Jumamosi, 27 Januari 2018

BALOZI SEIF, RC-AYOUB NA DK.MABODI WATANGAZIA UMMA UMUHIMU WA KUCHANGIA DAMU


 BAADHI ya wananchi walioshiriki tamasha  la uchangiaji damu wakifuatilia matukio mbalimbali yanayoendelea kwenye maeneo ya Kumbukumbu ya Mnara wa miaka 50 ya  Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.
 NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika tamasha la uchangiaji wa damu iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini na Magharib, katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge.
 MKUU wa Mkoa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud akizungumzia lengo la Tamasha hilo la uchangiaji wa damu salama.
 MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd ambaye ni mgeni rasmi akihutubia katika Tamasha la uchangiaji wa damu salama kwa hiari.


   BAADHI ya waandaji wa tamasha la uchangiaji damu kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana (BIWO).
 NAIBU Katibu Mkuu wa Cha Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Mabodi mara baada ya kumaliza kuchangia damu katika tamasha hilo. KATIBU Msaidizi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), MKoa wa Magharib Suleiman Mzee Suleiman akichangia damu katika tamasha hilo la uchangiaji damu.

 MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd akikagua zoezi la uchangiaji wa damu katika tamasha hilo.


 KOPLO  Suleiman Ali kutoka Jeshi la Polisi Kituo cha Ng'ambo Zanzibar akichangia damu. 

 VIJANA wa Chuo cha Sanaa ya mchezo wa kujihami cha Chicago bulls kilichopo Kijangwani Zanzibar  wakiwa katika Tamasha hilo na kuonyesha uwezo wao wa kupamba na adui kwa kutumia viungo vya mwili wa binadamu bila kutumia silaha.
 VIJANA wa Mchezo wa sanaa ya kujihami kundi la Taikwando wakionyesha uwezo wao katika Tamasha hilo.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema suala la uchangiaji wa damu salama kwa hiari linagusa maisha ya wananchi wote.

Kauli hiyo ameitoa leo katika tamasha la uchangiaji wa damu salama lililofanyika leo katika Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulioko Kisonge, amesema mahitaji ya damu ni ya kila siku na kwamba kuna haja ya wananchi kuwa na uzalendo wa kujitolea kwa ajili ya maisha ya wengine.

Amesema bado kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wagumu kujitolea katika mambo mbali mbali ya kijamii likiwemo suala la kuchangia damu, hali ya kuwa manufaa ya zoezi hilo yanabeba maslahi ya wengi hasa pindi panapotokea mahitaji ya damu.

Balozi Seif ameeleza kuwa kitendo cha kuchangia damu kwa hiari kina thamani kubwa juu ya uhai wa maisha ya watu wanaopata ajali na Wajawazito wanaohitaji damu nyingi wakati wa matibabu.

" Utamaduni wa kuchangia damu tuuendeleze na mimi nachukua jukumu la kuwambia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi nao waandae Tamasha kama hili la kuchangia damu ili wawe sehemu ya kuokoa maisha wa wananchi wao na kupunguza vifo.", ameeleza Balozi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharib Ayuob Mohamed amesema bado zanzibar ina mahitaji makubwa ya damu kwani kasi ya matumizi yake ni kubwa kuliko kasi ya uchangiaji wa damu hiyo.

Ayoub amebainisha kuwa bado wananchi, taasisi za umma na binafsi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mkoa na Serikali kuu ili kubatikana damu kwa wingi itakayoweza kukidhi mahitaji yac huduma husika.

Akizungumza katika tamasha hilo Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewataka wananchi wa visiwani humu bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila kuwa na utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wenzao  husasan wanaopata ajali na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Naibu huyo Katibu Mkuu amesema nchi zilizoendelea na zinazoendelea zimekuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo vifaa tiba vya hospitalini, lakini wameshindwa kutengeneza damu ya binadamu kwa ajili ya matumizi ya kitiba

Pia, amewambia wananchi kuwa wanatakiwa kutambua kuwa hakuna nchi, kampuni wala kiwanda kinachotengeneza damu bali wananchi wenyewe ndio wanaotakiwa kuchangia damu zao ili ziokoe maisha ya watu wenye mahitaji ya damu hiyo”,.amesema Dk.Mabodi.

Akizungumzia faida ya utoaji wa damu kitaalamu amebainisaha kuwamba mtu anapotoa damu anapunguza vichocheo vya hasira pia damu inapotoka mwilini inatoa fursa ya kutengeneza damu nyingine mpya inayokuwa na uwezo mkubwa wa kiutendaji katika mzunguko wa damu mwilini.

Hata hivyo, ameeleza kuwa matukio ya ajali za aina mbalimbali pindi yanapotokea huku wa kina mama wajawazito wanaojifungua wanahitaji damu hiyo na kwamba lazima utamaduni wa kutoa damu upewe kipaumbele.

Naye Ofisa Uhamasishaji kutoka Mpango wa Damu   salama Zanzibar, Omar Said Omar amezipongeza taasisi   zilizoandaa tamasha hilo la kuchangia damu na kwamba  litasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.

Amesema  matarajio ya kitengo hicho ni kupata zaidi ya chupa za damu 1,000 ambazo kwa matumizi yake chupa moja utumika kwa watu watatu ambao wanaohitaji huduma za kimatibabu.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi, askari wa majeshi ya ulinzi na Idara maalum za SMZ pamoja na wananchi walioshiriki kuchangia damu  waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuwahamasisha wananchi wengine kujitokeza kuchangia damu.

Kwa upande wake Koplo Suleiman Ali kutoka kituo cha Jeshi la Polisi la Ng’ambo, amewashauri askari wwenzake  kuwa mstari wa mbele katika kuchangia damu kwa lengo la kuunga mkono kampeni za uchangiaji wa damu.

Naye Nassor Othman Mkaazi wa Kisauni Unguja, amesema kuwa yeye ni  mdau wa kuchangia damu kwa miaka sita na wakati mmoja kati ya familia yake wanapohitaji damu wanapata huduma hiyo bila tatizo.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni