Ijumaa, 26 Januari 2018

THUWAYBA: AWATEMBELEA VIONGOZI WA ZAMANI WA UWT


 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi.

MAKAMU Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi(UWT),Thuwayba Kisasi, amewasihi  viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kuendelea kutoa maoni na ushauri mbali mbali utakosaidia kuimarisha taasisi hiyo kisiasa, kiutendaji na kiuongozi.

Nasaha hizo amezitoa wakati alipowatembelea viongozi wa zamani wa jumuiya hiyo kwa lengo la kupata ushauri unaotokana na uzoefu wao wa kiutendaji kisiasa pamoja na mambo mengine ya kijamii na kiuchumi.

Viongozi waliotembelewa ni pamoja na  Bi. Fatma Mbarouk, Bi. Fatuma Theresa,  Bi. Asha Mwinyi, Bi. Salma Yusuph, Bi. Mwantantu Yusuph Shaaly  pamoja na Bi. Johari Yusuph Khatib.

Akizungumza mara baada ya kuwatembelea Makamu Mwenyekiti huyo amesema bado jumuiya hiyo inathamini juhudi za viongozi na watendaji hao waliowahi kuongoza taasisi hiyo kwa mafanikio makubwa.

Makamu huyo amesema licha ya kupata michango yao na kuelekeza ni kwa namna gani viongozi wa sasa wataongoza tasisi hiyo pia aliongeza kuwa suala la kuwajulia hali zao viongozi hao ni sehemu ya utamaduni unaotakiwa kuendelezwa na viongozi wengine.

Katika maelezo yake Thuwayba aliongeza kuwa haitaishia hapo kuwatembelea viongozi hao wa jumuiya hiyo ambapo UWT itaendelea kuwawekea kipaumbele bila kuchoka.

"Nimejifunza mengi kutoka kwa viongozi wetu wastaafu na wametushauri kuwa tuendelee  kushikamana, tupendane na kufanya kazi zetu kwa bidii.,"alifafanua  Makamu huyo.

Aliongeza kuwa viongozi hao wameshauri jumuiya hiyo iwe na Umoja, nguvu na kutoyumba kwa namna moja ama nyingine na kwamba kufanya hivyo UWT itakuwa imara.

Naye miongoni mwa viongozi hao waliotembelewa Bi. Johari Yusuph Khatib, aliwataka UWT kuwa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Serikali zote mbili kwa lengo la kupata uzoefu mbali mbali wa masuala ya uongozi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni