Jumapili, 16 Septemba 2018

MAANGAIKO YATWAA UBINGWA MABODI CUP.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi (kushoto) akimkabidhi Kombe la ushindi nahodha wa Timu ya Maangaiko ndugu Mkongea Mohamed Hamada (kulia) mara baada ya timu  hiyo kushinda wa penalti 4-2 dhidi ya timu ya Ubina katika Fainali ya Ligi ya Mabodi CUP iliyochezwa Kajengwa Makunduchi Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi (kushoto) akimkabidhi Kombe la ushindi nahodha wa Timu ya Ubina ndugu Haji Kheri Ussi  (kulia) ambaye Timu yake imeibuka msindi wa pili katika ligi ya Mabodi CUP.
WANANCHI wa vijiji mbali mbali vya Jimbo la Makunduchi walioudhuria katika mechi ya Fainali za kombe la Mabodi CUP wakishuhudia utoaji wa zawadi mbali mbali kwa timu zilizoshiriki mashindano hayo.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Maangaiko katika Fainali za ligi ya Mabodi CUP.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akisalimiana na waamuzi wa mchezo wa Fainali hiyo ya ligi ya Mabodi CUP.


 WASHIRIKI wa mbio za magunia wakionyesha uwezo wao katika kiwanja cha Uhuru katika fainali hizo za Mabodi CUP.


 TIMU za Ubina na Maangaiko wakitimua vumbi katika mchezo huo wa Fainali za ligi ya Mabodi CUP 2017-2018.

WASHIRIKI wa mchezo wa kuvuta kamba wakionyesha uwezo wao katika fainali hizo za Mabodi CUP 2017-2018.





NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla (Mabodi) amewataka vijana kuchangamkia fursa za ajira zilizopo katika sekta ya michezo nchini.

Rai hiyo ameitoa wakati akifunga  fainali ya Mechi za ligi ya Mabodi Cup iliyochezwa katika uwanja wa Uhuru uliopo Kajengwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk.Mabodi amesema CCM inaendelea kusimamia ipasavyo Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika kuimarisha sekta ya michezo kwa kujenga Viwanja  vya kisasa vya michezo katika maeneo mbali mbali nchini.

Akizungumzia historia fupi ya ligi hiyo kuwa imeasisiwa na Marehemu Juma Abdulla Saadalla Mabodi kwa lengo la kudumisha mshikamano kwa wananchi wote wa Vijiji vya Makunduchi.

Alisema ni muhimu kwa wananchi hao hasa vijana kuthamini na kuendeleza tunu za maendeleo zilizoasisiwa na Wazee wa vijiji vya Jimbo la Makunduchi kwa sababu jitihada zao haziwezi kulipwa ila zithaminiwezi kuwarithisha vijana.

"Endelezeni ligi hii iwe  miongoni mwa chachu  za kuleta Umoja na Mshikamano na isiwe chanzo cha mifarakano kwani aliyeasisi ligi hii hakuwa na nia mbaya bali alitaka kuimarisha  Muungamo wa wanavijiji wanaoshi ndani na nje ya makunduchi.

Pia Sekta ya  Michezo inaimarika kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, chini ya Uongozi wa Serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.", alisema Dk.Mabodi.

Alisema Jimbo la Makunduchi limekuwa ni kitovu cha kuenzi utamaduni wa asili ulioasisiwa na wazee wa vijiji vilivyomo katika Jimbo hilo hatua inayotakiwa kuendelezwa kwa vitendo na vijana wa sasa.

"Wazee wetu wametuachia vitu muhimu vya asili tunavyotakiwa kuvienzi kwa mfano ligi hii ya Mabodi Cup, Hasnuu Makame CUP, Sherehe za Mwaka kogwa pamoja na tamasha la vyakula vya asili linalowaunganisha wananchi wa Makunduchi na vijiji jirani." alisema.

Aidha aliwasihi wananchi wa jimbo hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeo yanayoletwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi mzuri wa CCM.

Dk.Mabodi  alisikishwa na kukemea vikali kuibuka kwa utashi binafsi wa kuigawa ligi hiyo katika makundi mawili  na kuagiza ligi hiyo iwe na jina moja la Mabodi CUP lenye uongozi mmoja na ligi nyingine yoyote itakayoibuka itafutiwe jina jingine mbadala kwa ajili ya kuimarisha ushindani wa kimichezo.

Dk. Dk.Mabodi aliahidi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza ligi hiyo iweze kutoa wachezaji wenye vipaji vya kucheza katika timu kubwa za kitaifa na kimataifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Unguja anayekaimu  Wilaya Kusini Unguja Rajab Ali Rajab alisema michezo ni sekta muhimu inayodumisha urafiki na afya za vijana.

Akizungumza Mgeni mwalikwa ambaye ni Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP) Mkoa wa Kilimanjaro Haji Miraj Abdallah alisema michezo ni sehemu muhimu ya kuwaunganisha vijana wa vikundi mbali mbali kuwa wamoja katika kulinda maslahi ya nchi.

SSP Haji aliwashauri vijana hao kujiepusha na vikundi viovu badala yake watumie vizuri vipaji vyao  kupitia michezo kwa kujiajiri wenyewe.

Awali mechi hiyo ya fainali katika ligi ya Mabodi CUP 2017-2018 ilizikutanisha timu mbili za Ubina na Maangaiko ambazo zote zilionyesha ujuzi wa soka na kumaliza mechi wakiwa wametoka sare ya 1-1.

Baada ya matokeo hayo mechi hiyo ilienda katika hatua ya penalti ambapo timu ya Maangaiko ilishinda kwa goli 4-2 dhidi ya timu ya Ubina.

Kupitia michuano hiyo Timu ya Maangaiko ambayo ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo walipata zawadi ya Shilingi milioni moja na kikombe cha mshindi wa kwanza na timu ya Ubina imepata shilingi 500,000 pamoja na kikombe cha mshindi wa pili.

Pia mshindi wa tatu alipata shilingi 300,000 mshindi wa nne amepata shilingi 200,000 ambapo timu nne zilizoshiriki mashindano hayo kila timu imepewa kiasi cha shilingi 75,000.

Katika fainali hiyo pia ilipambwa na michezi mingine ikiwemo ya kuvuta kamba pamoja na mbio za magunia ambapo kila mshindi wa kwanza katika timu za michezo hiyo amezawadiwa kiasi cha shilingi 50,000.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni