Alhamisi, 4 Januari 2018

JUMUIYA YA WAZAZI IPO TAYARI KUSIMAMIA MAADILI YA WATANZANIA

Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa akizungumza na wanachama wa CCM kupitia jumuiya hiyo
hapo katika Ukumbi wa CCM Amani

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), imesema tayari imeshaanza kufanyia kazi agizo la Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Dk.John Magufuli la kusimamia maadili ya watanzania ambapo yameonekana kuendelea kupotea.

Agizo hilo lilitolewa na Dk.Magufuli,mnamo 12 Desemba, mwaka 2017 katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa tisa wa uchaguzi wa jumuiya hiyo, mjini Dodoma, ambapo alisema jumuiya ya wazazi ina jukumu la kusimamia maadili ya nchi.

Katika ufunguzi huo wa mkutano mkuu wa jumuiya hiyo,Dk.Magufuli alieleza kuwa jumuiya hiyo ikiwa itazungumzia masuala hayo ya maadili itasaidia kuwakumbusha watanzania kutokuwa na tabia ya kuiga kila kitu kutoka nje kwa kuwa mengine hayaendani na tamaduni za nchi.

Hayo yalizungumzwa leo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk. Edmund Mndolwa alipowasili visiwani humu, wakati akizungumza na wanajumuia wa jumuiya,alisema hadi sasa tayari jumuiya hiyo inatarajia kuanza juhudi za kutekeleza agizo hilo ikiwemo kuanzisha kamati ndogo za elimu na maadili ndani ya jumuia hiyo.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kumekuwepo na mmomonyoko wa maadili maadili katika taifa hususan katika masuala la mavazi kwa upande wa kike na wa kiume na kwamba jumuia hiyo haitoweza tena kuvumbia macho.

"Nimewaomba wenzangu tuitafute ile hotuba tuifanyie kazi na Rais amekereka sana na kwetu sisi ni agizo halina mjadala ikiwa mkubwa amezungumza lazima tuitekeleze na kuhakikisha hiyo kero imemalizika,"alisema Mwenyekiti huyo.

Katika maelezo yake Dk.Mndolwa alisema Rais Magufuli amenungunika sana suala hilo la mmonyoko wa maadili hivyo ni amri katika jumuia hiyo kuhakikisha inasimamiwa kisasawa.

Alisema tayari amekwishaifanyia kazi kero hiyo ya mmomonyoko wa maadili ambayo ndio ina kera sana lakini ikiwa kama jumuia hiyo ni ya wazazi haipendezewi na suala hilo hususan la mavazi kwa wasanii.

"Jamani maadili ya watanzania yamepotea sisi kama jumuiya tumepewa kazi hii lazima tuifanye kwa bidii ni mfano mdogo ni kuwa vileo wa siku hizi wakimaliza kidato cha nne hawaajiliki kutokana na kutokuwa na maadili mema,"alisema

Dk.Mndolwa alisema suala la kusimamia maadili itaanzia katika shule za jumuia hizo ambapo suala hilo litafika hadi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na kuhakikisha somo la maadili linafundishwa mashuleni.

Alisema jumuia hiyo haitaishia hapo bali itaenda mbali zaidi kwa kuzungumza na makanisa na misikiti kusaidia kuhubiri maadili hadi vileo wafahamu nini maana ya maadili.

"Tutaanza kuandaa mifumo ya kisasa ikiwemo ya muda mrefu na muda mfupi kwa upande wa muda mifupi ni kwa ajili ya watoto wanaoingia masomo ya awali kuanzia la kwanza hadi la tatu katika mifumo ya muda mrefu ni kwa wale wakubwa kuwapeleka katika vikosi vya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) na kwa kuwa kule ndio kwenye maadili mazuri,"alisema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo,Haidar Abdllah, alisema suala la maadili ni jambo ambalo halina mjadala katika kutekeleza kutokana na kuwa ni agizo la Mwenyekiti wa Taifa Rais Magufuli.

Alisema agizo hilo ni wazi kuwa linagusa kwa namna moja ama nyingine katika jumuiya hiyo na kwamba lazima lifanyiwe kazi hivyo jumuia zote za ndani za chama zinapaswa kushirikiana na kusimamia mmomonyoko huo wa maadili katika jamii.

"Tunapanga pamoja na Mwenyekiti wangu nanishauriana nae vyema katika kutekeleza maagizo na utendaji wote wa jumuiya hii yetu sote tupo pamoja na safari yetu ni ndefu,"alisema Makamu Mwenyekiti huyo.

Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Wazazi,Seif Shaban Mohamed alisema ni jambo la kukumbusha na katika agizo la Rais la kusimamia na kuachiwa suala la mmomonyoko wa maadili.

Alisema lile ni agizo na lazima jumuiya hiyo kulifanyia kazi kwa hali na mali hivyo agizo hilo linapaswa kuchukuliwa kama kitendea kazi ndani ya jumuiya.

"Ninachotaka kusema ni kuwa jumuia ya wazazi vikao vyetu vyote tunavyokaa lazima ajenda ya maadili izungumzwe, tunafahamu kuwa kuwa mambo haya yapo katika jamii yetu na endapo tukiwa tunazungumzia masuala ya maadili kuanzia ngazi ya kata nina imani kuwa taifa letu litakuwa na maadili mazuri,"alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni