Jumatano, 30 Desemba 2015

CCM YATOA UFAFANUZI JUU YA TAARIFA YA JUSSA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI. 

ITAKUMBUKWA kuwa Desemba 27, mwaka 2015, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Zanzibar ilikutana, chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. 

Kama ilivyo ada, mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kupitia Msemaji wake Mkuu kilipata nafasi ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, kwa madhumuni ya kuwajuvya kwa muhtasari maamuzi yaliyofikiwa na kikao hicho. 

Aidha, Chama Cha Mapinduzi kimesikitishwa sana na taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha CUF Ismail Jussa kwa kukariri na kuripoti mazungumzo ya ndani ya kikao chetu, chenye dhamana ya kuendesha na kusimamia masuala yote ya siasa kwa upande wa Zanzibar. 

CCM kinamshangaa kiongozi huyo kwa kuacha kuyazungumzia mambo yanayohusu chama chake na badala yake kuanza kufuatilia mambo ya ndani ya CCM ni dhahiri kwamba kiongozi huyo anavyoonyesha jinsi gani alivyoishiwa na kufilisika kisiasa. Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwaomba Viongozi na Wanachama wote wa CCM na wapenda Amani na Utulivu wa nchini kuzipuuza na kuzidharau porojo (Drip) hizo za kisiasa za wapinzani zilizokosa heshima, hekima, busara, maadili na uvumilivu wa kisiasa na badala yake waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo zitakaowapatia mapato halali na kujikwamua na umasikini. 

Aidha, waelekeze nguvu zaidi katika kudumisha suala zima la amani na utulivu huku wakisubiri maelekezo kutoka Vyombo vya Kisheria hususan Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza siku ya uchaguzi wa marudio, na kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza kwa wingi siku hiyo tayari kwa kuwaipigia kura wagombea wote wa CCM. 

Kama hiyo haitoshi, Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kinalaani vikali taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa ambayo kwa hakika inaendeleza makosa ya kutoa matokea ya uchaguzi ya Chama chake (CUF) ilhali akijua kuwa Uchauguzi huo tayari ulishafutwa na Tume halali na iliyowekwa kikatiba na hivyo kuwafanya Wazanzibari wajiulize masuala yasiyopata majibu sahihi kwamba Jussa haoni kufanya hivyo sio tu ni kwenda kinyume na sheria za nchi bali pia ni kosa la jinai. 

Mwisho kabisa, Chama Cha Mapinduzi kamwe haitaingilia maamuzi ya chama chocote cha kisiasa kwani chama hichi (CCM) ni kikubwa, kilichojijengea heshima kubwa kwa wananchi wa Tanzania, Barani Afrika na Duniani na kubwa zaidi ni chama pekee kinaheshimu demokrasia.

Ahsanteni.
(Waride Bakari Jabu), 
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM, ZANZIBAR.

Jumatatu, 28 Desemba 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KIKAO CHA KAMATI MAALUM YA NEC ZANZIBAR ILIYOFANYIKA AFISI KUU YA CCM KISIWANDUI TAREHE 27 DESEMBA, 2015.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein leo, amekiongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi Bibi Waride Bakari Jabu imesema kikao hicho cha kawaidi cha siku moja kilifanyika Afisi Kuu ya Chama hicho, iliyopo Mtaa wa Kisiwandui Mjini Unguja.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
1. Kikao pamoja na mambo mengine, kimempongeza kwa dhati kabisa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuteuliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Awamu ya Tano) baada ya kupata ushindi wa kishindo (58.46%) na hivyo kuweza kuendeleza wimbi la ushindi kwa CCM ndani ya Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa nchini. Aidha, kikao kimempongeza Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan, kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

2. Kikao kimefurahishwa, kuridhishwa na kufarajika na idadi kubwa ya wana CCM kwa kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Oktoba 25, 2015 na hatimaye kumchagua kwa kura nyingi za ndio Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, pamoja na Wabunge.

3. Kikao kimewataka wana CCM kujiimarisha, kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi wa marudio, ili kukiletea ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kuanzia Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wakati utakapowadia.

4. Kikao pia kimeridhia majadiliano yanayoendelea kuhusu hali ya Kisiasa Zanzibar yanayoshirikisha Viongozi kadhaa wakiwemo Marais Wastaafu wa Zanzibar Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Mhe, Dkt. Salmin Amour Juma na Mhe, Amani Abeid Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi,

Kuhusu Shughuli za Kimaendeleo.
1. Kikao kimepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii wananchi wake. Aidha, imempongeza Mhe. Dkt. Shein kwa kusimamia suala zima la Amani na utulivu wa nchi kwa kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.

2. Sambamba na hilo, Serikali imetakiwa kuongeza juhudi na kubuni mikakati madhubuti itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa miradi (mipya) mbali mbali ya maendeleo Mijini na Vijijini Unguja na Pemba, ili kuinua mapato ya Taifa.

Kuhusu Uhai wa Chama (CCM).
Kikao kimetoa pongezi za pekee kwa Wajumbe wote wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Viongozi wa Chama na Jumuiya zake kwa kazi nzuri ya kuimarjisha Chama na kuwataka kuwa mstari wa mbele katika kukipigania, kukilinda na kukitetea kwa nguvu zote Chama hicho. Aidha, kimewataka kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano, juhudi na maarifa katika kukijenga na kukiimarisha Chama, kwa maslahi ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

 Mwisho, kikao hicho kilihudhuriwa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan. Mwisho. Waride Bakari Jabu, Katibu wa Kamati Maalum wa NEC, Idara ya itikadi na Uenezi – CCM, ZANZIBAR. 27/12/2015.

Jumamosi, 21 Novemba 2015

TAMKO LA CHAMA CHA MAPINDUZI ZANZIBAR KULAANI KITENDO CHA UKAWA KUWAZOMEA VIONGOZI WA SMZ WALIOHUDHURIA SHEREHE ZA UZINDUZI WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA

Mhe. Waride B. Jabu, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi -CCM. ZANZIBAR akitoa Tamko la Chama Cha Mapinduzi, hapo katika Afisi Kuu za CCM Kisiwandui Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar: Kinaipongeza kwa dhati hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John P. Magufuli aliyoitowa jana Bungeni (Nov. 20, 2015), katika Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Moja(11). Kwani ni Hotuba ilyosheheni kila aina ya hekima na Busara za Hali ya juu. Aidha ni dira tosha ya maendeleo kwa maslahi ya jamii ya watu wa Watanzania.
Vile Chama Cha Mapinduzi kinatambua kuwa wananchi wa Zanzibar hasa wale wanaopenda Amani na Utulivu kwa mara nyengine wamepatwa na machungu makubwa juu kutokana na kitendo cha jana cha kuvunjiwa heshima kiongozi wao. Hata hivyo kwa niaba ya CCM, nchukua fursa hii kuwaomba kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu. Kwani Dawa ya Wapinzani iko njiani. kwa mara nyengine tena tunaiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar itangaze siku ya uchaguzi ili tufanye uchaguzi utakaokuwa wa huru na haki. Ni dhahiri, baada ya uchaguzi huo, CCM Zanzibar na Wananchi wa Zanzibar watalazimika kufanya maamuzi mengine ingawa yatakuwa magumu.

Mhe. Waride B. Jabu, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi -CCM. ZANZIBAR akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habri mara tu baada ya kutoa  Tamko la Chama Cha Mapinduzi,
hapo katika Afisi Kuu za CCM Kisiwandui Zanzibar


Aidha, CCM inawaambia Viongozi na wafuasi wa CUF kuwa suala la kuapishwa Maalim Seif Sharrif kuwa ni ndoto za mchana kwani Tume imeshatangaza kufutwa kwa Uchaguzi huo, na kinachofanywa na CUFni kuwadanganya wananchi tu na sio jengine

Jumamosi, 17 Oktoba 2015

MAELFU YA WANACCM WAJITOKEZA KUMPOKEA MAGUFULI - UNGUJA

Maelfu ya Wananchi wa Pemba wajitokeza kumpokea Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya watu wa Tanzania Mhe. Dkt. John P. Magufuli hapo katika  kiwanja cha Gombani ya Kale mnamo 16/10/2015.

Mapokezi hayo yalikuwa ya kustaajabisha huko kisiwani Pemba kwani maelfu ya wanachama wa CCM walijitokeza ili kwenda kumpokea Mgombea wetu.

Vile vile Mhe. Magufuli alisindikizwa na mwenyeji wake ambae ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed SHEIN.