Jumamosi, 27 Januari 2018

BALOZI SEIF, RC-AYOUB NA DK.MABODI WATANGAZIA UMMA UMUHIMU WA KUCHANGIA DAMU


 BAADHI ya wananchi walioshiriki tamasha  la uchangiaji damu wakifuatilia matukio mbalimbali yanayoendelea kwenye maeneo ya Kumbukumbu ya Mnara wa miaka 50 ya  Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika tamasha la uchangiaji wa damu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini na Magharib, katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.
 MKUU wa Mkoa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumzia lengo la Tamasha hilo la uchangiaji wa damu salama.
 MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd ambaye ni mgeni rasmi akihutubia katika Tamasha la uchangiaji wa damu salama kwa hiari.


   BAADHI ya waandaji wa tamasha la uchangiaji damu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana (BIWO).
 NAIBU Katibu Mkuu wa Cha Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Mabodi mara baada ya kumaliza kuchangia damu katika tamasha hilo.



 KATIBU Msaidizi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), MKoa wa Magharib Suleiman Mzee Suleiman akichangia damu katika tamasha hilo la uchangiaji damu.

 MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd akikagua zoezi la uchangiaji wa damu katika tamasha hilo.


 KOPLO  Suleiman Ali kutoka Jeshi la Polisi Kituo cha Ng'ambo Zanzibar akichangia damu. 

 VIJANA wa Chuo cha Sanaa ya mchezo wa kujihami cha Chicago bulls kilichopo Kijangwani Zanzibar  wakiwa katika Tamasha hilo na kuonyesha uwezo wao wa kupamba na adui kwa kutumia viungo vya mwili wa binadamu bila kutumia silaha.
 VIJANA wa Mchezo wa sanaa ya kujihami kundi la Taikwando wakionyesha uwezo wao katika Tamasha hilo.




NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema suala la uchangiaji wa damu salama kwa hiari linagusa maisha ya wananchi wote.

Kauli hiyo ameitoa leo katika tamasha la uchangiaji wa damu salama lililofanyika leo katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge, amesema mahitaji ya damu ni ya kila siku na kwamba kuna haja ya wananchi kuwa na uzalendo wa kujitolea kwa ajili ya maisha ya wengine.

Amesema bado kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wagumu kujitolea katika mambo mbali mbali ya kijamii likiwemo suala la kuchangia damu, hali ya kuwa manufaa ya zoezi hilo yanabeba maslahi ya wengi hasa pindi panapotokea mahitaji ya damu.

Balozi Seif ameeleza kuwa kitendo cha kuchangia damu kwa hiari kina thamani kubwa juu ya uhai wa maisha ya watu wanaopata ajali na Wajawazito wanaohitaji damu nyingi wakati wa matibabu.

" Utamaduni wa kuchangia damu tuuendeleze na mimi nachukua jukumu la kuwambia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nao waandae Tamasha kama hili la kuchangia damu ili wawe sehemu ya kuokoa maisha wa wananchi wao na kupunguza vifo.", ameeleza Balozi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharib Ayuob Mohamed amesema bado zanzibar ina mahitaji makubwa ya damu kwani kasi ya matumizi yake ni kubwa kuliko kasi ya uchangiaji wa damu hiyo.

Ayoub amebainisha kuwa bado wananchi, taasisi za umma na binafsi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mkoa na Serikali kuu ili kubatikana damu kwa wingi itakayoweza kukidhi mahitaji yac huduma husika.

Akizungumza katika tamasha hilo Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewataka wananchi wa visiwani humu bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila kuwa na utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wenzao  husasan wanaopata ajali na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Naibu huyo Katibu Mkuu amesema nchi zilizoendelea na zinazoendelea zimekuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vifaa tiba vya hospitalini, lakini wameshindwa kutengeneza damu ya binadamu kwa ajili ya matumizi ya kitiba

Pia, amewambia wananchi kuwa wanatakiwa kutambua kuwa hakuna nchi, kampuni wala kiwanda kinachotengeneza damu bali wananchi wenyewe ndio wanaotakiwa kuchangia damu zao ili ziokoe maisha ya watu wenye mahitaji ya damu hiyo”,.amesema Dk.Mabodi.

Akizungumzia faida ya utoaji wa damu kitaalamu amebainisaha kuwamba mtu anapotoa damu anapunguza vichocheo vya hasira pia damu inapotoka mwilini inatoa fursa ya kutengeneza damu nyingine mpya inayokuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji katika mzunguko wa damu mwilini.

Hata hivyo, ameeleza kuwa matukio ya ajali za aina mbalimbali pindi yanapotokea huku wa kina mama wajawazito wanaojifungua wanahitaji damu hiyo na kwamba lazima utamaduni wa kutoa damu upewe kipaumbele.

Naye Ofisa Uhamasishaji kutoka Mpango wa Damu   salama Zanzibar, Omar Said Omar amezipongeza taasisi   zilizoandaa tamasha hilo la kuchangia damu na kwamba  litasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.

Amesema  matarajio ya kitengo hicho ni kupata zaidi ya chupa za damu 1,000 ambazo kwa matumizi yake chupa moja utumika kwa watu watatu ambao wanaohitaji huduma za kimatibabu.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi, askari wa majeshi ya ulinzi na Idara maalum za SMZ pamoja na wananchi walioshiriki kuchangia damu  waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuwahamasisha wananchi wengine kujitokeza kuchangia damu.

Kwa upande wake Koplo Suleiman Ali kutoka kituo cha Jeshi la Polisi la Ng’ambo, amewashauri askari wwenzake  kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu kwa lengo la kuunga mkono kampeni za uchangiaji wa damu.

Naye Nassor Othman Mkaazi wa Kisauni Unguja, amesema kuwa yeye ni  mdau wa kuchangia damu kwa miaka sita na wakati mmoja kati ya familia yake wanapohitaji damu wanapata huduma hiyo bila tatizo.



Ijumaa, 26 Januari 2018

THUWAYBA: AWATEMBELEA VIONGOZI WA ZAMANI WA UWT


 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi.

MAKAMU Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi(UWT),Thuwayba Kisasi, amewasihi  viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kuendelea kutoa maoni na ushauri mbali mbali utakosaidia kuimarisha taasisi hiyo kisiasa, kiutendaji na kiuongozi.

Nasaha hizo amezitoa wakati alipowatembelea viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kwa lengo la kupata ushauri unaotokana na uzoefu wao wa kiutendaji kisiasa pamoja na mambo mengine ya kijamii na kiuchumi.

Viongozi waliotembelewa ni pamoja na  Bi. Fatma Mbarouk, Bi. Fatuma Theresa,  Bi. Asha Mwinyi, Bi. Salma Yusuph, Bi. Mwantantu Yusuph Shaaly  pamoja na Bi. Johari Yusuph Khatib.

Akizungumza mara baada ya kuwatembelea Makamu Mwenyekiti huyo amesema bado jumuiya hiyo inathamini juhudi za viongozi na watendaji hao waliowahi kuongoza taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa.

Makamu huyo amesema licha ya kupata michango yao na kuelekeza ni kwa namna gani viongozi wa sasa wataongoza tasisi hiyo pia aliongeza kuwa suala la kuwajulia hali zao viongozi hao ni sehemu ya utamaduni unaotakiwa kuendelezwa na viongozi wengine.

Katika maelezo yake Thuwayba aliongeza kuwa haitaishia hapo kuwatembelea viongozi hao wa jumuiya hiyo ambapo UWT itaendelea kuwawekea kipaumbele bila kuchoka.

"Nimejifunza mengi kutoka kwa viongozi wetu wastaafu na wametushauri kuwa tuendelee  kushikamana, tupendane na kufanya kazi zetu kwa bidii.,"alifafanua  Makamu huyo.

Aliongeza kuwa viongozi hao wameshauri jumuiya hiyo iwe na Umoja, nguvu na kutoyumba kwa namna moja ama nyingine na kwamba kufanya hivyo UWT itakuwa imara.

Naye miongoni mwa viongozi hao waliotembelewa Bi. Johari Yusuph Khatib, aliwataka UWT kuwa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali zote mbili kwa lengo la kupata uzoefu mbali mbali wa masuala ya uongozi.


Jumapili, 21 Januari 2018

MATUKIO KATIKA PICHA MKUTANO WA UCHAGUZI WA SHIRIKISHO LA VYUO VIKUU CCM SENETI YA UNGUJA.


 BAADHI ya Maafisa wa UVCCM na CCM Zanzibar wakimsubiri Mgeni rasmi katika  Mkutano wa Shirikisho la Vyuo Vikuu CCM  Seneti ya Unguja uliofanyika Afisi Kuu ya CCM  Kisiwandui Zanzibar.

 Mwenyekiti  mtaafu wa Shirikisho hilo Khamis Kheri Ame(kulia) akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi'(kushoto) mara baada ya kuwasili Kisiwandui kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano huo.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk.Mabodi akipokelewa kwa nyimbo maalum za Chama baada ya kuingia katika Ukumbi wa Mkutano wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

 BAADHI ya Wajumbe na Wagombea wa nafasi mbali mbali katika Mkutano huo wa Uchaguzi.

Mshereheshaji  wa Mkutano huo ambaye ni Katibu wa Hamasa Mstaafu wa Shirikisho hilo pia ni Afisa wa CCM Zanzibar akisoma Utaratibu wa matukio mbali mbali ya Mkutano huo katika Mkutano huo.

 KATIBU wa Shirikisho hilo Kassim Salum Abdi akisoma taarifa ya utekelezaji katika Mkutano huo.

 MSIMAMIZI wa Uchaguzi huo Bi.Asya akifafanu jambo juu ya utaratibu wa upigaji kura.

 Mwenyekiti mstaafu wa Shirikisho hilo Khamis Kheri Ame akizungumza katika Mkutano huo.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza na vijana wa Shirikisho hilo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akifugua mkutano huo na kusisitiza umuhimu wa viongozi  na wanachama  Kusoma Katiba ya CCM pamoja na Kanuni zake.
 KIONGOZI wa  zamani wa Shirikisho hilo akitoa neno la shukrani kwa niaba ya shirikisho hilo.
  




MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita (kushoto) akipeana mkono wa pongezi na aliyekuwa Mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa UVCCM Taifa kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Thuwaiba Pandu katika Mkutano wa Uchaguzi huo.

CCM ZANZIBAR YASEMA HAIWEZI KURUDI KATIKA MEZA YA MAZUNGUMZO NA WAPINZANI

NAIBU Katibu Mkuu wa  CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Uchaguzi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu CCM Seneti ya Unguja.



CHAMA Cha Mapinduzi CCM Zanzibar kimesema kuwa kwa sasa hawana muda tena wa kukutana na wapinzani kuzungumzia masuala ya uchaguzi na kazi iliyo mbele yao ni kupanga maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi alipokuwa akifunguwa mkutano mkuu wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Mkoa huko Ofisi Kuu CCM KIsiwandui.

Msimamo huo umetolewa na Dk. Mabodi kufuatia baadhi ya viongozi wa Chama cha CUF kupitia mikutano yao ya ndani kuwambia wafuasi wao kuwa wanatarajia kurudi katika meza ya mazungumzo na CCM kujadili uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema wakati ambao kulikuwa na muda wa kufanya hivyo waliwazungusha na kufikia hata kuwahangaisha wazee wao na sasa muda haupo tena na kilichobakia ni kuangalia namna gani wanaweza kukiimarisha chama na kupanga mikakati ya kuwaletea wananchi wao maendeleo.

“Hakuna mazungumzo tena kwa sasa tukutane 2020 katika uchaguzi, washaona mambo yanakwenda vizuri wanaleta vidudu mtu”, alisema Mabodi.

“Walikuja wzungu hapa ofisini kwangu nikawaambia sisi suala la uchaguzi limekwisha tunapanga maendeleao”, aliongeza Naibu Katibu Mkuu huyo.

Aidha alisema kuwa wakati huo CCM iliwatumia wazee akina Dk.Salimin na Marais wengine wastaafu pamoja na wanasiasa wakongwe wa CCM ili kuzungumzia suala hilo lakini badala yake walikimbia na kuutia mpira kwapani.

“Tuliwaita mpaka wazee wetu mkatuzungusha  sasa hivi wanataka nini hatuna muda tena na Dk. Shein huyo anapepea yupo  nje ya nchi kutafuta pesa za kuwaletea maendeleo wananchi”, alisema.

Samabamba na hilo aliwataka wana CCM wa Shirikisho hilo kujitahidi kuwa mabalozi wazuri katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuingiza wanachama wapya na kuwashaiwishi kwenda kujiandikisha katika daftari la kupiga kura wale wote ambao tayari wameshafikia umri wa
kupiga kura.

Alisema kuwa CCM pamoja na kuwa na wafanyakazi wengi ndani ya ofisi na jumuiya zao lakini bado nguvu za wanachama wa nje zinahitajika ili kuweza kukiletea ushindi.

“Kama hatujawatumia wanaCCM waliopo nje ya Ofisi zetu hatutofika mbele, lazima tutumie jeshi la wanaCCM hawa kuwaelezea watu ili kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi”, alisema.

Hata hivyo aliwataka wanashirikisho hilo kusoma katiba na kanuni za chama na kujenga ushirikiano na viongozi wao katika kujikjenga chama na inapotokea matatizo wayatatuwe kwa kulingana na katiba na kanuni zinavyoelekeza.

TABIA: AMESISITIZA MAADILI KWA VIJANA.


 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Viongozi wa Shirikisho la Vyuo vikuu CCM Seneti ya Unguja uliofanyika Kisiwandui.

 Aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kupitia Mkutano Mkuu wa 9 wa Uchaguzi wa Umoja huo  Thuwaiba  Pandu akitoa neno la shukrani kwa waalikwa katika  Mkutano huo.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


MAKAMU Mwenyekiti wa  UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita amewataka vijana waliopo katika Vyuo Vikuu kuwa mfano bora wa kulinda maadili na utamaduni wa nchi.

Rai hiyo ameitoa wakati akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu  Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma  Saadalla ‘Mabodi’ katika ufunguzi wa Mkutano  Mkuu wa Uchaguzi  wa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM Seneti  ya Unguja.

Alisema kuna baadhi ya vijana wa Vyuo Vikuu wamekuwa mstari wa mbele kuvunja maadili kwa kushiriki katika vikundi viovu vya matumizi ya dawa za kulevya  pamoja na vitendo vya uzinzi vinavyopelelekea maambukizo ya maradhi ya Ukimwi.

Alisema kwa mujibu wa takwimu mbali mbali za kitaalam kutoka Wizara ya Afya nchini zinaonyesha vijana wengi wameambukizwa  VVU hali inayotakiwa kila kijana kujitadhimini na kuchukua tahadhali kubwa juu ya Afya yake.

Tabia alieleza kuwa bila ya wasomi nchi haiwezi kupiga hatua yoyote ya maendeleo badala yake panaweza kutokea madhara ya nchi kutawaliwa kifikra na wageni.

 Pia , aliwasihi vijana wa Shirikisho hilo kujifunza mambo mbali mbali ya historia ya siasa za Zanzibar pamoja na Itikadi na misingi ya CCM kiuongozi na kiutawala ili waweze  kufahamu majukumu ya msingi ya Chama na Jumuiya zake.

Akizungumzia  Umoja na mshikamano, Tabia alisema UVCCM itakuwa imara endapo viongozi wake wataendeleza utaratibu mzuri wa kushirikiana na vijana wa makundi mbali mbali yaliyopo katika jamii kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa wakati.

Makamu Mwenyekiti huyo aliwambia vijana hao kuwa Uchaguzi ndani ya Chama umekwisha na kwa sasa kilichobaki kwa viongozi waliopo madarakani ndani ya UVCCM ni kufanya kazi kwa ushirikiano ili Chama cha Mapinduzi kiweze kupata ushindi katika harakati mbali za Uchaguzi wa Dola.

“ Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,,,tusikubali vijana wenzagu kuwa dhaifu ndani nan je ya jumuiya yetu ni lazima tuwe wamoja kwa kuepuka majungu na fitna zisizokuwa na msingi wa kuleta maendeleo ndani ya Jumuiya yetu.

Lazima tukubali mabadiliko ndani na ndani ya Jumuiya yetu kwa kuacha utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea kwani viongozi wetu ambao ni  Mwenyekiti wa  CCM Taifa Dkt.Magufuli pamoja na Makamu Mwenyeti wa CCM Zanzibar Dk.Shein,,wanakesha wakiangaika kwa ajili yetu naomba nasi tusiwaangushe bali tuwaunge mkono”,.alisisitiza Tabia.

Pamoja na hayo alisema kila kijana ndani ya UVCCM ana haki ya kushiriki katika harakati mbali mbali za kisiasa bila ya kuwekewa vikwazo wala mizengwe kwani taasisi hiyo inaongozwa kwa misingi ya Kikatiba.

Aliongeza kuwa huu ni wakati wa vijana kutumia vizuri muda wao kwa kuzitumia vizuri fursa zilizomo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa kutafuta nafasi za kujiendeleza kimasomo nje ya nchi pamoja na ujasiria mali katika mitandao ili kujiongezea kipato.
“ Nasaha kwenu tutumie muda mwingi kuombeana mema na kuonyeshana fursa za maendeleo kuliko kushambuliana wenyewe kwa wenyewe mitandaoni  badala ya kuelekeza nguvu hizo kwa wapinzani”,.alifafanua Tabia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Shirikisho hilo Mwanasiasa  kijana ambaye ni mwanaharakati na diwani wa kuteuliwa  Thuiwaba  Pandu ,alisema Chama cha Mapinduzi ni kinara wa kuwalea vijana wake katika misingi na malezi mema.

Alieleza kuwa Vijana wa shirikisho hilo watayafanyia kazi maelekezo  na maagizo mbali mbali yaliyotolewa na viongozi wa  CCM na UVCCM.


Pamoja na hayo amekiomba Chama kuzishauri Serikali zote mbili ya Zanzibar pamoja  na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandaa utaratibu wa kutoa kipaumbele cha kuwaajiri vijana mbali mbali wa CCM ambao wana sifa ili kupunguza wimbi la upungufu wa ajira kwa kundi hilo.

DK.MABODI: AMEWAAGIZA WASOMI WA CCM KUFANYA UTAFITI UTAKAOLETA MATOKEO CHANYA


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Seneti ya Unguja uliofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza na kusisitiza juu ya umuhimu wa vijana wa UVCCM hasa wa shirikisho hilo kusoma Kanuni na miongozi mengine ya Kikatiba ili kutambua wajibu wao.

MWENYEKITI wa Shirikisho hilo aliyemaliza muda wake Khamis Kheri Ame akitoa nasaha zake katika mkutano huo. 

Wajumbe wa Shirikisho la Vyuo Vikuu CCM seneti ya Unguja wakimsikiliza Mgeni rasmi Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ wakati akifungua  mkutano wa Uchaguzi wa seneti hiyo uliofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.


 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaagiza  vijana wasomi wa Chama hicho kuanzisha utamaduni wa kufanya Tafiti mbali mbali za kitaalamu ili kubaini baadhi ya changamoto zinazokabili kundi la vijana na jamii kwa ujumala  hasa upungufu wa ajira.

Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Mkutano wa Uchaguzi wa Shirikisho la Vyuo vikuu CCM Unguja la kuwachagua viongozi  Watano wa Seneti ya Unguja, ambapo Mkutano huo umefanyika katika Afisi Kuu CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.

Dk.Mabodi alisema Wasomi wa Vyuo vikuu ndani ya CCM ni lazima wakubali mabadiliko ya nyakati kwa kufanya kazi zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mfumo wa Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya ndani ya taasisi hiyo imara ya Kisiasa.

Alisema nchi zilizoendelea duniani zinategemea msaada mkubwa wa wasomi ambao ni vijana waliohitimu fani mbali mbali katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ambao wana uwezo na maarifa  ya kitaalamu yanayochochea ufanisi wa kimaendeleo.
Pia, aliongeza kwa kueleza kwamba CCM ina utajiri wa Rasilimali watu waliobobea katika fani mbali mbali hivyo ni lazima watoe mchango wao katika kuandaa mipango mikakati ya kukiletea chama hicho ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2020.

Hata hivyo amesema vijana hao wa Vyuo vikuu wana wajibu wa kusoma alama za nyakati kwa kuwa mfano bora wa kubuni na kutekeleza kwa vitendo mikakati mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ili vijana vya vyama vya upinzani wavutiwe na utamaduni huo na kujiunga na hatimaye kujiunga na Chama cha Mapinduzi.

Akizungumzia fursa zinazotokana na usimamizi pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 alitaja mchakato wa Utafiti wa Uchimbaji wa mafuta na Gesi Zanzibar  kuwa ni sehemu muhimu inayohitaji vijana wasomi watakaolinda rasilimali hiyo isifilisiwe na nchi za kigeni.

Alisema fursa ya kuanza utafti huo ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya  mwaka 1964 chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, aliyeasisi mfumo rasmi wa Zanzibar kujitawala kiuchumi, kisiasa na kijamii.

“ Utafiti huu umeanza mwaka 1952 ambao ulibaini ndani ya Ardhi na mwambao wa visiwa vya Zanzibar kuwepo kwa dalili za rasilimali hiyo inayoingia katika kundi la madini asilia, na juhudi ziliandelea hadi kufikia Serikali ya awamu ya saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Shein kupigania suala hilo likapewa baraka za kisheria zilizoruhusu Zanzibar  kushugulikia yenyewe mchakato wa utafiti hadi uchimbaji”,. Alieleza Dk.Mabodi.

“ Nyinyi ni wasomi ambao jamii ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wanakutegemeeni mlete mabadiliko ya kweli ndani ya Chama chetu na Serikali zote mbili zinazotokana na CCM.

Lakini pia ni lazima muwe wabuni  kwa kufanya utafiti ndani na nje ya CCM kwa lengo la kupata takwimu sahihi za mambo  mbali mbali yatakayosaidia Chama kuimarika kisiasa kutokana na mingo yake kutekelezwa Kisayansi.”, alisema.

Akizungumzia kwa ufupi historia ya Zanzibar  Dk.Mabodi alisema kuwa maandiko mbali mbali ya historia yanadhibitisha kuwa Zanzibar kabla ya kutawaliwa na Wakoloni ilikuwa na Utawala wake wa jadi uliokuwa katika mfumo wa ujima, ambao wananchi wake waliishi kwa amani , ujamaa na kujitegemea.

Alisema kupitia muongozo huo wa historia ni lazima vijana wa sasa wajijue kuwa wana jukumu la kuhakikisha CCM iliyotokana na vyama vya ASP na TANU inaendelea kutawala na hakuna Chama chochote cha upinzani kitakachoshika madaraka.

Akizungumzia  Uchaguzi wa viongozi mbali mbali wa Shirikisho hilo alisema ni lazima wachague viongozi bora wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa waliowachagua bila ya kusukumwa.

Pamoja na hayo aliwasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kuhakikisha wanachagua wenye uwezo na uthubutu wa kujenga hoja imara na kujibu hoja za wapinzani  bila ya kuteteleka.

Aliwataka wasimamizi wa Uchaguzi huo kutenda haki bila ya upendeleo wa mgombea yeyote ili kulinda heshima ya CCM na kuruhusui mkondo wa Demokrasia ifanye kazi yake kwa mujibu wa miongozo na kanuni za uchaguzi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita alisema mafanikio yaliyopatikana Zanzibar katika sekta mbali mbali yametokana na juhudi za kiutendaji na ushiriki  wa vijana wasomi wa Chama hicho.

Ametoa nasaha wa vijana hao kuwa ili kufikia malengo waliojiwekea kisiasa ni lazima wafanye kazi  kwa bidii ili kukisaidia chama kufikia malengo yake ya kushika dola kila uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo ndogo.

Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu wa vijana wa shirikisho hilo la vijana wa CCM wa vyuo vikuu kusoma Katiba ya CCM pamojana na kanuni ya UVCCM kwa lengo la kutambua wajibu,haki zao pamoja na mipaka yao kiutendaji.

Akitoa salamu za Mwenyekiti wa Umoja huo Kheri James, Tabia alisema kuwa kiongozi huyo anawasihi waendelee kuwa wamoja kwa kila jambo jema lenye malengo ya kuleta manufaa ndani ya CCM na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapema Mwenyekiti anayemaliza  muda wake katika Shirikisho hilo Khamis Kheri Ame alisema lengo la uchaguzi huo ni kutimiza matakwa ya Kikatiba yanayoruhusu mabadiliko ya awamu za uongozi kwa kila kipindi cha miaka mitatu.

Pamoja na hayo amewashukru wajumbe wa Shirikisho hilo alioshirikiana nao kwa kipindi chote cha uongozi wake na kuwataka viongozi wapya watakaochaguliwa kuhakikisha wanalivusha salama shirikisho hilo kuelekea ng’ambo ya maendeleo endelevu.


Katika Uchaguzi huo wanachaguliwa viongozi mbali mbali ikiwemo nafasi ya  Mwenyekiti, Katibu, Katibu wa hamasa pamoja na wajumbe wawili wa Kamati ya Uratibu.

Jumamosi, 20 Januari 2018

BALOZI SEIF ALI IDD: AMEUNGANA NA MAMIA YA WANANCHI KATIKA KHITMA NA DUA YA KUWAOMBEA ASKARI 10 WALIOUAWA DRC KONGO


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.



MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seid Ali Idd(wa pili kushoto) akizungumza na vyombo vya Habari juu ya Khitma na Dua ya kuwaombea Askari wa JWTZ waliouawa DRC Kongo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk,Mabodi(wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Ayoub wakiwa pamoja na Balozi.

MAMIA ya Wananchi, waumini wa Dini ya Kiislamu, Askari wa Majeshi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini pamoja na Ndugu na wana Familia leo wameungana katika Kisomo cha Hitma, Dua ya pamoja na Arubaini kwa ajili ya kuwarehemu Wanajeshi 10 wa Tanzania waliouawa wakati  wakilinda Amani Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepoteza Vijana wake hao mashujaa na walinzi wa Taifa waliouawa wakati wakitekeleza jukumu lao walilokabidhiwa na Umoja wa Mataifa la kusimamia ulinzi wa Amani Nchi ya DRC baada ya kuvamiwa ghafla na Waasi wa Nchi hiyo.

Kisomo cha Hitma na Dua hiyo ya pamoja kimefanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Noor Muhammad uliopo Mtaa wa Kwamchina Mombasa na kushirikisha pia Viongozi wa Serikali zote Mbili Wanasiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Tukio hilo la kusikitisha la kuuawa kwa Askari wa JWTZ lililogusa nyoyo za Watanzania wote pamoja na Walimwengu wapenda Amani limeacha msiba, simanzi, huzuni pamoja na majonzi makubwa hasa kwa Wana familia wa Vijana hao.

Akitoa nasaha mara baada ya Kisomo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Saeif Ali Iddi alisema upo umuhimu mkubwa kwa Jamii kuendelea kuwa na moyo wa subra wakati wanapopatwa na mitihani ili wazidi kuishi kwa Imani, Ushirikiano na upendo zaidi.

Balozi Seif alisema Muumba wa Dunia na vilivyomo ndani yake  ambae  ni Mwenyezi Muungu tayari ameshawabashiria mema na ya kheir wale wote waja wake walioamini na kupatwa na misiba na wakaamua kurejea kwake.

Amesema  Mkusanyiko wa Waumini na Wananchi katika kisomo hicho ulioweka pamoja waumini waliotoka Miji tofauti na Itikadi mbali mbali za Kisiasa pamoja na  madhehebu ya Dini ni dalili tosha ya kuonyesha mshikamano wa Jamii aliouamrisha Mwenyezi Muungu.

Balozi Seif ameeleza kwamba mahudhurio hayo ni kielelezo cha jinsi Taifa na Wananchi wake walivyoguswa na tukio hilo la msiba wa kuondokewa na wapenzi wao ambalo imani inaonyesha wazi kwamba halitosahaulika milele katika mioyo yao.

Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar aliishukuru Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar kwa jinsi inavyobuni mambo kadhaa yenye maslahi kwa Taifa likiwemo hilo la mkusanyiko huo wa ubunifu wa kuandaa dua hiyo ambalo ni jambo na kupongezwa.

Balozi Seif ameeleza  matarajio yake kwamba Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar itaendelea na jitihada zake za kuwaweka  pamoja Waumini wa Dini mbali mbali na kuahidi kwamba Serikali Kuu itahakikisha kwamba inaunga mkono na kuisaidia Kamati hiyo katika kutekeleza jukumu lake.

Amewasihi  Viongozi na Watendaji wa Kamati hiyo waendelee kuongeza jitihada katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya mapenzi ya Jinsia Moja, Ubakaji, Udhalilishaji wa Wananwake na Watoto pamoja na mambo mbali mbali yasiyo na maslahi kwa Taifa hili.

Akitoa salamu Mwakilishi wa Familia za Wafiwa wa Wanajeshi hao wa JWTZ Bw.Haji Hassan kwa niaba ya Familia hizo aliwashukuru Watanzania wote walioshirikiana na wafiwa hao katika msiba huo mkubwa.

Bw.Haji Hassan alisema msiba wa Wanajeshi hao 10 uliotokea Mnamo Tarehe 7 Disemba Mwaka 2017 Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ulikuwa wa Taifa zima jambo ambalo lilileta faraja kwa wana familia hao.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuwaaidhi Waumini walioshiriki Kisomo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Sheikh Salim Mohammed Al – Kadir amesema Kamati hiyo imeguswa na Msiba huo uliopelekea Uongozi wa Kamati hiyo kuandaa dua hiyo ili kuonyesha mapenzi kwa Wapiganaji hao

Sheikh Salim kwa niaba ya Uongozi wa Kamati yake  wameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano uloipa Kamati hiyo kuweza kutekeleza majukumu yake iliyopangiwa na Umma.


DK.MABODI : AMEWASISITIZA WANANCHI KUWAOMBEA DUA ASKARI WANAOUAWA WAKILINDA AMANI

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi ' akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya kumaliza Khitma na Dua za kuwaombea Askari wa JWTZ waliouawa nchini Kongo miezi ya hivi karibuni.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewasihi wananchi wa Tanzania   kuendelea kuwaombea Dua na visomo mbali mbali Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaouawa  wakilinda Amani katika nchini mbali mbali ikiwemo DRC Kongo.

Pia ameliomba Jeshi hilo pamoja na familia za ndugu wa marehemu Askari 10 waliofariki waliofariki siku za hivi karibuni wakilinda Amani Kongo, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Wito huo ameutoa leo mara baada ya kumalizika shughuli ya kisomo cha Khitma na Dua ya pamoja ya Arubaini ya kuwaombea marehemu hao iliyoandaliwa na Kamati ya Amani Kitaifa Zanzibar huko katika Msikiti wa Noor Muhammad (SAW) kwa Mchina Mwanzo Zanzibar.

Dk.Mabodi ameeleza kwamba Askari hao watakumbukwa daima kwa mchango wao wa kutetea na kulinda maisha ya Waafrika katika Nchi ya Kongo ambapo walikuwa wakiiwakikisha Tanzania kupitia Jeshi la Pamoja la Umoja wa Mataifa lililopo nchini humo kwa ajili ya kulinda Amani.

Aliwambia wananchi kuwa Mashujaa hao hakuna cha kuwalipa kwa sasa kwani wamepoteza uhai wao kutokana na uzalendo uliotukuka hivyo kilichobaki ni kuwaombea Dua wao Mwenyezi Mungu awapumzishe pahala pema peponi Amini na kuziombea familia zao ziendelee kuwa na subra.

Amefafanua kuwa msiba huo mzito ni sehemu ya Askari wa Majeshi mbali mbali ya Ulinzi na Usalama nchini wanaoendelea na kazi zao za kawaida wawe imara Kifkra na Kimwili bila kukata tamaa ili kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa Kituo kikuu cha Amani Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Akizungumzia matunda ya kulinda misingi ya Amani nchini Dk.Mabodi amesema ni kuwepo kwa maendeleo katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.

“Wananchi tulinde tunu ya Amani na Utulivu tuliokuwa nao katika Taifa letu, ili tuweze kuwa Mabalozi wazuri wa kulinda Amani kwa nchi jirani na Mataifa mengine.”, amesisitiza.

“Nawapongeza Kamati ya Amani ya Taifa Zanzibar kwa maandalizi yao mazuri ya kuandaa shughuli ya kuwaombea Dua kubwa kama hii vijana wetu waliouwawa na watu wanaosadikiwa kuwa Waasi huko Nchini Kongo.”, amesema Dk.Mabodi.

Aidha ameeleza kuwa wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa kuenzi Amani na Utulivu, uliopo nchini kwa lengo la kuepuka machafuko na migogoro isiyokuwa ya lazima nchini.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Hussein Mwinyi, amewashukru wananchi mbali mbali waliojitokeza katika Khitma hiyo kwa lengo la kuwaombea Dua Marehemu Askari hao.


Amesema licha ya Tanzania kuwapoteza Mashujaa hao bado Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) litaendelea kuwa imara na kulinda mipaka na kushiriki harakati mbali mbali za kulinda amani hata nje ya Tanzani kwa lengo la kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine Duniani.