Jumatatu, 3 Aprili 2017

CCM ZANZIBAR KUTUMIA SIASA ZA KISAYANSI



NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dkt. Abdallah Juma Abdallah “Mabodi”  amesema chama hicho kimejipanga kufanya siasa zenye ushindani wa kisera, kitaaluma, kiubunifu ili kwenda na wakati wa siasa za kisayansi zitakazojenga mazingira ya ushindi wa Dola kwa CCM mwaka 2020.

Msimamo huo ameutoa katika Ziara yake ya mwanzo toka akabidhiwe madaraka iliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, ameeleza kwamba  chama kina nyenzo za kila aina zitakazotumika  katika uwanja wa kisiasa kwa lengo la kuifuta  CUF na vyama vingine vyenye vinavyoshirikiana na chama hicho katika historia ya siasa za Zanzibar.

Mwanasiasa huyo  Mkongwe myenye Taaluma ya Udaktari ameweka wazi kuwa atatumia falsafa ya Sayansi ya Siasa kufuta kabisa upinzani Visiwani Zanzibar, kwani vyama hivyo hasa CUF wameshindwa hata kushauri utekelezaji wa Ilani ya CCM badala yake wanaeneza chuki na misimamo ya utengano kwa wananchi.

Ameeleza kwamba  Vyama vyenye asili ya migogoro na uchu wa madaraka, haviwezi kuongoza nchi hivyo jamii iviepuke na wafuasi wa vyama hivyo wahamie CCM milango ipo wazi ili wanufaike na siasa za maendeleo na demokrasia imara.

Dkt. Juma amesema ili kufikia malengo hayo kila mwanachama na mfuasi wa CCM pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuimarisha dhana ya umoja na mshikamano huku wakitafakari njia bora za kuzibakisha madarakani serikali za CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Pia akizungumza na wanachama wa  Tawi la CCM Mtende Mkoani humo amewataka  wafuasi wa chama hicho kufungua ukurasa mpya wa kuanzisha miradi ya maendeleo katika matawi yao ili waweze kujitegemea wenyewe badala ya kuwa tegemezi kwa wabunge, wawakilishi na madiwani.

Aliupongeza uongozi wa Tawi hilo pamoja na Shehia ya Mtende kwa hatua za kimaendeleo walizofikia katika sekta za miundombinu, afya na elimu na kuzitaka mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza changamoto ya upungufu wa maji safi na salama kwani visima vya eneo hilo vimengia maji ya chumvi.

“ Mtaji wa CCM ni wananchi hasa wale wanaokiamini chama na kukipigia kura kila uchaguzi  hivyo nyinyi ndio  waajiri wetu mliotukabidhi majukumu ya kiutendaji na kiuongozi ni lazima tukutumikieni kwa uadilifu na weledi unaoendana na hadhi ya chama chetu.

Pia  nakukumbusheni kuwa maendeleo yanayopatikana hivi sasa yanatokana na radhi za  Wazee wetu ambao ni waasisi wa ASP na TANU ambayo ni CCM ya sasa inayotutengenezea maisha bora yanayoambatana na amani na utulivu kwa kila mwananchi.”,  Alisema Dkt. Mabodi na kuwasihi  Wana CCM kuendelea kuwa karibu na kuwashawishi  wafuasi wa Vyama vya Upinzani kujiunga na Chama hicho ambacho ni kinara wa Demokrasia, amani, utawala bora na siasa za maendeleo.

Aidha  ametoa agizo kwa  Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Chama hicho kuwasilisha mrejesho wa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa ngazi husika kila baada ya miezi mitatu ili kufanyike tathimini za kitaalamu zitakazopima utekelezaji wa Ilani hiyo kama unaendana na mahitaji ya wananchi waliyoahidiwa katika Kampeni zilizopita.

Hata hivyo aliagiza kutekelezwa haraka agizo la kila Tawi la CCM katika Mkoa wa Kusini  kuwekwa kwa sanduku la maoni ambalo kila mwanachama mwenye kero atatumia njia hiyo kuwasilisha maoni yake moja kwa moja  ili Afisi Kuu CCM Zanzibar kwa kutumia utaratibu maalum itayachambua kwa kina kwa lengo la kubaini  mambo yanayokwamisha utekelezaji wa ilani kwa baadhi ya maeneo.

Akizungumzia  zoezi la Uchaguzi  wa Chama unaoendelea hivi sasa kwa ngazi ya matawi alisema Chama bila kuwa na Wazee wenye hekima na busara hakiwezi kwenda kwani vijana pekee yao hawana uwezo wa kuongoza bila ushauri wa Wazee  hivyo  taasisi hiyo inahitaji mchanganyiko wa makundi yote kugombea nafasi za uongozi hasa ngazi za matawi.

Wakati huo alizindua na kuweka jiwe la Msingi katika Maskani mbali mbali  zikiwemo Maskani ya Haroun, Haji Jecha , Tumegutuka na Maskani ya Kisonge ambapo jumla ya wanachama wapya 90 kutokana CUF wamejiunga na CCM na kukabidhiwa kadi rasmi za chama.

Akitoa maneno ya Shukrani  Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Unguja, Haroun Ali Suleiman aliwambia wanachama wa chama hicho kuendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM ili iweze kuwaletea maendeleo endelevu huku ikilinda Amani na utulivu wa nchi.

Ziara hiyo ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhai wa Chama na kuongeza hamasa kwa wanachama wa ngazi za  Mashina na Matawi ya CCM kuamini kuwa wao ndio nguzo ya mafanikio ya Chama ambapo Viongozi  mbali mbali wa chama, serikali na jumuiya wameshiriki katika ziara hiyo.

Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kusini, Ramadhani Abdalla Ali, Katibu wa Mkoa Sauda Mpambalyoto, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kusini Abdulaziz Haji, Mkuu wa Wilaya Kusini Idrissa Kitwana Mustafa na Katibu wa UVCCM Wilaya ya kusini Haji Mwalimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni