Jumapili, 7 Januari 2018

DK.SHEIN ATEKELEZA AHADI YA FUNDO.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiwahutubia wananchi wa Kisiwa cha Fundo mara baada ya kuzindua Mradi wa nishati ya Umeme Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali imejidhatiti kufikisha huduma za umeme katika maeneo yote wanayoishi wananchi kutokana na kutambua kuwa huduma hiyo inakwenda sambamba na maendeleo.
Dk. Shein ameyasema hayo jana mara baada ya kuzindua umeme katika kisiwa cha Fundo kilichopo mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kutimiza miaka 54 ya mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa ukosefu wa huduma hizo hudumaza juhudi za wananchi katika kujitafutia maendeleo na kwamba umeme katika dunia ya sasa sio anasa bali msingi wa maendeleo

Amewataka wananchi wa kisiwa hicho kuongeza kasi, ari na hamasa ya kutafuta maendeleo kwa kujishughulisha na miradi ambayo hapo awali haikuwezekana kutokana na kutokuwa na nishati hiyo.

“Ni jambo la faraja kuona kwamba tumepiga hatua kubwa kufikisha huduma muhimu katika visiwa vidogo vidogo na vijiji vilivyo katika maeneo ya mbali, kwani lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi wa Zanzibar anapata huduma za umeme, afya, elimu, maji safi na salama na huduma nyenginezo”,amesema Dk. Shein.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira na Shirika la Umeme kwa kuwa wepesi wa kutekeleza maagizo ya kusimamia vyema ilani ya CCM ya uchaguzi.

Ameeleza  kufurahishwa kwa kuwepo wataalamu wa hapa Zanzibar ambao wamefanya kazi hiyo kutokana na ujuzi wao na uwezo wa kuufikisha umeme kwenye visiwa kwa kuzipitisha nyaya za umeme chini ya bahari.

Amewapongeza wananchi wote wa kisiwa cha Fundo kwa kushirikiana na ZECO tangu hatua za mwanzo za utekelezaji wa mradi huo hadi pale umeme ulipoanza kuwaka pamoja na ukarimu na mashirikiano walioyonayo na umoja wao.

Dk. Shein ameongeza  kuwa yeye anapotoa ahadi kwa wananchi huwa hasahau kwani anakumbuka wakati akiwa katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010 akiwa Chanjani Chokocho katika uwanja wa “Black Wizard” aliahidi kuwa kisiwa cha Makongwe na Kisiwa Panza ataufikisha umeme ahadi ambayo tayari ameshaitekeleza.

Ameeleza  kuwa hivi sasa Serikali imeshafikisha umeme katika visiwa saba vya Zanzibar ambapo visiwa hivyo ni Tumbatu na Uzi kwa upande wa Unguja na Kojani, Kisiwa Panza, Makongwe, Mwambe Shamiani na Fundo kwa upande wa Pemba.

Dk. Shein amesema kuwa hivi sasa serikali inaendelea na visiwa vitatu vilivyobaki ambavyo ni Uvinje, Kokota na Njau vyote vipo Pemba ambapo serikali imejipanga kufikisha umeme katika visiwa hivyo kabla ya kumalizika mwaka 2020.

Sambamba na hayo, Dk. Shein amewaeleza  wananchi wa kisiwa cha Fundo kuwa ameliona tatizo la usafiri wa bahari wanaoupata wananchi wa kisiwa hicho na kuahidi kuwa serikali italitafuatia muwarubaini wa tatizo hilo.

“Umeme huu ni wa kweli na sio umeme feki … natoa pongezi kwa ZECO kwa kuwakopesha wananchi hawa umeme pamoja na kuwapunguzia malipo ya kuwaungia umeme, nasema ahsanteni sana”, amesema Dk. Shein.

Nae Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib alimpongeza Dk. Shein kwa kuwa makini katika kutekeleza ahadi anazoziahidi kwa wananchi huku akieleza mashirikiano makubwa yaliopatikana kutoka kwa wananchi.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Alhalil Mirza, ameeleza  kuwa mradi huo wa usambazaji wa umeme umehusisha ujenzi wa njia kuu za umeme wa kilovolti 33 kutoka Ukunjwi hadi Ras Ukunjwi na pia ndani ya kisiwa cha Fundo wenye jumla ya kilomita 7.29.

Uwekaji wa transfoma nne katika vijiji vya Kimeleani, Ngagu, Ndooni na Mabaoni, ujenzi wa njia ndogo za umeme zenye jumla ya kilomita 8 na ulazaji wa waya wa bahari wenye urefu wa kilomita 2.5.

Ameongeza  kuwa mradi huo umegharamiwa na Sarikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa shilingi bilioni 2,078,222,518 ambapo kati ya fedha hizo serikali imetoa bilioni 1.7 na ZECO imechangia milioni 302.2

Amesema kuwa kazi ya ujenzi wa umeme mkubwa, umeme mdogo na uwekaji wa transfoma zilimalizika mwezi Aprili, 2017 na kazi ya ulazaji wa waya baharini ilimalizika tarehe 6 Agosti 2017 na kumalizika Agosti 11 mwaka jana.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa kazi zote za upelekeaji wa umeme kisiwani humo zimefanywa na kusimamiwa na wataalamu wazalendo wa ZECO huku akieleza kuwa tayari nyumba 340 kati ya nyumba 640 zimeshatiwa umeme kisiwani humo.

Amefafanua  kuwa katika kufikia malengo ya dira 2020 na MKUZA III, serikali kupitia ZECO imeshafikisha huduma ya umeme kwa asilimia 100 kwa shehia zote za Unguja na Pemba ambapo ni sawa na asilimia 91 kwa ngazi ya Vitongoji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni