NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), Mhe:Dk. Abdulla Juma Saadalla "Mabodi", amesema kuungwanishwa kwa vyama vya TANU na ASP, haikuwa kazi rahisi hivyo kuna haja ya wanaCCM kuendeleza matunda yaliyotokana na vyama hivyo.
Mabodi alisema matunda hayo kwa sasa wanaCCM, wanapaswa kujivunia na kuhakikisha yanafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa kwa CCM.
Dk Mabodi aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akifungua kongamano la kuadhimisha miaka 41 ya Cham Cha Mapinduzi, huko katika Ukumbi wa skuli ya fidel Castro.
Alisema CCM imepata mafanikio makubwa, tangu kuunganishwa kwa vyama vya ASP na Tanu, hivyo ni muhimu kwa wanaccm kuendeleza Umoja na Mshikamano katika kuyalinda mafanikio yaliyopatikana.
Alifahamisha kuwa CCM ndio chama peke, kinacholeta maendeleo nchini na kuwapatia wananchi huduma bora na muhimu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
"Kabla ya ukoloni wa sultani, Watanzania hasa wazanzibari tulikuwa tukiishi katika maisha ya ujima, umoja, mshikamano, kulitokea mtafaruku wa sultani na muengereza, waasisi wakasema Afrika kwa nini wasitengeneze umoja wa afrika"alisema.
"Vuguvugu la ukombozi wa bara la Afrika likaanza, Zanzibar ikapatiwa uhuru wake Januari 12/1964, wapo wanaoamini vyenginevyo"aliongeza.
Alifahamisha kuwa kabla ya uhuru wa Zanzibar 1964, kulifanyika chaguzi nne bila ya kupatikana ushindi, ndipo waasisi waliposema wakati umefika kwa wazanzibari kujitawala wenyewe.
Hata hivyo aliwataka vijana kutambua kuwa kwa Zanzibar uchaguzi umeshafanyika, kwa sasa hakuna tena uchaguzi hadi 2020, hivyo vijana kujipanga kuhakikisha wanairudisha tena CCM madarakani.
Akiwasilisha Mada ya historia ya TANU , ASP na CCM katika Kongamano hilo Mshauri wa Rais Pemba Ndugu, Maua Abeid Daftari amesema ni vyema vijana kuwa wazalendo na pamoja na kuijua historia ya nchi yao.
Akiwasilisha mada ya fursa na mikakati ya serikali katika kusimamia Ujasiriamali na Ilani ya CCM, Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, alisema lengo la msajasiriamali ni kutengeneza kitu ambacho kitakachoweza kumpatia tija kubwa.
Mapema Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma, alisema Zanzibar inaendelea kuheshimu haki za bianadamu, kwani inaongozwa kwa misingi ya katiba na sheria.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Tabia Maulid, alisema vijana ndio wasimamizi wakubwa wa chama cha Mapinduzi, hivyo aliwataka vijana kuhakikisha wanairudisha tena madarakani CCM 2020.
Wakichangia mada mbali mbali washiriki wa kongamano hilo, walisema bado vijana hawajawa tayari kuingia katika suala zima la ujasiriamali, kwa sasa walioingia katika kazi hizo ni watu wazima tu.
Washiriki hao walisema wakati umefika kwa vijana wa wilaya ya micheweni kupatiwa boti za uvuvui, sambamba na kujengwa kwa kiwanda cha uvuvi ili vijana waweze kujikomboa na umaskini.
Mada kuu nne zimeweza kujadiliwa katika kongamano hilo, historia ya TANU na ASP, fursa na mikakati ya serikali katika kusimamia ujasiriamali, malengo ya CCM katika vita dhidi ya madawa ya kulevya na udhalilishaji wa kijinsia na nafasi ya wasomi wa CCM katika Mapinduzi na maendeleo ya nchi.
PICHA MBALI MBALI ZA MATUKIO YA KONGAMANO HUKO PEMBA FIDEL CASTRO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni