Jumatano, 19 Aprili 2017

MH.SAMIA : AWAPA SOMO VIONGOZI WA CCM WILAYA YA KUSINI UNGUJA.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Mh.Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuchukua hatua za kuwasilisha changamoto zinazowabili wananchi kwa viongozi wa serikali wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu na Wakurugenzi ili watafute ufumbuzi wa kudumu.

Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za matawi hadi Wilaya za Wilaya ya Kusini Unguja huko katika Ukumbi wa Skuli ya Makunduchi alisema baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wamekuwa na utamaduni wa kulalamika pindi wanapokutana na viongozi wa ngazi za juu za chama, hali ya kuwa utatuzi wa kero hizo upo katika uwezo wa  utekelezaji wa viongozi wa serikali wanaotokana na chama hicho.

Maelekezo hayo yamekuja mara baada ya Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini, Hamdan Haji Machano  kusoma taarifa ya utekelezaji na hali ya kisiasa ndani ya Wilaya hiyo iliyokuwa na kero za Kesi za udhalilishaji wa kijinsia kuwa na urasimu wa kutotolewa hukumu haraka, pamoja na upungufu wa maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo.

 Mh. Samia ambaye pia ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza kwamba tabia hiyo inatakiwa kukemewa kwani haijengi uimara wa chama, kwani inatoa mwanya wa viongozi wa Chama kuwaogopa watendaji wa Serikali wakati wao ndio waliowapa ridhaa ya kuongoza dola.

Alisema haiwezekani wananchi wakabiliwe na changamoto za kijamii, kisiasa na kiuchumi wakati wapo viongozi wa serikali wenye dhamana ya kutatua kero hizo.

Akifafanua juu ya Changamoto ya vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa Kijinsia, Mh. Samia aliwambia viongozi hao kuwa suala hilo walipeleke kwa Waziri anayehusika na masuala ya Katiba na Sheria ili aweze kuwasimamia watendaji wake watekeleze wajibu wao.

“Nyingi ndio mabosi wa hao viongozi wote waliopo serikali haiwezekani eti serikali mmeiweka madarakani alafu mnakuja kukaa wanyonge kwa kuwa kuna matatizo yanawakabili wananchi yamekosa utekelezaji kutokana na Urasimu wa viongozi wachache,  na mkiwaita wakakataa kuja nendeni kwa Rais wa Zanzibar Dkt, Shein ambaye ni Makamo Mwenyekiti wa Chama chetu.

Lazima tuwe imara na misimamo thabiti ya kiutendaji ndani na nje ya chama chetu kwa kuondokana na uendeshaji wa taasisi yetu kwa mazoea kwani sote tupo kwa ajili ya wananchi ”, Alisema Mh.Samia.

Alifafanua Mh.Samia na kuongeza kwamba  CCM mpya na Tanzania mpya ni muhimu dhana hiyo kutekelezwa kwa vitendo ili kuendana na marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 yaliyofanyika hivi karibuni, kwa lengo la kuongeza ufanisi ndani ya taasisi hiyo.

Hata hivyo aliwataka wanachama wa CCM hasa vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi katika Uchaguzi wa Chama unaoendelea kwa sasa katika ngazi za mashina na matawi huku akiwasihi Wazee kuwa karibu na vijana wao sambamba na kuwafunza uzalendo na itikadi za chama hicho.

Alisema Chama hicho kwa sasa kinaenda na kasi ya kiutendaji na kiungozi isiyokuwa ya kawaida ambayo ameifananisha na kasi ya mtandao wa 4G, hivyo panahitajika nguvu za vijana imara walioiva kiuzalendo ambao wataweza kupokea kijiti cha uongozi kutoka kwa wazee waliotumikia nchi na chama kwa muda mrefu.

“ Vijana mtakapokaa kando basi jueni hii nchi mtaiuza kwa gharama nafuu na kuirudisha itakuwa ni vigumu, lazima mtulie na kuacha tabia za kukubali kushawishiwa na kuweni na msimamo ili mjenge heshima kwa vizazi vyenu vya sasa na baadae , kama ilivyo kwa wazee wetu waliokomboa Tanzania bara na Zanzibar na kwa sasa tunafaidi matunda yao.”, Alisisitiza mwanasiasa huyo.

Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu wa wachama, watumishi na viongozi wa jumuiya na chama kusoma kwa kina Katiba ya Chama na kanuni zake  ili waweze kujua majukumu yao ili wajadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa njia ya vikao  rasmi vya kikanuni. 

Hata hivyo Kabla ya kuwahutubia  Wanachama hao alianza kufanya kazi za uimarishaji wa Chama kwa kuweka jiwe la msingi katika Tawi la kisasa la Mungoni Jimbo la Paje, sambamba na kutembelea miradi  ya ujenzi wa skuli mbili zenye ukumbi wa mikutano iliyogharimu kiasi cha zaidi ya milioni 217, katika vijiji vya Kajengwa na Kizimkazi ambazo ni moja ya ahadi alizotoa wakati akiwa na nafasi ya Ubunge katika jimbo la Makunduchi. 

Mapema akizunguimza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadalla “ Mabodi”  aliwambia viongozi hao kwamba  mtaji wa chama kisiasa ni wanachama hai wanaokubalika kisheria, hivyo kila mtu anatakiwa kutendea haki nafasi aliyokuwa nayo ili chama hicho kishinde katika uchaguzi wa 2020.

Dkt.Mabodi aliwasihi wanachama hao kuwachagua viongozi wenye ushawishi na wanaokubalika katika jamii watakaoweza  kuongeza wanachama wapya kutokana hata katika vyama vya upinzani, na makundi mengine yaliyopo nchini.

Pia aliahidi kwamba atatumia uwezo na ujasiri wake katika kusimamia masuala ya kiutendaji ndani ya chama ili kwenda sambamba na matarajio, dira na dhamira ya Chama hicho kwa kuwatumikia wananchi kwa weledi. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika harakati za ziara hiyo kabla ya kuanza kwa kikao hicho mmoja wa Raia Swaziland wanayeishi hapa nchini Bw. Nicolas Sarraj amesifu siasa zinazofanywa na CCM, zilizozaa matunda ya kuwepo kwa sekta ya utalii ambayo imetoa uhuru wa raia wan chi za kigeni kuja nchini kutalii kwa amani na Utulivu.

Sambamba na hayo alisema Zanzibar imekuwa kitovu cha maendeleo katika ukuaji wa sekta mbali mbali za miundombinu zikiwemo barabara, viwanja vya ndege pamoja na uimarishaji wa huduma za kijamii na kiuchumi.

Jumatatu, 17 Aprili 2017

MH. SAMIA AKIWEKA JIWE LA MSINGI KATIKA TAWI CCM MUUNGONI ZANZIBAR

MH.SAMIA: ASISITIZA WANA CCM KUENZI KWA VITENDO JUHUDI ZA WAASISI.


MJUMBE WA KAMATI KUU YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), MH.SAMIA SULUHU HASSAN AMESEMA KUWA CCM NDIO CHAMA CHENYE MIZIZI YA  ASILI YA KITANZANIA KWANI KIMETOKANA NA VYAMA VYA UKOMBOZI AMBAVYO NI TANU NA ASP.

KAULI HIYO AMEITOA WAKATI AKIZUNGUMZA NA KAMATI ZA SIASA ZA NGAZI ZA MATAWI HADI SIASA ZA MKOA WA KUSINI UNGUJA KICHAMA HUKO DUNGA, AMEELEZA KWAMBA HESHIMA HIYO ILIYOJENGWA NA WAASISI WA VYAMA HIVYO INATAKIWA KUENDELEZWA NA WANACHAMA WA SASA KWA KUHAKIKISHA CHAMA KINAENDELEA KUONGOZA DOLA KWA NJIA ZA KIDEMOKRASIA.

AIDHA  MH.SAMIA AMBAYE PIA NI MAKAMO WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA  AMESISITIZA UMOJA NA MSHIKAMANO BAINA YA WANACHAMA NA VIONGOZI WA NGAZI MBALI MBALI NDANI YA CHAMA NA  JUMUIYA KWA UJUMLA, ILI KUENDELEZA DHANA YA SERIKALI KUJITEGEMEA YENYEWE BILA YA KUSUBIRI UFADHILI WA WAHISANI KUTOKA NJE.

MAPEMA NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR, DKT.ABDALLA JUMA SAADALLA MABODI AMEAHIDI KUSIMAMIA IPASAVYO MCHAKATO WA UCHAGUZI NDANI YA CHAMA HICHO ILI KILA MWANACHAMA AWEZE KUPATA HAKI YAKE KWA MUJIBU WA KATIBA NA MIONGOZO YA CCM.


SAMBAMBA NA HAYO AMEELEZA KUWA KATIKA MCHAKATO HUO HATORUHUSU KUFANYIKA VITENDO VYA KUPANGWA SAFU ZA MAKUNDI YA UONGOZI NA RUSHWA.