Jumatatu, 10 Septemba 2018

CATHERINE: AKEMEA UPOTOSHAJI KUHUSU UUZAJI WA KADI ZA CCM

 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Ndugu Catherine Peter Nao.



KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar ndugu Catherine Peter Nao amesema kadi za CCM haziuzwi wala sio kibali cha kutoa ajira bali zinapatikana kwa utaratibu uliowekwa Kikatiba.

Amesema serikali inatoa ajira kwa utaratibu wake iliyojiwekea kwa kuangalia vigezo na sifa za kitaaluma walizonazo waombaji wa ajira hizo lakini sio kwa vigezo vya kuwa na kadi ya Chama Cha Mapinduzi.

Amefafanua kwamba sharti la msingi kwa mtu yeyote kupata kadi ya CCM ni lazima  akubali kupewe mafunzo ya Itikadi kwa muda wa  miezi mitatu na sio kama wanavyopotosha baadhi ya watu wasiyoitakia mema CCM na serikali zake. 

Ufafanuzi huo ameutoa leo wakati akizindua darasa la Itikadi la CCM Mkoa wa Mjini kichama, uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa iliyopo Amani. 

Amesema endapo  Chama Cha Mapinduzi  kitabaini kuwepo kwa baadhi ya viongozi ama wanachama wanaojihusisha na vitendo vya kuuza kadi hizo watachukuliwa hatua kali za kimaadili.

Ameongeza kuwa Chama kimeendelea kuimarika na kadi zote za wanachama zitawekwa katika mfumo wa kisasa utakaokuwa na taarifa zote za wanachama na wataweza kuzitumia kadi hizo hata kwa huduma nyingine za kijamii.

“Kadi ya CCM haiuzwi mtaani wala haitowi ajira hivyo wananchi msipotoshwe na baadhi ya wanasiasa waliofilisika kisiasa na kuanza kutengeneza ajenda za upotosha wananchi.”, amesisitiza Catherine.

Katibu huyo wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Cathenine amewataka vijana hao wanaopata mafunzo ya itikadi kuwa wavumilivu wakati wa masomo hayo ili wawe viongozi bora wa sasa na baadae walioiva itikadi, uzalendo, falsafa na historia halisi ya Zanzibar.

Ameeleza kwamba changamoto kubwa iliyopo kwa vijana wa sasa ni kuwa na tamaa ya kupata nafasi za uongozi bila kupitia katika mafunzo mbali mbali ya uongozi na itikadi yanayowajenga kuwa viongozi imara na wenye misimamo isiyoyumba juu ya maslahi ya nchi.

Akizungumzia suala la ajira Catherine ameeleza kuwa licha ya kuwa ajira bni changamoto ya dunia nzima lakini serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kutoa fursa mbali mbali za ajira kwa vijana kupitia sekta za umma na binafsi.

Catherine amewasihi vijana hao kuendelea kuiamini na kuunga mkono serikali ya awamu ya Saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein anayetekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote bila ya ubaguzi wa kidini wala kikabila.

Kupitia uzinduzi huo Katibu huyo wa Idara ya itikadi na uenezi Zanzibar amesema CCM imejipanga vizuri kushiriki uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jan’gombe na kuhakikisha mgombea wa Chama hicho anaibuka mshindi na kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Katika juhudi za kuunga mkono Darasa hilo la itikadi Katibu huyo ametoa kiasi cha shilingi 350,000 kwa vijana hao ili ziwasaidie kugharamikia mahitaji mbali mbali katika mafunzo hayo.

Akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Ndugu Talib Ali Talib amesema Mkoa huo utaendelea kuwakusanya vijana mbali mbali kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya mafunzo mbali mbali yatakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Mjini  Ndugu Maulid Issa amesema mbali na vijana hao kupatiwa masomo ya itikadi pia wanapewa mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali na mafunzo ya lugha za kigeni ili wanufaike na soko la utalii kwa kujiajiri wenye kwa wale wasiokuwa na ajira.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni