Jumamosi, 20 Januari 2018

BALOZI SEIF ALI IDD: AMEUNGANA NA MAMIA YA WANANCHI KATIKA KHITMA NA DUA YA KUWAOMBEA ASKARI 10 WALIOUAWA DRC KONGO


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.



MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seid Ali Idd(wa pili kushoto) akizungumza na vyombo vya Habari juu ya Khitma na Dua ya kuwaombea Askari wa JWTZ waliouawa DRC Kongo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk,Mabodi(wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Ayoub wakiwa pamoja na Balozi.

MAMIA ya Wananchi, waumini wa Dini ya Kiislamu, Askari wa Majeshi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini pamoja na Ndugu na wana Familia leo wameungana katika Kisomo cha Hitma, Dua ya pamoja na Arubaini kwa ajili ya kuwarehemu Wanajeshi 10 wa Tanzania waliouawa wakati  wakilinda Amani Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepoteza Vijana wake hao mashujaa na walinzi wa Taifa waliouawa wakati wakitekeleza jukumu lao walilokabidhiwa na Umoja wa Mataifa la kusimamia ulinzi wa Amani Nchi ya DRC baada ya kuvamiwa ghafla na Waasi wa Nchi hiyo.

Kisomo cha Hitma na Dua hiyo ya pamoja kimefanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Noor Muhammad uliopo Mtaa wa Kwamchina Mombasa na kushirikisha pia Viongozi wa Serikali zote Mbili Wanasiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Tukio hilo la kusikitisha la kuuawa kwa Askari wa JWTZ lililogusa nyoyo za Watanzania wote pamoja na Walimwengu wapenda Amani limeacha msiba, simanzi, huzuni pamoja na majonzi makubwa hasa kwa Wana familia wa Vijana hao.

Akitoa nasaha mara baada ya Kisomo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Saeif Ali Iddi alisema upo umuhimu mkubwa kwa Jamii kuendelea kuwa na moyo wa subra wakati wanapopatwa na mitihani ili wazidi kuishi kwa Imani, Ushirikiano na upendo zaidi.

Balozi Seif alisema Muumba wa Dunia na vilivyomo ndani yake  ambae  ni Mwenyezi Muungu tayari ameshawabashiria mema na ya kheir wale wote waja wake walioamini na kupatwa na misiba na wakaamua kurejea kwake.

Amesema  Mkusanyiko wa Waumini na Wananchi katika kisomo hicho ulioweka pamoja waumini waliotoka Miji tofauti na Itikadi mbali mbali za Kisiasa pamoja na  madhehebu ya Dini ni dalili tosha ya kuonyesha mshikamano wa Jamii aliouamrisha Mwenyezi Muungu.

Balozi Seif ameeleza kwamba mahudhurio hayo ni kielelezo cha jinsi Taifa na Wananchi wake walivyoguswa na tukio hilo la msiba wa kuondokewa na wapenzi wao ambalo imani inaonyesha wazi kwamba halitosahaulika milele katika mioyo yao.

Makamu wa Pili wa Raiswa Zanzibar aliishukuru Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar kwa jinsi inavyobuni mambo kadhaa yenye maslahi kwa Taifa likiwemo hilo la mkusanyiko huo wa ubunifu wa kuandaa dua hiyo ambalo ni jambo na kupongezwa.

Balozi Seif ameeleza  matarajio yake kwamba Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar itaendelea na jitihada zake za kuwaweka  pamoja Waumini wa Dini mbali mbali na kuahidi kwamba Serikali Kuu itahakikisha kwamba inaunga mkono na kuisaidia Kamati hiyo katika kutekeleza jukumu lake.

Amewasihi  Viongozi na Watendaji wa Kamati hiyo waendelee kuongeza jitihada katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya mapenzi ya Jinsia Moja, Ubakaji, Udhalilishaji wa Wananwake na Watoto pamoja na mambo mbali mbali yasiyo na maslahi kwa Taifa hili.

Akitoa salamu Mwakilishi wa Familia za Wafiwa wa Wanajeshi hao wa JWTZ Bw.Haji Hassan kwa niaba ya Familia hizo aliwashukuru Watanzania wote walioshirikiana na wafiwa hao katika msiba huo mkubwa.

Bw.Haji Hassan alisema msiba wa Wanajeshi hao 10 uliotokea Mnamo Tarehe 7 Disemba Mwaka 2017 Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ulikuwa wa Taifa zima jambo ambalo lilileta faraja kwa wana familia hao.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuwaaidhi Waumini walioshiriki Kisomo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Sheikh Salim Mohammed Al – Kadir amesema Kamati hiyo imeguswa na Msiba huo uliopelekea Uongozi wa Kamati hiyo kuandaa dua hiyo ili kuonyesha mapenzi kwa Wapiganaji hao

Sheikh Salim kwa niaba ya Uongozi wa Kamati yake  wameishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano uloipa Kamati hiyo kuweza kutekeleza majukumu yake iliyopangiwa na Umma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni