Alhamisi, 11 Januari 2018

DK.SHEIN AFUNGUA BARABARA YA CHEJU, JENDELE NA UNGUJA UKUU.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt,Ali Mohammed Shein akikata Utepe kuashiria Ufunguzi wa Barabara ya Jendele,Cheju na Unguja Ukuu Kaebona Wilaya ya Kati Unguja ,Ikiwa ni miongoni mwa Shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
  Barabara ya Jendele,Cheju hadi Unguja Ukuu yenye urefu wa Kilomita 13 iliofunguliwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein hafla iliofanyika Cheju Wilaya ya Kati Unguja ,Ikiwa ni miongoni mwa Shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya juhudi katika kuhakikisha inatumia wataalamu wake wazalendo katika kujenga barabara za hapa Zanzibar kwani hatua hiyo tayari imeanza kuzaa matunda. 

Dk. Shein alisema hayo leo mara baada ya ufunguzi wa barabara ya Jendele, Cheju hadi Unguja Ukuu ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 54 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964.

Dk. Shein alieleza kuwa vijana wa Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) wana utaalamu mkubwa lakini kinachowakwaza ni ukosefu wa vifaa pekee na kueleza kuwa ujenzi unaofanywa na mafundi wazalendo hupelekea kujenga barabara imara kwa fedha kidogo ikifananishwa na Kampuni za kutoka nje ya Zanzibar.

Alisisitiza haja ya kujitegemea katika kujenga barabara za hapa nchini na ndipo Serikali imeamua kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa ili kuendeleza shughuli hizo kwa ufanisi mzuri zaidi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kufanya mambo yake.

Dk. Shein aliongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mpango wa Serikali wa kujenga barabara hiyo na wala Serikali haijakurupuka kwani barabara hiyo itasaida katika usafirishaji wa mazao mbali mbali yakiwemo mpunga pamoja na bidhaa nyengine na wananchi.

Alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yameleta umoja na usawa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar na wala hayajambagua mtu kwa rangi yake, dini yake, kabila lake na yote yanayofanywa Unguja yanafanywa na Pemba, na yanayofanywa mjini hufanywa na vijijini.

Aidha, alieleza kuwa Serikali anayoiongoza haimbagui mtu na yote yanayofanywa yameanza kufanywa na Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu mzee Abeid Amani Karume na kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Serikali ya wananchi wote wa Zanzibar.

Alieleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo na kwa upande wa sekta za maendeleo Zanzibar imepiga hatua kubwa ikifananishwa na nchi nyengine za bara la Afrika.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara pamoja na Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) kwa kazi nzuri waliyoifanya pamoja na kufikiria haja ya kuongeza urefu wa barabara kwa urefu wa kilomita mbili zinazojumuisha mzunguko wa makutano ya barabara ili kuweka vizuri matumizi ya barabara hiyo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisisitiza usemi wa wazee kuwa “Subira huvuta heri” na “Baada ya dhiki faraja” kutokana na uvumilivu uliotokea baada ya kushindwa kwa Kampuni ya ujenzi iliyoanza kujenga Barabara hiyo.

Alieleza makubaliano yaliofikiwa kati ya Serikali na Benki ya  Maendeleo ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi ya Afrika (BADEA) kuwa Serikali ikamilishe ujenzi wa barabara hiyo ya Jendele-Cheju-Kaebona kwa kiwango cha lami kwa kutumia fedha zake za ndani na BADEA itaendelea kuifadhili barabara ya Koani-Jumbi kwa bakaa ya fedha zilizobakia kwa mujibu wa mkataba wa fedha baina ya Serikali na Benki ya (BADEA).

Dk. Shein alieleza madhumuni ya barabara ikiwa ni pamoja na kusafirisha mazao pamoja na bidhaa nyengine ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi kusafiri wao wenyewe kutoka sehemu moja kwenda nyengine.

Alisema kuwa hivi sasa Zanzibar ina mtandao mzuri wa barabara ikifananishwa na wakati kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964 ambapo baada ya hapo ndipo barabara nzuri zilipotengenezwa na kusisitiza kuwa kabla ya Mapinduzi hayo maeneo machache tu ndio yaliokuwa na barabara za lami.

Aidha, aliwaeleza wananchi haja ya kuzitumia barabara kwa maendeleo na kuwataka wananchi hao kuitunza  na kuienzi barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu huku akiwaeleza wananchi azma ya Serikali ya kuubadilisha mji wa Zanzibar kwa kujenga majengo sambamba na miji ya kisasa ndani yake.

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Abeid Karume alitoa shukurani kwa juhudi zake na ahadi zake sambamba na kuipa upendeleo Wizara yake ili iweze kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo sambamba na kuwapa miongozo na hatimae barabara hiyo imekamilika.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe akitoa maelezo ya kitaalamu  alisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni moja wapo ya jitihada ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua tokea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kujenga ustawi wa wananchi wake kwa kuimarisha na kuendeleza miundombinu ya barabara mijini na vijijini Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa tarehe 5 Aprili 2016 wakati wa uzinduzi wa Baraza za Tisa la Wawakilishi.

Aliongeza kuwa  ujenzi wa barabara hiyo ulianza rasmi mwezi Januari 2013 kwa lengo la kujengwa kwa barabara tatu kwa kiwango cha lami, barabara hizo ni pamoja na Barabara ya Koani-Jumbi kilomita 6.3 na Kizimbani-Kiboje kilomita 7.2 na ulitegemewa kuchukua muda wa miezi 17 hadi kukamilika kwakwe.

Alieleza kuwa mradi huo unafadhiliwa na Benki ya (BADEA) ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ulitarajiwa kugharimu TZS Bilioni 14.8 ambapo mradi huo ulianza kutekelezwa na Kampuni ya DB Shaprya kutoka Dar-es-Salaam na kusimamiwa na Kampuni ya Newtech Industrial Engineering Group kutoka Sudan ikishirikiana na Kampuni ya EM Consult ltd kutoka Tanzania.

Aidha, Katibu Jumbe alieleza kuwa Kampuni ya DB Shapriya ilishindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ambapo ilifikia asilimia 24 tu ya kazi yote aliyokabidhiwa kwa mujibu wa muda ulioanishwa katika Mkataba wa ujenzi wa barabara hizo licha ya kuongezewa miezi 13 aliyoomba lakini alishindwa kukamilisha na ndipo Wizara ilipovunja nae Mkataba.

Kutokana na hali hiyo Serikali iliamua kutumia wataalamu wake kutoka Idara ya Ujenzi na Utunzaji wa Barabara (UUB) ambapo kazi hiyo ilikamilika mwezi Julai, 2017 na kuitengeza barabara hiyo yenye kilomita 13 kwa kiwango cha lami.

Aliongeza kuwa hadi Julai 2017 jumla ya TZS Bilioni 6.1 zimetumika katika utekelezaji wake kwa kazi za ujenzi, kati ya fedha hizo jumla ya TZS Bilioni 3.7 ni kutoka BADEA na TZS Bilioni 2.4 ni kutoka Serikalini.

Katibu Jumbe alitoa shukurani kwa Dk. Shein ambapo Serikali anayoiongoza imetenga jumla ya TZS Bilioni 5.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Ujenzi wa barabara ikiwemo mtambo wa kupikia lami, gari la kutandaza lami iliyopikwa na gari la lami ya maji ili kuijengea uwezo Idara ya UUB pamoja na ununuzi wa tani 1,700 za lami kwa matumizi ya Unguja na Pemba.

Viongozi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo iliyokwenda sambamba na burudani iliyotolewa na vikundi vya ngoma za utamaduni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni