NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Seneti ya Unguja uliofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar. |
MWENYEKITI wa Shirikisho hilo aliyemaliza muda wake Khamis Kheri Ame akitoa nasaha zake katika mkutano huo. |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaagiza vijana wasomi wa Chama hicho kuanzisha
utamaduni wa kufanya Tafiti mbali mbali za kitaalamu ili kubaini baadhi ya
changamoto zinazokabili kundi la vijana na jamii kwa ujumala hasa upungufu wa ajira.
Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Mkutano wa Uchaguzi wa
Shirikisho la Vyuo vikuu CCM Unguja la kuwachagua viongozi Watano wa Seneti ya Unguja, ambapo Mkutano
huo umefanyika katika Afisi Kuu CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Dk.Mabodi alisema Wasomi wa Vyuo vikuu ndani ya CCM ni lazima
wakubali mabadiliko ya nyakati kwa kufanya kazi zao za kisiasa, kiuchumi na
kijamii katika mfumo wa Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuleta mabadiliko
chanya ndani ya taasisi hiyo imara ya Kisiasa.
Alisema nchi zilizoendelea duniani zinategemea msaada mkubwa
wa wasomi ambao ni vijana waliohitimu fani mbali mbali katika vyuo vikuu na
taasisi za elimu ya juu ambao wana uwezo na maarifa ya kitaalamu yanayochochea ufanisi wa
kimaendeleo.
Pia, aliongeza kwa kueleza kwamba CCM ina utajiri wa
Rasilimali watu waliobobea katika fani mbali mbali hivyo ni lazima watoe
mchango wao katika kuandaa mipango mikakati ya kukiletea chama hicho ushindi wa
kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2020.
Hata hivyo amesema vijana hao wa Vyuo vikuu wana wajibu wa
kusoma alama za nyakati kwa kuwa mfano bora wa kubuni na kutekeleza kwa vitendo
mikakati mbali mbali ya kiuchumi na kijamii ili vijana vya vyama vya upinzani
wavutiwe na utamaduni huo na kujiunga na hatimaye kujiunga na Chama cha
Mapinduzi.
Akizungumzia fursa zinazotokana na usimamizi pamoja na
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 alitaja mchakato wa
Utafiti wa Uchimbaji wa mafuta na Gesi Zanzibar
kuwa ni sehemu muhimu inayohitaji vijana wasomi watakaolinda rasilimali
hiyo isifilisiwe na nchi za kigeni.
Alisema fursa ya kuanza utafti huo ni miongoni mwa matunda ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964
chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume, aliyeasisi mfumo rasmi wa Zanzibar kujitawala kiuchumi, kisiasa
na kijamii.
“ Utafiti huu umeanza mwaka 1952 ambao ulibaini ndani ya
Ardhi na mwambao wa visiwa vya Zanzibar kuwepo kwa dalili za rasilimali hiyo
inayoingia katika kundi la madini asilia, na juhudi ziliandelea hadi kufikia Serikali
ya awamu ya saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Shein kupigania suala
hilo likapewa baraka za kisheria zilizoruhusu Zanzibar kushugulikia yenyewe mchakato wa utafiti hadi
uchimbaji”,. Alieleza Dk.Mabodi.
“ Nyinyi ni wasomi ambao jamii ya Wazanzibar na Watanzania
kwa ujumla wanakutegemeeni mlete mabadiliko ya kweli ndani ya Chama chetu na
Serikali zote mbili zinazotokana na CCM.
Lakini pia ni lazima muwe wabuni kwa kufanya utafiti ndani na nje ya CCM kwa
lengo la kupata takwimu sahihi za mambo
mbali mbali yatakayosaidia Chama kuimarika kisiasa kutokana na mingo
yake kutekelezwa Kisayansi.”, alisema.
Akizungumzia kwa ufupi historia ya Zanzibar Dk.Mabodi alisema kuwa maandiko mbali mbali
ya historia yanadhibitisha kuwa Zanzibar kabla ya kutawaliwa na Wakoloni
ilikuwa na Utawala wake wa jadi uliokuwa katika mfumo wa ujima, ambao wananchi
wake waliishi kwa amani , ujamaa na kujitegemea.
Alisema kupitia muongozo huo wa historia ni lazima vijana wa
sasa wajijue kuwa wana jukumu la kuhakikisha CCM iliyotokana na vyama vya ASP
na TANU inaendelea kutawala na hakuna Chama chochote cha upinzani
kitakachoshika madaraka.
Akizungumzia Uchaguzi
wa viongozi mbali mbali wa Shirikisho hilo alisema ni lazima wachague viongozi
bora wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa waliowachagua bila ya
kusukumwa.
Pamoja na hayo aliwasisitiza wajumbe wa Mkutano huo
kuhakikisha wanachagua wenye uwezo na uthubutu wa kujenga hoja imara na kujibu
hoja za wapinzani bila ya kuteteleka.
Aliwataka wasimamizi wa Uchaguzi huo kutenda haki bila ya
upendeleo wa mgombea yeyote ili kulinda heshima ya CCM na kuruhusui mkondo wa
Demokrasia ifanye kazi yake kwa mujibu wa miongozo na kanuni za uchaguzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita
alisema mafanikio yaliyopatikana Zanzibar katika sekta mbali mbali yametokana
na juhudi za kiutendaji na ushiriki wa
vijana wasomi wa Chama hicho.
Ametoa nasaha wa vijana hao kuwa ili kufikia malengo
waliojiwekea kisiasa ni lazima wafanye kazi
kwa bidii ili kukisaidia chama kufikia malengo yake ya kushika dola kila
uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo ndogo.
Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu wa vijana wa shirikisho
hilo la vijana wa CCM wa vyuo vikuu kusoma Katiba ya CCM pamojana na kanuni ya
UVCCM kwa lengo la kutambua wajibu,haki zao pamoja na mipaka yao kiutendaji.
Akitoa salamu za Mwenyekiti wa Umoja huo Kheri James, Tabia
alisema kuwa kiongozi huyo anawasihi waendelee kuwa wamoja kwa kila jambo jema
lenye malengo ya kuleta manufaa ndani ya CCM na Serikali zote mbili ya Zanzibar
na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mapema Mwenyekiti anayemaliza
muda wake katika Shirikisho hilo Khamis Kheri Ame alisema lengo la
uchaguzi huo ni kutimiza matakwa ya Kikatiba yanayoruhusu mabadiliko ya awamu
za uongozi kwa kila kipindi cha miaka mitatu.
Pamoja na hayo amewashukru wajumbe wa Shirikisho hilo
alioshirikiana nao kwa kipindi chote cha uongozi wake na kuwataka viongozi
wapya watakaochaguliwa kuhakikisha wanalivusha salama shirikisho hilo kuelekea
ng’ambo ya maendeleo endelevu.
Katika Uchaguzi huo wanachaguliwa viongozi mbali mbali
ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti, Katibu,
Katibu wa hamasa pamoja na wajumbe wawili wa Kamati ya Uratibu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni