Ijumaa, 9 Februari 2018

Watokwa na Machozi Kwa hotuba ya Dk. Mabodi

WAZEE Azizi Abdalla (70) na Omar Ali Khamis (75), wamejikuta wakibubujikwa na machozi na kumlazimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Mhe:Abdulla Juma Mabodi, kukatisha hutuba yake na kuanza kuwanyamazisha wazee hao.

Wazee hao wamekumbwa na hali hiyo baada hotuba ya Naibu huyo, kuwagusa moja kwa moja ndani ya nyoyo zao, kufuatia sitofahamu zilizozuka hivi karibuni katika shehia ya Chimba.

Kufuatia hali hiyo naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, aliwataka wazee wa chama na matawi katika shehia hiyo, kukaa pamoja na vijana wao kuwafahamisha misingi imara ya Chama cha Mapinduzi.

Tukio hilo lilitokea wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi na wanachama wa Tawi la CCM Chimba, jimbo la Tumbe Wilaya ya Micheweni, huko katika skuli ya Chimba katika ziara yake ya kichama katika wilaya hiyo.

Alisema wazee wa chama katika matawi ya CCM, wanapaswa kuwaelimisha vijana juu ya suala zima la itikadi za chama, Ilani ya Chama na katiba ya chama ambazo ndio zinazowaongoza wanachama katika maisha ya kila siku.

Alisema wanachama wengi saivi ni vijana ambao damu zao bado zinawachemka lakini wachanga ki historia na itikadi na hivo busara hekima na miongozo lazima itawale katika utendaji wao, lakini pia ni bora kupatiwa elimu hiyo ili kuweza kukifahamu kiundani chama cha Mapinduzi na madhumuni na malengo ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Alisema vijana na wanachama wapya lazima kufahamu umuhimu wa CCM, pamoja na madhumuni ya Mapinduzi ya mwaka 1964, kuwa ndio ndio siku ya kujikomboa kwa wazanzibari na kujipatia uhuru wapo.

Mabodi alisema CCM ni chama kinachosaidia watu wote bila ya kujali ubaguzi wa kisiasa, uzawa wala itikadi za aina yeyote, hivyo suala la ubaguzi na uvunjifu wa amani Zanzibar halikubaliki.

Alifahamisha kuwa CCM ndio chama kinacho himiza amani na utulivu katika nchi, huu sasa sio  wakati wa kuharibu amani sambamba na kuwataka wanasiasa kutokujaribu kuchafua amani na utulivu iliyopo Zanzibar.

“Sasa hivi ni wakati wa kushindana kwa sera na sio kushindana kwa vituko, kama baadhi ya viongozi wa vyama vya vengine wanavyoendelea kuwadanganya na kuwashajihisha wananchi, niwakati viongozi hao kusema ukweli, kwani uchaguzi mkuu wa Zanzibar haupo tena mpaka 2020”aliongeza.

Alisema haiwezekani wanaccm wa Zanzibar kuendelea kuyumba yumba kwa kulishwa dhana potofu, lakini wawe mabalozi kwa waZanzibar wenzao ambao bado hawajafahamu dhana ya Kuleta maendeleo kudumisha amani mshikamano wa kitaifa na upendo wa kiujima. Alionya pia kuwa Zanzibar haiwezi kuwa yenye fujo na kutofahamiana kama nchi za jirani yenu  hata siku moja, kwani bado CCM iko macho na imara zaidi na anaetaka kujaribu ataona umuhimu wa kulinda Dola.

Hata hivyo Mabodi alikemea suala zima la ukataji wa miti ya mikarafuu ambayo ndio tegemeo la taifa, huku akimpongeza Dk Shein kwa kuendelea kulisimamia zao la karafuu kwa kufika pishi shilingi 14000 kwa kilo gredi ya kwanza lakini pia kwa kuthamini kilio cha wananchi wanaoishi katika  mashamba kwa mauzo na kupewa asilimia na pamoja na agizo la kupewa hati.

Aidha aliwataka wazee wa Chama kukaa na vijana na kuzungumza nao, juu ya maendeleo ya chama na sio kukubali kuwapatia madaraka vijana wasio na uchungu na Chama.

Hata hivyo alisema wakati wa umefika kwa mafisadi, wanaokisaliti chama cha Mpainduzi kuondoka wenyewe na sio kusubiri kuondolewa, hivyo aliwataka viongozi hao kuwachia ngazi na nafasi zao kuchukuliwa na wengine.

Mapema akizungumza na kamati ya siasa ya Wilaya ya Micheweni, Mabodi alisema kamati ya siasa ndio msimamizi wa yale ambayo yameagizwa na Ilani ya CCM.

Akizungumzia lengo la ziara hiyo, alisema ni kuimarisha chama ambapo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, siasa imeanza kushamiri na CCM kuwa tishio, huku akiwataka wanachama kutokurudi nyuma.

Aidha alipongeza Redio Jamii za  Micheweni na Mkoani kwa kuendelea kuwaelimisha jamii, kwa kuzungumzia suala la Maendeleo ambayo ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

Hata hivyo alisema chama cha Mpainduzi Kimependekeza, kujengwa kwa kiwanda cha kusindikia Samaki katika eneo la Uwekezaji Pemba, ili kuweza kutoa ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, alilitaka shirika la Umeme ZECO Tawi la Pemba, kujenga kituo cha kuuzia huduma hiyo, ili kuwaondoshea usumbufu wananchi kwenda kufuata huduma za umeme Wete. Lakini na huduma za Benki ATM na uzwaji wa Tiket za Meli ili kuweka huduma hizo karibu na wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Micheweni, Mariyam Omar Ali, alisema chama cha Mapinduzi wilaya hiyo, bado kinamashirikiano na  Serikali na asasi nyengine za kijamii na maendeleo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Ali Masoud Kombo, alisema tayari skuli ya sizini imeshaingizwa katika mpango wa halmashauri kupitia fedha za jimbo pamoja na bajeti ya Halmashauri ya utejkelezaji wa kazi zake.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib, alisema skuli ya Chimba karibu wanafunzi wao watarudi katika skuli yao kutoka skuli ya Kinowe ambayo iko masafa marefu, na huduma za afya zimeimarika kwa kupelekewa wakunga ambao ni wakazi wa maeneo ya hapo hapo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa aliwapongeza Viongozi wote waliochaguliwa na kuwataka wasichoke kugombania wakati utakapofika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni