KATIBU Mkuu wa CCM Tanzania Dk.Bashiru Ally akizungumza na makundi mbali mbali ya Vijana katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani Unguja |
BAADHI ya vijana wa UVCCM kutoka makundi
mbali mbali walioudhuria mkutano huo.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
|
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)
Tanzania Dk.Bashiru Ally amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa ya elimu
ili wapate ujuzi na maarifa ya kulinda na kusimamia rasilimali za nchi zisiporwe.
Rai hiyo ameitoa leo katika mwendelezo wa
ziara yake ya kujitambulisha visiwa humo wakati akizungumza na vijana kutoka makundi mbali
mbali ya Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM) katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa
Mjini uliopo Amani Unguja.
Amesema elimu ndio njia pekee ya kuwajenga
vijana wa CCM kuwa na fikra chanya za kulinda tunu za taifa lao zisihujumiwe
bali ziendelezwe kwa lengo la kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijanavyo.
Akizungumza na vijana zaidi ya 1560 kutoka katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar, ameeleza wazi kuwa elimu
hiyo itakuwa na manufaa zaidi endapo makundi hayo yatafuzwa siasa na itikadi
zinazoeleza historia halisi ya nchi yao ili wapate ujasiri wa kulinda Mapinduzi
ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa vitendo.
Dk.Bashiru amesema vijana waliopikwa
kiitikadi na kurithishwa siasa za ukombozi na ulinzi juu ya misingi ya kitaifa,
wanakuwa madhubuti katika kuendeleza kwa kazi Nyanja mbali mbali za kijamii,
kiuchumi kisiasa.
Katika kutilia mkazo malengo hayo Chama
kinajenga Chuo Kikuu cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo kibaha Mkoani Pwani, ambacho kitatoa viongozi
walioiva na kubobea katika siasa zenye tija zinazolinda misingi ya kitaifa kwa
maslahi ya jamii.
“ Vijana hamuwezi kulinda Mapinduzi ya
Zanzibar wala azimio la Arusha bila kujielimisha juu ya historia ya taifa lenu
ambalo ndio chimbuko ya vuguvugu la ukombozi wa nchi mbali mbali za bara la
Afrika.”amesema Dk.Bashiru.
Akizungumzia kuimarika kwa misingi ya
demokrasia nchini amesema viongozi wa CCM ndio walioasisi na kutoa baraka zote
juu ya mfumo huo.
Pia amesema milango ya Tanzania ipo wazi kwa
mataifa yanayotaka kuja kujifunza demokrasia hapa nchini kwani mfumo huo
unazidi kuimarika kila kukicha.
Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa baadhi ya
vikundi vinavyojiita vyama vya kisiasa na kutumiwa vibaya na mataifa ya kigeni
visiporudi katika mstari vitakufa kifo cha mende.
Katika mkutano huo Katibu Mkuu huyo amezitaja
sababu za CCM kuwa na mvuto kwa wananchi kwa kueleza kwamba kwa sasa imerudi
kwa wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.
Sababu nyingine amesema ni kutokana na
viongozi wakuu wa Serikali zinazotokana na CCM ambao ni Rais wa Zanzibar Dk.
Ali Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli ni wasafi kiungozi hawana kasoro za vitendo viovu vya rushwa na wizi
wa mali za umma.
“ Hizo ndio sababu za wapinzani kujiunga na
CCM kwani huko walipokuwa katika vyama vya upinzani kumejaa ubabe, rushwa na
mifumo dume ya kukandamiza haki na fursa za vijana na wanawake”, ameendelea
kueleza Dk.Bashiru.
Amewataka vijana kuendelea kuiunga mkono CCM
kwa kuhakikisha mwaka 2020 inashinda kwa lengo la kusimamia umoja,amani,
utulivu na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.
Akizungumzia
usimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa upande wa Zanzibar,
amempongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi kwa kasi yake ya
kuisimamia serikali kutekeleza dhana hiyo inayowaletea wananchi maendeleo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk.Abdulla
Juma Mabodi amesema CCM kwa upande wa
Zanzibar inaendelea na kazi ya kufanya siasa za ushindani wa sera kwa vitendo
zinazotekelezeka na sio maneno matupu.
Dk.Mabodi amesema katika juhudi za kuimarisha
taasisi hiyo kubwa ya kisiasa imeamua kuwa karibu zaidi na vijana wa rika
tofauti kwa kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Mapema akizungumu Makamu Mwenyekiti wa UVCCM
Taifa Tabia Maulid Mwita, amesema vijana hao wapo imara na watahakikisha
wanatekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya katika ya CCM ya mw aka 1977 toleo la
mwaka 2017 kwa kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka
2019 pamoja na serikali kuu mwaka 2020.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa CCM
Mkoa wa Magharibi Mohamed Rajab Soud amempongeza Katibu Mkuu wa hotuba zake
nzuri zenye na kuahaidi kuwa viongozi hao watayafanyia kazi kwa vitendo
maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM kwa la lengo la kuimarisha
Chama Cha Mapinduzi.
Mkutano
huo umehitimisha ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dk.Bashiru Ally kwa upande
wa Unguja, ambapo kesho anatarajia
kuendelea na ziara hiyo Kisiwani Pemba kwa kuzungumza na viongozi wa CCM na
jumuiya zake pamoja na makundi mbali mbali ya vijana wa Mikoa miwili ya
Kichama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni