BAADHI ya viongozi na wanachama wa CCM walioudhuria katika ziara hiyo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein. |
WANANCHI walioudhuria katika ziara hiyo ya Dk.Ali Mohamed Shein.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amesema serikali itaimarisha taasisi zote za utafiti nchini ziweze kufanya utafti wenye hadhi ya kimataifa. Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifanya ziara katika taasisi mbali za utafiti ambazo ni taasisi ya Utafti wa Mifugo Langoni Kizimbani Wilaya ya Magharibi "A" pamoja na Taasisi ya Utafti wa masuala ya Afya iliyopo Wilaya ya Kati Zanzibar. Amesema Taasisi hizo ni nyenzo za kuharakisha maendeleo ya Zanzibar kwani katika ulimwengu wa sasa kila jambo lenye kuleta maendeleo ama madhara katika jamii lazima lifanyiwe Utafti wa kitaalamu. Dk.Shein Akizungumza mara baada ya kukagua eneo litakalojengwa Hospitali kuu ya kisasa Zanzibar, ambayo itakuwa na taasisi ya utafti ya Afya itakayotoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili waweze kuwa na ujuzi mkubwa wa kutoa huduma za afya kitaalamu. Amesema ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika itawasaidia wananchi wa maeneo mbali mbali ya Zanzibar na kupunguza msongamano wa wananchi kwenda kufuata huduma za Afya katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Dk.Shein ameongoza kuwa hatua hizo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa lengo la kutatua changamoto za wananchi na kuwaletea maendeleo. Ameeleza kwamba CCM inaendeleza utamaduni wake wa asili wa kutekeleza kwa vitendo miradi mbali mbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote. "Hospitali hii itakapokamilika itakuwa na uwezo mkubwa wa vifaa tiba, wataalamu na miundombinu ya kisasa ya masuala ya Afya hivyo wananchi mnaoishi karibu na eneo hili muunge mkono juhudi za serikali. Pia vijana wetu wenye utaalamu wa masuala ya Afya watakuja hapa kupata mafunzo na kufanya utafti wa tiba za maradhi mbali mbali na kuwatibu wananchi.",amesema Dk.Shein. Akikagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Taasisi ya utafti wa Mifugo huko Langoni Unguja, Dk.Shein amesema taasisi hiyo itasaidia kufanya utafti wa Mifugo hapa nchini na kupunguza gharama za kwenda Tanzania bara na maeneo mengine kufanya utafti huo. Mapema Akizungumza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafti wa Mifugo Zanzibar,Dk.Kassim Gharib Juma amesema taasisi hiyo tayari imefanya utafti mbali mbali wa mifugo ikiwemo Ng'ombe,Mbuzi na kuku ulioweza kuleta tija kwa kubaini maradhi na njia za kitaalamu za kukabiliana na changamoto hizo pamoja na ufugaji bora wa Mifugo hiyo. Pia alieleza kwamba wamefanya utafti wa kutengeneza chakula cha wanayama kupitia zao la mwani, ambao utasaidia kuzalisha chakula bora cha mifugo hapa nchini. Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Halma Maulid Salum amesema ujenzi wa majengo mbali mbali ya Taasisi ya utafti wa afya pamoja na Hospitali katika eneo la Binguni Wilaya ya Kati Unguja hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha shilingi bilioni nne. Ameeleza kuwa Wizara ya Afya itasimamia kikamilifu ujenzi wa majengo hayo ili taasisi hiyo itowe huduma bora za Afya kwa jamii. Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla (Mabodi), amempongeza Dk.Shein kwa mfumo mzuri wa uongozi shirikishi baina ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema mambo mema yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya Saba Zanzibar chini ya uongozi wa Dk.Shein inafuata nyayo za utawala wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar hayati Abeid Aman Karume kwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayodumu kwa muda mrefu kwa maslahi ya jamii. Amesema kazi kubwa inayofanywa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha huduma muhimu za kijamii ni miongoni mwa kibali halali cha kisiasa cha kuiletea ushindi CCM katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni