Jumapili, 21 Januari 2018

TABIA: AMESISITIZA MAADILI KWA VIJANA.


 MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Viongozi wa Shirikisho la Vyuo vikuu CCM Seneti ya Unguja uliofanyika Kisiwandui.

 Aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kupitia Mkutano Mkuu wa 9 wa Uchaguzi wa Umoja huo  Thuwaiba  Pandu akitoa neno la shukrani kwa waalikwa katika  Mkutano huo.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


MAKAMU Mwenyekiti wa  UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita amewataka vijana waliopo katika Vyuo Vikuu kuwa mfano bora wa kulinda maadili na utamaduni wa nchi.

Rai hiyo ameitoa wakati akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu  Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma  Saadalla ‘Mabodi’ katika ufunguzi wa Mkutano  Mkuu wa Uchaguzi  wa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM Seneti  ya Unguja.

Alisema kuna baadhi ya vijana wa Vyuo Vikuu wamekuwa mstari wa mbele kuvunja maadili kwa kushiriki katika vikundi viovu vya matumizi ya dawa za kulevya  pamoja na vitendo vya uzinzi vinavyopelelekea maambukizo ya maradhi ya Ukimwi.

Alisema kwa mujibu wa takwimu mbali mbali za kitaalam kutoka Wizara ya Afya nchini zinaonyesha vijana wengi wameambukizwa  VVU hali inayotakiwa kila kijana kujitadhimini na kuchukua tahadhali kubwa juu ya Afya yake.

Tabia alieleza kuwa bila ya wasomi nchi haiwezi kupiga hatua yoyote ya maendeleo badala yake panaweza kutokea madhara ya nchi kutawaliwa kifikra na wageni.

 Pia , aliwasihi vijana wa Shirikisho hilo kujifunza mambo mbali mbali ya historia ya siasa za Zanzibar pamoja na Itikadi na misingi ya CCM kiuongozi na kiutawala ili waweze  kufahamu majukumu ya msingi ya Chama na Jumuiya zake.

Akizungumzia  Umoja na mshikamano, Tabia alisema UVCCM itakuwa imara endapo viongozi wake wataendeleza utaratibu mzuri wa kushirikiana na vijana wa makundi mbali mbali yaliyopo katika jamii kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa wakati.

Makamu Mwenyekiti huyo aliwambia vijana hao kuwa Uchaguzi ndani ya Chama umekwisha na kwa sasa kilichobaki kwa viongozi waliopo madarakani ndani ya UVCCM ni kufanya kazi kwa ushirikiano ili Chama cha Mapinduzi kiweze kupata ushindi katika harakati mbali za Uchaguzi wa Dola.

“ Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,,,tusikubali vijana wenzagu kuwa dhaifu ndani nan je ya jumuiya yetu ni lazima tuwe wamoja kwa kuepuka majungu na fitna zisizokuwa na msingi wa kuleta maendeleo ndani ya Jumuiya yetu.

Lazima tukubali mabadiliko ndani na ndani ya Jumuiya yetu kwa kuacha utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea kwani viongozi wetu ambao ni  Mwenyekiti wa  CCM Taifa Dkt.Magufuli pamoja na Makamu Mwenyeti wa CCM Zanzibar Dk.Shein,,wanakesha wakiangaika kwa ajili yetu naomba nasi tusiwaangushe bali tuwaunge mkono”,.alisisitiza Tabia.

Pamoja na hayo alisema kila kijana ndani ya UVCCM ana haki ya kushiriki katika harakati mbali mbali za kisiasa bila ya kuwekewa vikwazo wala mizengwe kwani taasisi hiyo inaongozwa kwa misingi ya Kikatiba.

Aliongeza kuwa huu ni wakati wa vijana kutumia vizuri muda wao kwa kuzitumia vizuri fursa zilizomo katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kwa kutafuta nafasi za kujiendeleza kimasomo nje ya nchi pamoja na ujasiria mali katika mitandao ili kujiongezea kipato.
“ Nasaha kwenu tutumie muda mwingi kuombeana mema na kuonyeshana fursa za maendeleo kuliko kushambuliana wenyewe kwa wenyewe mitandaoni  badala ya kuelekeza nguvu hizo kwa wapinzani”,.alifafanua Tabia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Shirikisho hilo Mwanasiasa  kijana ambaye ni mwanaharakati na diwani wa kuteuliwa  Thuiwaba  Pandu ,alisema Chama cha Mapinduzi ni kinara wa kuwalea vijana wake katika misingi na malezi mema.

Alieleza kuwa Vijana wa shirikisho hilo watayafanyia kazi maelekezo  na maagizo mbali mbali yaliyotolewa na viongozi wa  CCM na UVCCM.


Pamoja na hayo amekiomba Chama kuzishauri Serikali zote mbili ya Zanzibar pamoja  na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuandaa utaratibu wa kutoa kipaumbele cha kuwaajiri vijana mbali mbali wa CCM ambao wana sifa ili kupunguza wimbi la upungufu wa ajira kwa kundi hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni