Jumamosi, 24 Februari 2018

WANASIASA WAKONGWE NA WAASISI WA UWT WASISITIZA MAGEUZI YA KIUTENDAJI

 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi akiongoza msafara wa Umoja huo katika mwendelezo wa ziara ya kuwatembelea waasisi wa UWT katika Mkoa wa Magharibi Unguja, huko Mbweni kwa Mwanasiasa Mkongwe Bi. Rufea Juma Mbarouk.

 MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Magharib Ndugu Zainab Ali Maulid akizungumza nyumbani kwake muasisi huyo.
 KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UWT anayefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu Tunu Kondo akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu Mwenyekiti kuzungumza na muasisi Bi.Rufea 



 WATENDAJI wa UWT wa ngazi mbali mbali wakiwa katika ziara hiyo nyumbani kwake Bi.Rufea.

 MUASISI wa UWT Bi.Rufea Juma Mbarouk(kushoto) akizungumza na viongozi mbali mbali wa UWT waliofika nyumbani kwake kwa lengo la kumtembelea.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi(kulia) akimkabidhi bahasha yenye zawadi Muasisi huyo Bi.Rufea Juma Mbarouk (kushoto).

 VIONGOZI na Watendaji wa UWT wakiomba dua nyumbani kwake Bi.Rufea.


 MJUMBE wa Baraza la Wadhamini wa CCM Taifa Bi.Mariam Hengwa(aliyekuwa katikati pichani) akitoa nasaha kwa Uongozi wa UWT uliofika nyumbani kwake kwa Mchina Mwisho kwa ajili ya kumtembelea.

  MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi(kushoto) akimkabidhi bahasha yenye zawadi Muasisi huyo Bi.Mariam Hengwa (kulia).
 VIONGOZI wa UWT wakiomba Dua pamoja na Bi.Mariam Hengwa. 

 VIONGOZI wa UWT wakiwa nyumbani kwake muasisi wa Umoja huo Bi.Salama Majaliwa huko Mwera.

  MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi(kushoto) akizungumza na muasisi wa UWT Bi.Salama Majaliwa, hapa Nyumbani kwake Mwera.
 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi(kushoto) akimkabidhi bahasha yenye zawadi muasisi huyo Bi.Salama Majaliwa(kulia).



NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

VIONGOZI na watendaji wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Tanzania wameshauriwa kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea wananchi ili kuibua kero zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa mujibu wa matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya  mwaka 2015/2020.

Pia wametakiwa kuzitendea haki dhamana za uongozi walizonazo katika medali za kisiasa kwa kuhakikisha CCM inazidi kuwa Chama bora na imara chenye sera , taratibu na misingi ya maadili yanayokidhi matakwa ya wananchi wote bila ya ubaguzi wa kidini na kikabila.

Ushauri huo umetolewa kwa wakati tofauti na Waasisi na viongozi wa zamani wa UWT katika mwendelezo wa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi, katika Mkoa wa Magharibi Unguja.

Akizungumza mwasisi wa UWT aliyewahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani Umoja huo na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa CCM Taifa Bi.Mariam Hengwa (75) hapo nyumbani kwake kwa Mchina mwisho, amesema Chama Cha Mapinduzi kipo ngazi za chini kwa wananchi hivyo viongozi hao wapange utaratibu wa kuwatembelea wananchi mara kwa mara.

Bi. Mariam amesema viongozi wa UWT wanatakiwa kubuni mipango mbali mbali ya kimaendeleo itakayoongeza Ari na utendaji kwa Akina Mama wa Umoja huo, na kuwavutia wanawake wa upinzani kujiunga na CCM.

Hata hivyo amewakumbusha kuwa ni lazima viongozi hao wawe na mbinu mpya za kuwasimamia watendaji kwa lengo la kuondokana na mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe visiwani Zanzibar na muasisi wa UWT Bi. Rufea Juma Mbarouk (73), amesema njia ya pekee ya kurejesha hadhi na heshima ya UWT ni Akina mama hao kuacha tabia za fitna, majungu na kauli za kuchafuana kisiasa  badala yake washikamane na kulinda maslahi ya  Chama.

Bi.Rufea aliyewahi kushika nyadhifa ndani ya SMZ na Chama Cha Mapinduzi, amesema enzi za uongozi wake wanawake walikuwa kitu kimoja wakipendana na kushirikiana kwa kila jambo, ndio maana taasisi hiyo ilivuka vikwazo na changamoto za kisiasa na imebaki salama na  kuwa na heshima kitaifa na kimataifa.

“ Viongozi, watendaji na wanachama wote wa UWT  acheni tabia na ubinafsi usiokuwa na faida kwa Chama na Umoja wetu, fanyeni kazi kwa bidii na mtambue kuwa CCM inakutegemeeni sana”, aliwasihi viongozi hao Bi. Rufea.

Naye Bi.Salama Majaliwa ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Umoja huo, alisema UWT imekuwa taasisi yenye nguvu toka enzi za Afro-Shiraz Party(ASP), ambapo Akina mama walikuwa mstari wa mbele katika kupigania demokrasia ndani na nje ya CCM.

Bi.Salama ameeleza kwamba licha ya kuwepo na mabadiliko ya mfumo wa kisiasa ni lazima viongozi wa UWT waliopo hivi sasa madarakani wasome alama za nyakati na kufanya siasa zinazoendana na mahitaji ya wananchi.

Pamoja na hayo muasisi huyo amesisitiza suala la mshikamano kwa UWT huku akiwakumbusha jukumu la msingi la Chama Chochote cha kisiasa ni kushinda kwa kila uchaguzi na ibara ya tano(5) ya Katiba ya CCM inaelekeza suala hilo, hivyo ni jukumu la Umoja huo kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinashinda na kuendelea kuongoza dola mwaka 2020.

Pia Waasisi hao wamekiri kuwa Makamu Mwenyekiti Thuwayba Kisasi ni kiongozi wa mwanzo aliyewatembelea kwa lengo la kuomba ushauri na mazungumzo, na wakawataka viongozi wa Chama na Jumuiya nyingine kufuata nyayo hizo zenye dhamira ya kuleta mageuzi ya kimaendeleo ndani na nje ya taasisi hiyo.

Akitoa tathimini ya ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi, ameahidi kuzifanyia kazi kwa vitendo nasaha, maelekezo na ushauri uliotolewa na viongozi hao wa zamani ili kujenga Jumuiya na Chama yenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuwatembelea na kuwakagua waasisi wa Chama, Serikali na Jumuiya kwa kujifunza mambo mengi ya kiuongozi na kiutendaji kutoka kwao.

Pia ameeleza kuwa miongoni mwa tunu ya kujivunia kutoka kwa viongozi hao ambao ni Akina mama ni kupigania Demokrasia na misingi ya usawa ndani ya CCM, iliyowawezesha wanawake kusimama wenyewe na kupata nafasi za uongozi katika Chama na Serikali.

Mapema akizungumza Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Kondo, amesema Umoja huo unathamini na kuwaenzi wastaafu mbali mbali kwani nguvu na maarifa yao ndio matunda yanayowanufaisha wanachama na wananchi kwa ujumla.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni