Ijumaa, 19 Januari 2018

DK.MABODI AMECHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA BARAZA LA VYAMA VYA SIASA TANZANIA

NA IS-HAKA OMAR, DAR ES SAALAM.

 MAKAMU Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania Dk.Abdalla Juma Saadalla 'Mabodi'

BARAZA la Vyama vya Siasa Tanzania limekutana jana Januari 18, 2018 pamoja na mambo mengine wajumbe wa Baraza hilo wamemchagua na kumthibitisha Makamu Mwenyekiti  mpya Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi'.

Mara baada ya Baraza hilo kumthibitisha Dk.Mabodi ameahidi kusimamia mshikamano wa Kitaifa, kulinda utamaduni wa maridhiano ya kisiasa sambamba na kuheshimu tunu za kitaifa kwa lengo la kuenzi dhana ya demokrasia kwa vyama vyote nchini.

Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika Ofisi ndogo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dar es saalam.

Dk.Mabodi  ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ameeleza kwamba misingi hiyo ndio chimbuko la kuwaunganisha  Watanzania bila kujali asili ya uzawa itikadi za kisiasa na kidini.

“Nitaheshimu itikadi za vyama vyote vya kisiasa nchini lakini nasisitiza tulinde demokrasia maana kama  demokrasia ikipote gharama za kuirejesha ni kubwa kuliko tunavyofikria “,.alisema Mabodi na kusisitiza kuwa kila chama kina wajibu wa kulinda haki na utu wa wananchi kupitia sera huru zinazohimiza Amani na Utulivu wa kudumu.

Pia amehimiza utaratibu wa kujenga hoja imara za kuhamasisha maendeleo na kulinda rasilimali za nchi.

Dk.Mabodi amesema akiwa ni kiongozi ndani ya Baraza hilo atalinda Katiba zote mbili ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 pamoja na kutoa kipaumbele kwa wananchi kupata habari, maoni na ushiriki katika siasa kwa mujibu wa Katiba na miongozo ya kisiasa.

Kupitia hotuba yake Dk.Mabodi aliwahakikishia Wajumbe wa Baraza hilo na wananchi kwa ujumla kuwa hatoruhusu baadhi ya wanasiasa watakaohubiri sera na ajenda za kudhihaki mihimili ya Dola iliyopo Kikatiba, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuzalisha mbegu za chuki na migogoro isiyokuwa ya lazima nchini.

Aidha alisema kupitia Baraza hilo ni lazima kila Chama cha siasa nchini kijielekeze katika kufanya siasa za kuwaunganisha wananchi katika masuala mbali mbali ya maendeleo .

“ Siasa za jino kwa jino ncha ya upanga kwa ncha ya upanga zimepitwa na wakati hivyo ni muhimu sana sisi viongozi kupitia vyama vyetu tujitathimini na kuwa mfano bora kwa wananchi”,alisema
  Makamu Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo amewashukru wajumbe wa baraza hilo kwa kumuamini na kumchagua ili aweze kutoa mchango wake wa kiuongozi na kiutendaji kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo, John Shibuda alisema kila chama kina wajibu wa kuthamini juhudi za serikali katika utekelezaji masuala mbali mbali yanayowanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.

Katika Mkutano huo walifanya uteuzi wa Kamati nne za kudumu za Baraza hilo ambazo ni Kamati ya fedha, Kamati ya Bunge na Siasa, Kamati ya Maadili na uhusiano pamoja na Kamati ya Sheria na Utawala bora zenye dhamana ya kusimamia  mwenendo wa utendaji wa vyama pamoja na Kamati ya uongozi ya baraza la vyama vya siasa.


Sambamba hayo pia Baraza hilo lilipokea maoni ya vyama vya siasa na mapendekezo ya wadau mbali mbali juu ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 pamoja na mapendekezo yake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni