MAKAMU wa Rais Mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, akifungua barabara ya kilomita mbili ya Fuoni meli tano Kwarara, katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.
MAKAMU wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilali, amesema ujenzi wa barabara za mjini na vijijini ni miongoni mwa matokeo na juhudi zinazochukuliwa na serikali ya kuimarisha miundombinu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Aliyasena hayo wakati akizindua barabara ya Fuoni Kwarara yenye urefu wa kilomita 2.2 ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha mawasiliano baina ya watu wa mjini na vijijini na shughuli za maendeleo ikiwemo biashara na kilimo na wananchi kujipatia kipato.
Alisema barabara zinazojengwa, zilizokamilika na zinazoendelea kujengwa zitakuwa kichocheo cha kuinua uchumi wa nchi.
Alisema mapinduzi ya mwaka 1964 ndio yaliyotoa dira ya nini serikali inataka kufanya kwa wananchi wake na kuleta maendeleo muhimu ikiwemo afya, miundombinu ya barabara, elimu na maji safi na salama.
Aidha alisema wananchi wana kila sababu ya kuyaenzi na kuyathamini mapinduzi yao kwani ndio yaliyowakomboa wanyonge na kupata maendeleo.
“Msichoke kusema mapinduzi daima kila saa na dakika, tembeeni kifua mbele kuyatetea mapinduzi yenu kwani bila mapinduzi haya serikali isingetekeleza miradi hii muhimu kwa ajili ya sisi wananchi,” alisema
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii kwani uongozi wa awamu ya saba na ulioipita una ubunifu katika kusimamia miradi.
Aliwaomba wananchi kuitunza barabara hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kuwasihi madereva wanaoendesha vyombo vya moto kuwa waangalifu na kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali.
Nae Waziri wa Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji, Balozi Ali Karume, alisema ujenzi wa barabara unachangia uchumi wa nchi na kujenga ustawi wa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, Shomari Omar Shomari, alisema kutoka Fuoni hadi njia nne kilomita moja imejengwa na kampuni ya Mecco na kilomita 1.2 njia nne hadi skuli ya Kwarara imejengwa na UUB.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo umezingatia mahitaji muhimu ikiwemo kuweka kingo za kupitishia maji ya mvua ili kuzuia tatizo la kuharibika, michoro na alama za barabarani.
Zaidi ya shilingi milioni 750 zimetumika katika ujenzi huo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni