RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizindua Soko la Tibirinzi lililopo Chakecheke Pemba.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein, amesema kuwa miongoni mwa malengo ya mapinduzi matukufu ya
mwaka 1964, ni kuzifanya hali za maisha ya wazanzibari kuwa bora.
Dk. Shein alieleza hayo huko Tibirinzi Chakechake, mara baada
ya kulizindua soko jipya la Tibirinzi, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za
kutimia miaka 54 ya mapinduzi.
Amesema ujenzi wa soko la Tibirinzi, umelenga kuinua maisha
ya wananchi sambamba na kujipatia mahitaji yao na kamwe lisitumike kama
kichocheo cha kubaguana misingi ya vyama, dini, jinsia au mahala mtu
anapotokea.
Amesisitiza kuwa jengo soko hilo jipya ni ukombozi kwa
wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na wananchi wote kwa
jumla kwa kuwaongezea kipato chao kitakachoimarisha maisha yao.
Amesema si vyema soko hilo likahusishwa na masuala ya kisiasa
kwani ni soko la watu wote wa vyama vyote, dini zote na jinsia zote huku
akiwataka wafanyabiashara watakaolitumia soko hilo kuleta bidhaa zenye ubora
zitakazolingana na hadhi ya soko hilo.
Ameeleza kuwa ujenzi
wa soko hilo ni katika hatua za kutafsiri mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo
kwa kuwaletea wananchi maendeleo zaidi bila ya ubaguzi.
Ametumia fursa hiyo
kueleza mafanikio sambamba na azma ya mapinduzi matukufu ya Januri 12, 1964
ambayo yamewakomboa wananchi wa Zanzibar na kukata minyororo ya chuki, udhalimu
na manyanyaso.
Ameeleza madhumuni ya
mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa huru hatua ambayo imepekea kupanga mambo bila ya
kuingiliwa na mtu na kuweza kuongoza nchi sambamba na kuandaa mipango ya muda
mrefu na muda mfupi na wakati.
Amesema kuwa Zanzibar imepata maendeleo makubwa katika kukuza
uchumi wake ndani ya kipindi cha miaka 54 huku akieleza kuwa mabadiliko makubwa
ya kiuchumi, sera ya serikali maisha ya watu ambayo yote hayo ni maendeleo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni