda urithi ulioachwa na waasisi wa ASP na TANU kwa lengo la kuijenga CCM yenye nguvu kisiasa,kiuchumi na kijamii.

" Wazee wetu wamefanya mengi ambayo sisi leo hii tunajivunia hivyo na sisi lazima tufanye makubwa ili vizazi vyetu vya sasa na vijavyo waweze kujivunia tuliyofanya", anasema.

Hata hivyo aliongeza kuwa CCM ndani ya miaka 41 imekuwa imara zaidi kwa kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Akifunga Kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi', amesema Demokrasia iliyopo ndani ya CCM ndio chimbuko la mafanikio ya kujivunia kwa kipindi cha miaka 41 tangu kuzaliwa kwa Chama.

Ametoa wito kwa wananchi wa Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kulinda amani na utulivu wa nchi kwani tunu hiyo ikitoweka kuirejesha kwake ni gharama.

'' Chama Chetu kipo vizuri tunaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili kila mwananchi anufaike na matunda ya nchi yake huku tukijipanga na ushindi wa Dola kupitia uchaguzi Mkuu ujao",ameeleza.

Mada tatu zimetolewa katika Kongamano hilo zikiwemo Mchango wa CCM kuelekea Mapinduzi ya Viwanda, Miaka 41 ya kuzaliwa kwa CCM kumetimiza malengo ya ASP na TANU pamoja na Kuimarika kwa Demokrasia ndani ya CCM kunatoa fundisho gani kwa siasa za Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni