Jumatatu, 27 Julai 2015

VUAI: AFARAJIKA NA IDADI KUBWA WANACCM KUWANIA UONGOZI KATIKA VYOMBO VYA DOLA.NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg. Vuai Ali Vuai, amewataka Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi kutozifunga Ofisi za CCM, ili kutoa fursa kwa wanachama wa chama hicho kufanikisha mahitaji yao ya msingi hasa  kipindi hiki cha mchakato wa kuwapata wana CCM watakaokiwakilisha Chama katika Uchaguzi ujao wa Dola.

Mhe. Vuai ametoa kauli hiyo wakati akifungua Mkutano wa UWT wa Mkoa wa Kichama wa Mjini Unguja, kwa ajili ya kuwachagua wana CCM watakaowania nafasi za Viti Maalum vya Ubunge na Uwakilishi kupitia Jumuiya hiyo.

Amesema si jambo la busara kwa Watendaji wa CCM kuzifunga Ofisi za Chama hasa wakati huu wa harakati za kutafuta uongozi ndani ya vyombo vya dola na badala yake waziache wazi ili wana CCM wenye mahitaji muhimu, ili waweze kuhudumiwa kwa ufanisi na kwa uadilifu mkubwa.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar ametumia mkutano huo kusisitiza haja kwa  wana CCM kuchagua viongozi bora, mahiri, weledi na wenye uwezo wa kujenga hoja madhubuti zitakazosaidia Chama na Serikali kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Akizungumzia kuhusu wana CCM waliochukua fomu za kugombea nafasi za dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mhe. Vuai ameelezea kufurahishwa kwake na idadi kubwa ya Wanachama wa Chama hicho waliojitokeza kuomba waruhusiwe kugombea nafasi za Ubunge, Uwakilishi,  Udiwani pamoja na Viti Maalum Wanawake.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar, amesema jumla ya wanachama 1,322  kutoka  Mikoa sita ya Kichama ya Unguja na Pemba, wakiwemo 623 (wanaume) na 699 (wanawake) wamejitokeza kuomba kuteuliwa na Chama chao (CCM), ili waweze  kugombea nafasi hizo.

Akifafanua zaidi,  Mhe. Vuai amesema kati ya hao,  wana CCM 378 wameomba Ubunge, 358 Ujumbe wa Baraza la Uwakilishi, 289 Udiwani na 297 wameomba nafasi hizo kupitia Viti Maalum.

Amesema idadi  ya wana CCM walioomba kugombea kupitia Majimboni na idadi ya walizoomba kwenye mabano kwa wanaume ni Ubunge (222), Uwakilishi (221)  na Udiwani (180), ambapo kwa wanawake Ubunge (156), Uwakilishi  (137) na Udiwani (109) pamoja na wanachama 297 wameomba kupitia Viti Maalum (wanawake) Mikoani mote.

Mhe. Vuai  amesema miongoni mwa wana CCM 297 kupitia Viti Maalum nao wameomba kuwania nafasi hizo za uongozi ndani ya vyombo vya dola, ambapo 129 (Ubunge), 101 (Uwakilishi) na  67 (Udiwani).

Amesema kuwa idadi hiyo kubwa imekuja kufuatia kuwepo kwa demokrasia pana ndani ya Chama Tawala (CCM) nchini inayotoa fursa kwa kila mwanachama mwenye uwezo wa kugombea nafasi yoyote katika vyombo vya dola anaweza kufanya hivyo.

Mhe. Vuai amewapongeza kwa dhati kabisa Makada hao waliojitokeza kutaka waruhusiwe na Chama chao (CCM), ili waweze kuwania nafasi hizo na kuwatakia kila la heri na mafanikio makubwa katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, 2015, nchini kote.


Ijumaa, 17 Julai 2015

MAGUFULI APOKELERWA KWA SHANGWE ZANZIBAR


Mgombe wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli apokelewa na maelfu ya wanachama,wapendana amani, wakereketwa hapa kisiwani Unguja.

Mnamo tarehe 16/07/2015. Mgombe wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kupitia tiketi ya Chama Cha Mpainduzi {CCM} alipokelewa kwa shangwe kubwa na wanachama wa CCM.

Akiwasili kisiwani Zanzibar alifuatana na Mgombea mwenza wa CCM Mhe. Samia SuluhU Hassan walifikia Afisi Kuu CCM Zanzibar.


Add caption


Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein akimsalimia kwa bashasha mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, mgombea huyo alipowasili leo mjini Zanzibar kwa ajili ya utambulisho kwa wana CCM.
Jumatano, 15 Julai 2015

Mimi na Rais Kikwete tumebeba dhamana ya kulinda amani

Rais wa Zanzibar dk.Ali Mohamed Shein amewaonya wanasiasa na kusema hakuna mtu aliyepo juu ya sheria ambapo yeye na rais Jakaya Kikwete wamebeba dhima kubwa ya kuhakikisha nchi inakuwa na utulivu mkubwa wakati wowote.

Dk.Shein alisema hayo muda mfupi baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama cha mapinduzi kuchaguliwa kuongoza Zanzibar kwa kipindi chengine cha miaka mitano hapo Afisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini hapa.

Dk.Shein ambaye ni makamo mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Zanzibar alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wanachama wa chama hicho ambao walichukuwa jukumu la kumdhamini kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.

Alisema wapo wanasiasa wengine wanatumia nafasi ya kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa ajili ya kuvuruga amani na utulivu jambo ambalo haliwezi kukubalika hata kidogo.

‘Mimi na rais Jakaya Kikwete ndiyo tuliyokabidhiwa jukumu la kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa salama lenye amani na utulivu kwa muda wote’alisema dk.Shein huku akiahidi uchaguzi mkuu utakuwa huru na haki.