Jumatatu, 18 Septemba 2017

Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar. 18/09/2017

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, leo amekiongoza kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM  Taifa Zanzibar.

Kikao hicho cha kawaida kimefanyika kwa mafanikio makubwa katika ukumbi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar Ndg Waride Bakari Jabu, pamoja na mambo mengine  kilipokea  na kujadili majina ya wagombea 50 waliojitokeza  kuomba nafasi za Uenyeviti  CCM  Wilaya 12 za Unguja na Pemba na kutoa mapendekezo yake ili  kuyapeleka  katika vikao husika.

Aidha  kikao hicho kilimpongeza  Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar,  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kufanya ziara ya Chama na Serikali kwa wakati mmoja kufuatilia Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 Unguja na Pemba kwa mafanikio makubwa  .

Kwa upande wake Rais za Zanzibar aliwashukuru viongozi, watendaji na  wananchi mbalimbali walioshiriki katika ziara  yake na kusisitiza juu ya umuhimu wa viongozi wa Chama na Serikali kuteremka chini  kwa wananchi  na kushirikiana nao katika harakati za  maendeleo kubaini changamoto zilizopo na kazipatia ufumbuzi .

Dk Sheni alimalizia kwa kusema viongozi wa Chama na Serikali wana wajibu mkubwa wa kutimiza wajibu wao  kikamilifu katika kukiwezesha Chama na Serikali kuendelea kukubalika zaidi kwa  wananchi na kushinda kwa kiwango cha juu zaidi  katika uchaguzi mkuu ujao.

Picha mbali mbali za kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.18/09/2017

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Juma Abdalla Juma (Mabodi) wakiimba wimbo wa Chama mara walipoingia katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja katika  kikao cha siku moja cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kilichofanyika leo,

Baadhi ya wajumbe kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar wakiimba wimbo wa Chama kumkaribisha  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani) katika kikao cha Siku moja  kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja.

 Baadhi ya Wajumbe wa kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar wakifuatilia kwa makini taarifa zilizotolewa katika kikao hicho kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja,chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani)

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Juma Abdalla Juma (Mabodi) alipokuwa akimkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) kuzungumza na Wajumbe wa kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(kushoto) alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa  Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar katika kikao cha siku moja kilichofanyika leo katika Ukumbi wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Unguja

 Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar wakiwa katika kikao cha siku moja cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kilichofanyika leo katika Ukumbi wa CCM Kisiwandui Mjini Unguja,chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(hayupo pichani)

Alhamisi, 14 Septemba 2017

" Hatutowavumilia wanaotumiwa na Upinzani " Dkt. Mabodi


Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Abdulla Juma Mabodi amesema chama hicho hakitowavumilia baadhi ya wanachama wanaotumiwa na vyama vya upinzani kuvuruga mshikamano uliopo ndani ya taasisi hiyo.

Hayo ameyasema wakati akihitimisha ziara zake za kuimarisha chama na kuwapa mikakati ya kiutendaji viongozi wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa chama hicho kuanzia ngazi za matawi hadi majimbo Unguja, uko katika Tawi la Ijitimai jimbo la Mwanakwerekwe.

Alisema kupitia uchaguzi wa chama unaofanyika kwa ngazi mbali mbali ni lazima wanachama wasaliti wawekwe kando kwa kutopewa nafasi za uongozi na kiutendaji ili kunusuru uhai wa chama hicho kisiasa.

Aliwasihi  viongozi waliochaguliwa kuzitendea haki nafasi zao kwa kushuka ngazi za chini kutafuta wanachama wapya hasa wa vyama vya upinzani wajiunge na CCM ili mwaka 2020 upatikane  ushindi wa kihistoria.

Aidha aliwataka viongozi hao  wapya kutumia rasilimali watu  za  wanasiasa wakongwe na wazee wa chama hicho kujifunza itikadi na historia ya chama ili watekeleze kazi zao kwa ufanisi.

“ Ustawi na umadhubuti wa CCM utaendelezwa na nyinyi ambao mmepewa dhamana ya uongozi kwa njia ya kidemokrasia kupitia chama chetu, pamoja na mambo mengine ni kumbukeni kuwa mtaji wetu kisiasa ni wapiga kura hivyo hakikisheni mtaji huu unaendelea kuimarika ili 2020 tushinde na kubaki madarakani.”, alieleza Dk.Mabodi.

Dk. Mabodi alisema chama hicho kina imani kubwa na viongozi wake wa jumuiya na chama waliochaguliwa  kuwa watakivusha na kuendeleza mambo mema yaliyoachwa na watangulizi wao.

Alisema CCM inaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020  ili kero mbali mbali zinazowakabili wananchi ziweze kutafutiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kupitia ziara hiyo aliwaagiza makatibu wa Matawi wa chama hicho pamoja na kamati zingine kuhakikisha wanashuka ngazi za chini za zoni kutafuta wanachama wapya pamoja na kufanya shughuli za kijamii za kuwasaidia wazee katika maeneo mbali mbali nchini.

Sambamba na hayo alitoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi na wanachama wanaouza kadi za uanachama kwa wapinzani na kuwataka waache tabia hiyo na atakayebainika atachukuliwa hatua za kimaadili kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.
 Naye Katibu wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe , Ramadhan Fatawi alisema  Madiwani kwa kushirikiana na Mwakilishi wa jimbo hilo wamesimamia na kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo kusimamia ujenzi wa barabara ya lami inayotoka katika mtaa wa Kwamabata kwenda magogoni iliyogharamiwa na Wizara ya nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalum.

Mradi mingine ni uendelezaji wa  ujenzi wa chuo cha Amali cha jimbo hilo, kulipia ada za masomo  wanafunzi wa vyuo vikuu na sekondari, kujenga vyoo katika skuli ya Urafiki ya Mwanakwerekwe.

Alizitaja changomoto zinazowakabili katika jimbo hilo kuwa pamoja na mafuriko yanayotokea kila mwaka, upungufu wa ajira kwa vijana pamoja idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika darasa moja maskulini.

Pamoja na hayo Katibu huyo aliahidi kuwa Chama cha Mapinduzi ndani ya jimbo hilo kimejipanga kuhakikisha Uchaguzi ujao wanarudisha nafasi ya kiti cha Ubunge kilichoshikiliwa na chama cha upinzani.




















Jumanne, 12 Septemba 2017

" VIJANA CHANGAMKIENI FURSA YA ELIMU " DKT. MABODI

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Abdulla Juma Mabodi amewataka vijana wa chama hicho kuchangamkia fursa za kielimu zinazotolewana serikali ili kupata wasomi watakaoendeleza misingi ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na vijana wa chama hicho katika kongamano la kuwajengea uwezo  vijana lililoandaliwa na Shirikisho la Vyuo na Vyuo vya Elimu ya juu CCM Zanzibar, lililofanyika katika hoteli ya Bravo Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kimeweka mikakati endelevu ya kuhakikisha serikali inatoa kipaumbele kwa sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha vijana wanasoma na kupatikana kwa viongozi na wataalamu waliobobea katika fani mbali mbali.

Dk.Mabodi alieleza kwamba mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 waasisi wa CCM walitoa fursa ya elimu kwa kuanzisha mfumo wa elimu bure kwa nia ya kuhakikisha watoto wa wanyonge wanapata elimu ili baadae waweze kujitawala.

“Vijana wa CCM tumieni fursa ya elimu vizuri kwani serikali imeimarisha mfumo wa elimu kuanzia ngazi za maandalizi mpaka vyuo vikuu hivyo hakuna sababu ya kushindwa kusoma.

Maendeleo ndani ya chama chetu yataimarika endapo kutakuwa na vijana makada waliosoma fani mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja zenye nguvu zitakazolinda heshima ya chama chetu”, alisema Dk.Mabodi.

Akifungua kongamano hilo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Dk. Mohamed Seif  Khatib aliwataka vijana waliopata fursa ya elimu ya juu kuwa wabunifu wa masuala mbali mbali yatakayoweza kuisaidia nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Alisema matarajio ya Chama cha Mapinduzi na serikali ni kuona vyuo vikuu vinazalisha vijana wenye weledi na uwezo wa hali ya juu katika kuchanganua na kushauri mambo yenye tija na manufaa kwa wananchi wote.

“ Rika la vijana ndio nguvu kazi ya taifa lolote duniani na Chama cha Mapinduzi tunajivunia kuwa tunao vijana waliobobea katika fani mbali mbali hivyo tunaamini kupitia wingi wenu mtaendelea kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo yatakayoweza kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”, alieleza Dk. Seif.

Dk. Seif aliwataka vijana kuendelea kuwa wazalendo ili Chama Cha Mapinduzi kiweze kushinda na kusimamisha serikali kwa kila uchaguzi mkuu wa Dola.

Naye Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya Mjini, Baraka Shamte ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho, akitoa mada ya Zanzibar  ilipotoka, ilipo hivi sasa na inapoelekea alisema historia ya Zanzibar ndio somo pekee litakalowajengea uwelewa mzuri vijana wa sasa.

Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar  mwaka 1964 nchi ilikuwa katika dhiki na mateso makubwa yaliyotekelezwa na watawala wa wakati huo dhidi ya wananchi.

Alisema maendeleo yaliyopo nchini yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa CCM wanaosimamia kwa nguvu zote sera za maendeleo na kukuza uchumi kama walivyoaidi kupitia Ilani ya uchaguzi ya chama ya mwaka 2015/2020.