Ijumaa, 17 Agosti 2018

DK.BASHIRU ATOA ONYO KALI KWA BALOZI ZA NCHI ZINAZOINGILIA SIASA ZA TANZANIA.

 KATIBU Mkuu wa CCM Tanzania Dk. Bashiru Ally akizungumza na mamia ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na Wananchi kwa ujumla katika viwanja vya Afisi ya Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
 

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk.Bashiru Ally amezitadharisha baadhi ya nchi za kigeni kuacha tabia ya kuingilia siasa za ndani ya nchi.

Amesema lazima nchi hizo hasa zenye balozi Tanzania ziheshimu Katiba na miongozo ya kisheria ya nchi, vinginevyo Tanzania itashindwa kuvumilia uchochezi unaofanywa na baadhi ya balozi nazowakilisha nchi hizo Tanzania.
  
Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika viwanja vya  Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar makuu, Dk. Bashiru amesisitiza kuwa Tanzania ni taifa huru linalojitawala lenyewe na hakuna nchi yoyote itakayoweza kuyumbisha demokrasia ya nchi hiyo.

Mkutano huo wa mapokezi ambao ni wa kwanza kwa Dk.Bashiru visiwani Zanzibar  toka alipoteuliwa kushika nafasi hiyo ya Ukatibu Mkuu wa CCM miezi kadhaa iliyopita, amekuja kujitambulisha kwa wanachama na viongozi mbali mbali wa CCM na jumuiya zake.

Amesema kumejitokeza baadhi ya mataifa yanayojifanya viranja wa demokrasia ambayo yamekuwa na tabia ya kutoa matamko ya kuhusu ushindi wa CCM wakati haijasajiliwa kufanya kazi za kisiasa.

Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa katika siku za hivi karibuni kumetokea taifa moja la kibeberu linatuma matamko kwenye mitandao ya kubeza ushindi wa CCM hivyo wanatakiwa waheshimu utawala na demokrasia ilioko nchini.

Dk.Bashiru amefafanua kuwa hakuna taifa lenye haki ya kubeza ushindi wa CCM inaoupata katika chaguzi ndogo zinazofanyika nchni, kwani kufanya hivyo ni kuingilia siasa za ndani za taifa hili.

Katika maelezo yake amebainisha kwamba kinachotakiwa kitambulike ni kuwa CCM haitishwi na matamko ya aina hiyo ya kuibeza na kwamba hawache kuidharau.

Amesema Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia ya kweli kwa kupitia misingi ya Azimio la Arusha na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 hivyo waache kuingilia shughuli za
uendeshaji wa Tanzania.

Amesema wanaandika matamko ya uongo ya kudanganya ulimwengu ya kuwa Tanzania hakuna uhuru na CCM ina iba kura kwenye uchaguzi na wanatakiwa kutambua CCM imeshinda kutokana na kuwa wananchi wamekuwa na matumaini na CCM katika kutekeleza ilani zake.

Dk.Bashiru ameongeza kwa kusema kuwa  uhuru wowote wa taifa haupatikani ovyo katika kujitawala, hivyo vijana wanatakiwa kuzingatia historia ya ukombozi wa taifa la Tanzania ili kuendeleza kudumisha amani iliyopo.

Aidha alisema, CCM imeamua kulinda rasilimani, mali na utu wake bila ya kuhitaji msaada wa viranja hao wa demokrasia katika utawala wao.

Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa uhuru huu ambao upo wa kujitawala umepiganiwa na haojapewa kwenye kupitia sahani ama msaada, hivyo aliwataka mataifa hayo makubwa na madogo kupitia balozi zake kuacha kudharau CCM ambayo imekomboa uhuru wa kujitawala.

Akizungumzia dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya alisema zinatakiwa kutekelezwa kwa vitendo kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ndani ya chama ili kiweze kuwa na nguvu za kutosha za kuendesha mambo yake chenyewe.

Amesema pia dhana hiyo imelenga kudhibiti vitendo vyote vya rushwa, ubinafsi na makundi maovu yaliyodhoofisha taasisi hiyo ya kisiasa kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine Dk.Bashiru amewaonya baadhi ya Wana-ccm walioanza kusaka nafasi za uongozi hasa Urais kabla ya muda wake na kuwambia kuwa wasipoacha tabia hiyo watashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za kimaadili ndani ya Chama Cha Mapinduzi

Aliongeza kuwa bado Zanzibar ina Rais wake na hajamaliza muda wake hivyo hakuna haja ya watu kuanza kampeni za kusaka kiti hicho.

Kupitia mkutano huo Dk.Bashiru amewapokea vigogo wawili ACT wazalendo visiwani humu ambao ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Ramadhani Suleiman na Katibu Mkuu wake Khamis Ali Lila amabye aliyewai kugombe nafasi ya urais mwaka 2016.

Pia amewapokea wanachama 35 kutoka Chama cha CUF, ambao wote walikuwa ni wanachama wa CUF katika maskani maarufu ya Mtendeni Mkoa wa Kusini Unguja kijiji cha Makunduchi, na wote wamejiunga na CCM. 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Zanzibar Abdulla Juma Saadalla(Mabodi), amesema chama kimejipanga vizuri na wanachama katika ngazi zote tayari wameshashuka nyumba kwa nyumba kujua changamoto zinazowakabili wananchi ili zifanyiwe kazi kwa vitendo.

Pamoja na hayo ameongeza kuwa CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020  kwa vitendo ili wananchi waendelee kunufaika na maendeleo yanayoletwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mabodi ameahidi kulinda,kuendeleza na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kulinda kwa vitendo Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani ndio sehemu ya kudumisha udugu uliopo baina ya nchi hizo mbili zilizoungana zote zikiwa huru.

Mapema akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib amesema hali ya kisiasa katika mkoa huo ipo shwari na CCM imeendelea kuimarika zaidi kutokana na sera zake nzuri zinazokubalika na makundi yote katika jamii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni