NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewasihi wananchi wa Tanzania kuendelea kuwaombea Dua na visomo mbali mbali Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wanaouawa wakilinda Amani katika nchini mbali mbali ikiwemo DRC Kongo.
Pia ameliomba Jeshi hilo pamoja na familia za ndugu wa marehemu Askari 10 waliofariki waliofariki siku za hivi karibuni wakilinda Amani Kongo, kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Wito huo ameutoa leo mara baada ya kumalizika shughuli ya
kisomo cha Khitma na Dua ya pamoja ya Arubaini ya kuwaombea marehemu hao iliyoandaliwa
na Kamati ya Amani Kitaifa Zanzibar huko katika Msikiti wa Noor Muhammad (SAW)
kwa Mchina Mwanzo Zanzibar.
Dk.Mabodi ameeleza kwamba Askari hao watakumbukwa daima kwa
mchango wao wa kutetea na kulinda maisha ya Waafrika katika Nchi ya Kongo ambapo
walikuwa wakiiwakikisha Tanzania kupitia Jeshi la Pamoja la Umoja wa Mataifa
lililopo nchini humo kwa ajili ya kulinda Amani.
Aliwambia wananchi kuwa Mashujaa hao hakuna cha kuwalipa kwa
sasa kwani wamepoteza uhai wao kutokana na uzalendo uliotukuka hivyo
kilichobaki ni kuwaombea Dua wao Mwenyezi Mungu awapumzishe pahala pema peponi
Amini na kuziombea familia zao ziendelee kuwa na subra.
Amefafanua kuwa msiba huo mzito ni sehemu ya Askari wa
Majeshi mbali mbali ya Ulinzi na Usalama nchini wanaoendelea na kazi zao za
kawaida wawe imara Kifkra na Kimwili bila kukata tamaa ili kuhakikisha Tanzania
inabaki kuwa Kituo kikuu cha Amani Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
Akizungumzia matunda ya kulinda misingi ya Amani nchini
Dk.Mabodi amesema ni kuwepo kwa maendeleo katika Nyanja mbali mbali za
Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.
“Wananchi tulinde tunu ya Amani na Utulivu tuliokuwa nao
katika Taifa letu, ili tuweze kuwa Mabalozi wazuri wa kulinda Amani kwa nchi
jirani na Mataifa mengine.”, amesisitiza.
“Nawapongeza Kamati ya Amani ya Taifa Zanzibar kwa maandalizi
yao mazuri ya kuandaa shughuli ya kuwaombea Dua kubwa kama hii vijana wetu
waliouwawa na watu wanaosadikiwa kuwa Waasi huko Nchini Kongo.”, amesema
Dk.Mabodi.
Aidha ameeleza kuwa wananchi wanatakiwa kujenga utamaduni wa
kuenzi Amani na Utulivu, uliopo nchini kwa lengo la kuepuka machafuko na
migogoro isiyokuwa ya lazima nchini.
Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dk.Hussein Mwinyi, amewashukru wananchi mbali mbali
waliojitokeza katika Khitma hiyo kwa lengo la kuwaombea Dua Marehemu Askari
hao.
Amesema licha ya Tanzania kuwapoteza Mashujaa hao bado Jeshi
la Wananchi Tanzania (JWTZ) litaendelea kuwa imara na kulinda mipaka na kushiriki
harakati mbali mbali za kulinda amani hata nje ya Tanzani kwa lengo la
kudumisha mahusiano mema na nchi nyingine Duniani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni