Jumatatu, 8 Januari 2018

MNEC akabidhi msaada kwa UVCCM



NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Zahor Saleh Mohamed amekabidhi msaada wa vyakula kwa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM,(UVCCM) visiwani humu kwa ajili ya kufanikisha matembezi ya kuenzi Mapinduzi ambayo yanatarajiwa kufanyika leo. 

 Akikabidhi msaada huo ikiwemo maboski ya biskuti, pakiti za maji,magunia ya mchele, mbuzi wawili na kondoo mmoja, katika Ofisi ya UVCCM iliyoko Gymkana, Mjumbe huyo alisema msaada huo utasaidia jumuia hiyo katika shughuli hiyo ya kuyaenzi mapinduzi kutokana na kuwa suala hilo la mapinduzi hakuna namna lazima yaenziwe. Mohamed ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa ,aliongeza kuwa vijana ndio wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha yanaenziwa na kwamba lazima watanzania washirikiane kuyalinda mapinduzi hayo yaliotokea mwaka 1964.

"Nichotaka kusema kuwa hii ndio serikali ya mapinduzi na hakuna serikali nyingine na itaendelea kuwepo hadi mwisho ninachowashangaa baadhi ya watu wanasema kuna serikali nyingine wanajidanganya,"alisema Mjumbe huyo. Katika maelezo yake alisema baadhi ya watu hao wamezaliwa na wazazi wao na kulelewa, wamesomeshwa na wameoa ndani ya serikali ya mapinduzi jambo ambalo baadae wanajidanganya kuwa kutatokea serikali nyingine. 

 Aliwaomba watu hao kuachana na mambo hayo katika misingi ya kudanganywa na mtu mmoja ambaye kila siku anadai serikali nyingine inakuja na kwamba waje kushirikiana,kuunga na Serikali ya Mapinduzi pamoja na Chama Cha Mapinduzi. Kwa upande wake Naibu Katibu wa UVCCM, Zanzibar, Abdulghafar Idrissa, alishukuru kwa msaada huo na kwamba utasaidia sana katika kufanikisha matembezi hayo ya kuenzi mapinduzi. 

Alisema katika kufanikisha suala hilo na kwamba hata mapinduzi yenyewe ya mwaka 1964 yalishirikiana na watu hivyo hayakufanywa na mtu mmoja hivyo kwa msaada huo utasaidia kukamilisha matembezi hayo. "Kila mwaka katika kuyaenzi na kuyakumbuka mapinduzi yetu tunafanyaga matembezi sisi UVCCM na dhamira yetu kuonesha kwa vitendo kuwa vijana walishiriki katika kufanya mapinduzi,"alisema.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni