RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ametangaza kuanzia Julai mwaka huu
serikali yake itaanza kutekeleza azma ya kurudisha utoaji wa elimu bure katika
shule za Sekondari ili kuendelea kutekeleza kwa vitendo shabaha ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya 12 Januari, 1964.
Amesema kuwa hatua hiyo
itahusisha elimu ya ngazi ya msingi hadi sekondari na kwamba katika kipindi cha
miaka 54 ya mapinduzi hayo SMZ inajivunia kuimarika kwa huduma za elimu ambapo
kabla ya Mapinduzi shule zilikuwa chache na zikitolewa kwa ubaguzi na zilikuwa
za kulipia.
Rais Dk.Shein alitangaza neema
hiyo wakati akihotubia wananchi katika sherehe za kuadhimisha miaka 54 ya
Mapinduzi kwenye uwanja wa Aman Karume,ambapo alisema kutokana na juhudi za
serikali ya SMZ sekta ya elimu imeendelea kuimarika huku shule za msingi
zikiongezeka mara saba.
Awali kabla ya kuhutubia, Rais,
Shein ambaye alikuwa ni mgeni rasmi aliingia katika uwanja huo saa 2:56 asubuhi
ambapo alipanda gari maalum la wazi na kupigiwa mizinga 21 ya heshima na kupata
fursa ya kukagua gwaride liloandaliwa katika sherehe hizo.
Kabla ya kuingia Dk.Shein,
alitanguliwa na Rais Dk.John Magufuli ambapo aliingia saa 2:35 asubuhi naye
alipata fursa ya kupanda jukwa maalum ambalo alipokea salamu za heshima kwa
ajili ya kukaribishwa katika sherehe hizo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na
viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi(CCM) wakiwemo Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar,
Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni Marais wa wastaafu
akiweo wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya pili Ali
Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar
wa awamu ya sita Aman Abedi Karume.
Sherehe hizo ziliambatana na
maandamano yaliyoandaliwa kutoka kwa wafanyakazi wa taasisi za serikali na
vyama vya siasa ambao walibeba mabango mbalimbali yalikuwa na ujumbe tofauti
tofauti iliolenga kusherekea madhimisho ya mapinduzi ya miaka 54.
Dk.Shein aliongeza kuwa kwa upande wa shule za
Sekondari zimeongezeka mara 53 huku idadi ya wanafunzi wa shule za Msingi na
sekondari zikiongezeka mara 14 kutoka wanafunzi 25,372 kwa mwaka 1963 hadi
wanafunzi 378,211 kwa mwaka 2017.
"Ni wazi kuwa baada ya
mapinduzi kufaulu tatizo ambalo walilotengeneza wakoloni kuwa watoto wa wafanyakai
na wakulima tusiingie sekondari na kupata elimu ya juu, leo halipo tena na kwamba haya ni mafanikio
makubwa yakupigiwa mfano,"alisema.
Alitaja juhudi za serikali ya SMZ
katika sekta hiyo ya elimu kuwa katika jitihada za kuhakikisha inaongeza madarasa
kwa mwaka 2017 serikali yake ilianza ujenzi wa shule 9 za ghorofa za sekondari
kwa Unguja na Pemba.
Rais Dk.Shein alisema pamoja na
hatua hzio serikali yake imeendelea kushughulikia suala la ununuzi wa madawati
yote kw ajili ya shule zote za Unguja na Pemba hivyo kutokana na hatua
zinachukuliwa katika kukusanya fedha inatarajiwa tatizo la uhaba wa madawati
kumalizika mwaka huu.
"Mipango yetu ya elimu
imepata mafanikio makubwa ambapo sasa Zanzibar ina vyuo vikuu vitatu
vinavyoendeshwa na wataalamu wetu wenyewe ambapo wanafunzi 1,800 wa fani
mbalimbali wanahitimu kwenye vyuo vikuu visiwani humu kila mwaka kwa hivyo
Zanzibar itajitosheleza kwa kuwa na wataalamu wake wenyewe hivi karibuni,"
alisema.
Mbali na hilo, Rais Dk.Shein aliongeza kuwa
serikali yake ya SMZ imechukua juhudi kubwa za makusudi katika kuimarisha
huduma za afya ambapo sera mpya ya afya ya mwaka 2014 inatekelezwa katika
kuwapa wananchi huduma hizo bila ya malipo kutokana na malengo ya Mapinduzi.
"Hivi sasa huduma za afya
zinatolewa katika hospitali za serikali 12 baadala ya hospitali 5 na vituo vya afaya 158, badala ya
36 vilivyokuwepo kabla ya mapinduzi na vilevile huduma za afya zinatolewa na
hospitali za vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Idara ya Maalum za SMZ,
mpango ambao kabla ya mapinduzi haukuwepo,"alisema Dk.Shein
Rais Dk.Shein aliendelea kueleza
namna katika kipindi cha miaka 54 ya mapinduzi hayo serikali ya SMZ
inavyojivunia ambapo mafanikio katika sekta hiyo ya afya imeendelea kuimarika
ikiwemo ununuzi na upatikanaji wadawa na vifaa tiba.
Alisema katika kipindi cha mwaka
wa fedha 2016/2017 serikali yake ya SMZ ilitenga sh.bilioni 4.9 kwa ajili ya
ununuzi wa dawa na vifaa tiba ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018
serikali imetenga sh.bilioni 7 na hivyo kwa zaidi ya hayo kwa mwaka wa fedha
2018/2019 imetenga bajeti ya jumla ya wizara ya afya sh.bilioni 12.
"Katika kujivunia mafanikio
yaliopatikana katika kipindi cha miaka 54 ya mapinduzi serikali ya SMZ
imeendelea kutambua umuhumi wa kilimo ambapo wakulima wamepatiwa ruzuku ya
asilimia 75 ya pembejeo na huduma za matrekta hivyo hatua hiyo imepekea mavuno
ya mpunga kuongezeka kutoka tani 33,655.06 za mpunga kwa mwaka 2013 hadi tani
39,000 kwa mwaka 2017,"alisema.
Katika hotuba yake Rais Shein
alitumia fursa ya kumpongeza Rais Dk.Magufuli katika jitihada zake za kuingoza
Tanzania katika kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, uhujumu uchumi, dawa
za kulevya na kulinda rasilimali na kwamba kila mtu ana wajibu wa kumuunga
mkono.
Alisema Serikali ya SMZ
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika kuendeleza na
kuimarisha Muungano katika kushirikiana kwenye mambo yasiokuwa ya Muungano kwa
faida ya pande zote mbili.
"Mimi na Mwenzangu Rai
Dk.Magufuli tunatambua dhamana tulionayo katika kuhakikisha kuwa muungano wa
Tanzania unadumu na unaimarika kwa dhamira ile ile ya viongozi wetu wa awamu
zilizotangulia hivyo ninawahakikishia wananchi kuwa serikali zetu hizi mbili
zitaendelea kuchukua hatua ili nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na
ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu,"alisema Rais Dk.Shein.
alieleza kuwa katika kuwahudumia
wakulima visiwani humo kwa msimu wa mwaka 2017/2018 tani 1,800 za mbolea, tani
350 za mbegu ya mpunga na lita 15,000 za dawa za kuulia magugu zimenunuliwa na
zinatarajiwa kusambazaw kwa wakulima hao.
"Pia katika kuhakikisha kuwa
huduma za matrekta zinakua za uhakika visiwani humu serikali imeanzisha wakala
wa serikali wa huduma za Matrekta na zana nyinginezo za kilimo ambapo mbali na
matrekta ya zamani yaliopo kwenye kiwanda cha matrekta, SMZ imetiliana saini
hati ya maelewano na kampuni ya Mahindra Mahindra ya India ya kununua matrekta
100 na matrekta 20 kutoka kampuni ya Mahindra Mahindra tayari
yamekwishaagizwa,"alisema Rais Dk.Shein.
Pia, aliongeza kuwa serikali yake
imeanzisha kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki kilichopo Beit el Raas kwa
kushirikiana na serikali ya Japan na FAO chenye uwezo wa kuzalisha vifaranga
milioni 10 kwa mwaka.
"Aidha, serikali ya SMZ
imeanzisha kampuni ya uvuvi ya Zanzibar(ZAFICO) kwa mtaji wa sh.bilioni 7
ambapo imeamua kununua meli mbili za uvuvi kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo
ya uvuvi visiwani humo,"alisema.
Rais Dk.Shein alisema katika
mwaka wa tatu wa kipindi cha pili cha mwaka 2017/2018 cha awamu ya saba
serikali ya SMZ imetekeleza vyema ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), ya uchaguzi wa mwaka 2015-2020, MKUZA 3, na
dira ya Maendeleo 2020 na hivyo kupata mafanikio ya kuridhisha.
Alisema juhudi kubwa
zilizochukuliwa na serikali ya SMZ katika kuimarisha uchumi zimewezesha
kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambapo sh.bilioni 548.571 zilikusanywa
katika mwaka 2017 ikilinganishwa na sh.bilioni 487.474 kwa mwaka 2016.
"Katika mwaka 2017 mapato
yameongezeka kwa sh.bilioni 61.097 ikilinganishwa na makusanyo ya
ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2016 ikiwa sawa na ongezeko la asilimia
12.5 hivyo natoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato
Zanzibar(ZRB) za juhudi za ukusanyaji wa mapato"alisema.
Pia, alisema katika sekta ya
utalii imeendelea kuimarika ambapo watalii 433,116 waliingia visiwani humo,
katika mwaka 2017 ikilinganishwa na idadi ya watalii 379,242 waliongia katika
kipindi cha mwaka 2016 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.2.
"kuongezeka kwa idadi ya
watalii visiwani humu inaonesha wazi kuwa lengo la kufikia watalii 500,000
ifikapo mwaka 2020 litafananikiwa kabla ya mwaka huo na kwamba kwa upande wa
biashara kati ya Zanzibar na Tanzania bara inaendelea vizuri ambapo bidhaa
zenye thamani ya sh.bilioni 32.32 zilisafirishwa kwenda Tanzania bara na bidhaa
zenye thamani ya sh.bilioni 184.84 zilisafirishwa kutoka Tanzaia bara kuja
Zanzibar kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2017,"alisema Rais
Shein.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni