Jumapili, 14 Januari 2018

THUWAIBA: AMESISITIZA TAKWIMU SAHIHI ZA WANACHAMA.

 MAKAMU Mwenyekiti wa  UWT Taifa Bi.Thuwaiba Kisasi akizungumza na wanawake wa Umoja huo katika Mikoa ya Mjini na Magharibi Unguja katika mwendelezo wa ziara yake visiwani Zanzibar.(PICHA NA ABEID MACHANO)

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

VIONGOZI na watendaji mbali mbali wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) wametakiwa kukusanya taarifa na takwimu sahihi za wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Umoja huo kwa lengo la kupata wanachama wa uhakika watakaoleta ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020.

Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Thuwaiba Kisasi wakati akizungumza na wanawake wa umoja huo wa Mikoa ya Mjini na Magharibi Zanzibar huko katika ukumbi wa Mkoa Mjini uliopo Amani, amesema ili CCM ishinde kwa kishindo katika Chaguzi mbali mbali za dola ni lazima kuwepo na mfumo rasmi wenye takwimu sahihi za wanachama hai.

Alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kinakabiliwa na changamoto zisizokuwa za lazima kwa baadhi ya uchaguzi mbali mbali uliopita kutokana na kuwepo kwa tabia chafu za baadhi ya watendaji kupotosha takwimu,hali inayopelekea kuwepo kwa wanachama ambao sio halisi.

“Hatutowavumilia baadhi ya watendaji ambao wanapotosha takwimu za wanachama wetu kwa kusudi ama kutumiwa na baadhi ya watu wengine kwa maslahi yao binafsi lazima tuwe waadilifu na wenye kuipenda jumuiya na Chama chetu kwa ujumla.

Kitendo cha kupotosha takwimu ni sawa na kukisaliti chama chetu na kupelekea kitumie nguvu nyingi wakati wa uchaguzi hali ya kuwa tuna rasilimali kubwa ya wanachama wanaokipenda na kukiunga mkono chama chetu”, amesema Makamu Mwenyekiti huyo na kuwasisitiza viongozi na watendaji wa UWT kuanzia ngazi za mashina hadi taifa kuhakikisha wanaratibu takwimu sahihi za wanachama hai hasa wapya wanaojiunga na chama hicho.

Pia alieleza kuwa Chama cha Mapinduzi kwa sasa kipo katika utaratibu mzuri wa kuanzisha mfumo wa kisasa wa kadi za wanachama za Kielectoniki zitakazokuwa na taarifa zote za mwanachama kwa lengo la kurahisisha masuala mbali mbali ya kiutendaji ndani taasisi hiyo.

Alifafanua kwamba kupitia kadi hizo itakuwa rahisi kupata taarifa za wanachama hasa wa UWT ili iwe rahisi kuwapatia mikopo mbali mbali kupitia vikundi vyao vya ujasiriamali na fursa zingine zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe.

Kupitia mkutano huo ambo ni mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Makamu Mwenyekiti huyo yenye lengo la kuwashukru wanawake wa Umoja huo kwa busara zao za kumchagua kwa kura nyingi katika  uchaguzi wa UWT ngazi ya taifa pamoja na kukumbushana utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya kiutendaji ndani ya umoja huo.

Pia liwambia  Akina Mama hao kuwa uchaguzi umekwisha hivyo makundi yaliyoundwa wakati wa vuguvugu la uchaguzi yavunjwe na badala yake washikamane kwa mustakabali wa maendeleo ya umoja huo na CCM kwa ujumla.

“ Tunashukru katika uchaguzi wa jumuiya zetu hazikutokea figisufigisu kama zilizotokea kwa baadhi ya uchaguzi wa jumuiya za wenzetu hivyo tusirudi nyuma bali tupendane, tushirikiane na kushauriana mambo mema yatakayoimarisha UWT kwa maslahi ya wanawake wote wa Tanzania.”, alieleza Thuiwaba.

Akizungumzia mikakati ya kiutendaji ya umoja huo kuwa ni pamoja na kuwapatia viongozi, watendaji na wanachama wa ngazi mbali mbali mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Naye Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Bi. Tunu Kondo amesema UWT  kwa Zanzibar imejipanga vizuri katika kwenda sambamba na mabadiliko mbali mbali ya kiutendaji yanayotokea katika chama na umoja huo.

Aliahidi kuwa maagizo mbali mbali yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti kwa upande wa Umoja huo yatatekelezwa kwa wakati mwafaka huku wakiendelea kufanya kazi kwa kasi,uadilifu na ufanisi wa hali ya juu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UWT anayefanyia kazi zake Tanzania bara, Eva Kiwele Mwingizi ameeleza kufurahishwa kwake na ari na hamasa za kiutendaji za wanawake wa Umoja huo katika Mikoa mbali mbali Zanzibar na  kueleza kuwa hiyo ni ishara ya mafanikio.

Amesema huu ndio wakati wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania nzima kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kiamendeleo, kijamii na kisiasa kwa lengo la kuidhibitishia dunia kuwa wanawake ni wachapakazi na sio watu wa kukaa ndani tu bila kufanya kazi.

Katika mwendelezo wa ziara hiyo Makamu Mwenyekiti huyo jioni ya leo atakuwa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni