Jumamosi, 10 Februari 2018

Uchaguzi mwengine hadi 2020 - Dk. Mabodi

WANANCHI wa Kisiwani Pemba, wametakiwa kufahamu kuwa Serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na Dk Ali Mohamed Shein ni halali, imechaguliwa kwa Baraka zote na wananchi na wala hakuna uchaguzi mwengine kwa sasa hadi 2020.

Uchaguzi uliomalizika 2015 uliweza kuvishirikisha vyama mbali mbali vya siasa, hivyo kupapatikiwa mtu mmoja haiwezekani kwa kujitoa kwake wakati wengi wameshiriki katika uchaguzi huo.

Naibu katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Mhe:Dk Abdulla Juma Saadalla, aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM wa Tawi la Mwambe na Kendwa Jimbo la Kiwani Wilaya ya Mkoani, ikiwa ni ziara yake ya kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015/2020.

“Kwa mwaka huu na hii inayofuata sahauni, kura kwa Zanzibar haipigwi tena wala hakuna tena uchaguzi kwa sasa, CCM mbele kwa mbele na sio mguu mbele mguu nyuma kama wanavyosema wapinzani, uchaguzi mkuu kwa Zanzibar ni 2020 mungu akipenda”alifahamisha Naibu.

Aliwataka viongozi wa matawi kushuka chini kwa wananchama na wananchi, kuwaelezea maendeleo mbali mbali yaliyofanywa na Serikali iliyopo madarakani.

Mabodi alifahamisha umuhimu wa vyama vya siasa ni kushindana kwa sera na sio kushindana kwa vituko, kwani bado wazanzibari wanahitaji kuishi kwa amani na utulivu.

Hata hivyo aliwataka kamatibu na wenyekiti wa matawi, kuwapokea wanachama wapya watakaojiunga na CCM, kutoka vyama vya upinzani kwani tayari kuna idadi kubwa ya wapinzani wanatarajiwa kujiunga na CCM kwa upande wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema wakati umefika wa kurudisha madarasa ya Itakadi ya CCM, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambayo ni muhimu kwa CCM.

“Wajumbe wa Nec wajibu wenu kupita kwa wananchi na sio kukaa ofisi, sasa kazi ya kwenda vijijini imewadia kuhakikisha wanachama wapya wanapatikana”alisema.

Hata hivyo aliwataka wanaCCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la Mpiga kura wakati utakapofika, ili CCM iweze kurudi tena madarakani.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kusini Pemba Yussuf Ali Juma, aliwataka wanaCCM kujitokeza kuchukuwa vitambulisho, ili kushiriki katika haki yake ya msingi na sio kuwachia wanachama wa upinzani pekee.

Hata hivyo aliahidi kurudisha madarasa ya Itikadi ya CCM, ili vijana waweze kuelewa mambo muhimu yaliyomo ndani ya chama cha Mpainduzi.

Nao baadhi ya wanachama wa CCM katika Jimbo la Kiwani, walimshukuru Naibu katibu Mkuu wa CCM, kwa juhudi zake za kusimamia na kuendeleza chama cha mapinduzi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni