WAZIRI wa Fedha na
Mipango Zanzibar Dkt.Khalid Mohamed Salum akifungua mkutano wa kujadili
maazimio ya kongamano la siku ya vijana Duniani uliofanyika hoteli ya Ngalawa
Bububu. |
MWENYEKITI wa Baraza
la Vijana Zanzibar, Khamis Rashid Kheir akizungumza katika mkutano huo. |
MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Maulid Mwita akisoma maazimio hayo 14 yaliyowasilishwa katika kongamano la vijana 300 lililofanyika Augost 9 mwaka huu. |
MWENYEKITI wa muda Mkutano huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid akiongoza mkutano huo wa kujadili maazimio 14 ya vijana. |
WAZIRI wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohamed akizungumza katika mkutano huo. |
MBUNGE wa viti maalum (CCM) kupitia nafasi za Vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Khadija Nassir Ali akichangia maazimio mbali mbali katika mkutano huo. |
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib akizungumza katika Mkutano huo. |
NAIBU Mkurugenzi wa Manispaa ya Mjini Zanzibar , Said Natepe akizungumza katika mkutano huo. |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Leila Burhan Ngozi akizungumza katika mkutano huo. |
NAIBU Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi akichangia juu ya mikakati ya CCM
ya kuwezesha vijana.
|
KATIBU Mkuu Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar akizungumza katika Mkutano huo. |
BAADHI ya washiriki wa mkutano huo. |
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharib Ayoub Mohamed Mahmoud akifunga Mkutano huo wa siku moja uliofanyika katika Hoteli ya Ngalawa Bububu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. |
NA IS-HAKA OMAR,
ZANZIBAR.
WAZIRI wa Fedha na
Mipango Zanzibar Dkt.Khalid Salum Mohamed amesema uchumi wa Zanzibar utaendelea
kukua kwa kasi endapo vijana watashirikishwa ipasavyo katika mipango ya
maendeleo.
Alibainisha kwamba
taifa lolote linaloshindwa kushirikisha ipasavyo kundi hilo katika mikakati
yake ya kimaendeleo basi taifa hilo haliwezi kupata maendeleo badala yake
uchumi wake utayumba na kuendelea kuwa tegemezi kwa mataifa yaliyoendelea.
Hayo aliyasema wakati
akifunga mkutano wa kujadili maazimio 14 ya kongamano la siku ya vijana duniani
kwa viongozi mbali mbali lililofanyika katika hoteli ya Ngalawa nje kidogo ya
Mji wa Zanzibar.
Dkt.Khalid alisema
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kuwaweka karibu vijana
ilianzisha kwa makusudi Baraza la Vijana la Taifa ili kundi hilo lipate sehemu
maalum ya kukutana pamoja na kujadili masuala mbali mbali ya kuisaidia nchi
kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alieleza kuwa vijana
ndio nguvu kazi ya taifa lolote kwani kila jambo jema la kuiletea nchi manufaa
linasimamiwa kwa kiasi kikubwa na kundi la vijana wenye taaluma na uwezo mzuri
wa kufikri mawazo chanya ya kuisadia nchi kimaendeleo.
Alisema siri ya
mafanikio katika nchi mbali mbali zilizoendelea kiuchumi ni kutokana na mbinu
za kutumia vizuri rasilimali watu ya vijana, waliosaidia kuinua kwa kasi
mikakati endelevu ya kiuchumi na kijamii kupitia sekta mbali mbali hasa za
uzalishaji mali na viwanda.
Waziri Dkt. Khalid
alizitaja takwimu za kiuchumi, kwa kufafanua kuwa mwaka 2018 uchumi wa Zanzibar
unatarajia kukua kwa asilimia 7.7 ikilinganishwa na mwaka, 2017 ambapo umekuwa
kwa asilimia 7.5.
Alisema uchumi huo ni
lazima uwe jumuishi na endelevu unaogusa makundi yote ya kijamii.
“Wananchi sote lazima
tushiriki kupanga na kukuza uchumi wetu ili uwe endelevu na wenye maslahi ya
kutunufaisha wote, na hapo ndipo tutakapokuwa tumefikia malengo ya serikali ya
kufikia kiwango cha nchi zenye uchumi wa kati.
Imani yangu kwa nyie
vijana mlioshiriki kongamano hili na wengine waliopo katika shughuli mbali
mbali za ujenzi wa taifa ambao hawakuweza kujumuika nasi hapa, leo hakika
matarajio haya yatafikiwa kwa haraka na kwa ufanisi.
Aliwasisitiza vijana
kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kuachana na mazoea ya kubagua
kazi kwa kigezo cha kusubiri ajira kutoka serikalini.
Alisema hakuna nchi
iliyoweza kuwaajiri vijana wote kwani sekta binafsi ndio chombo pekee chenye
fursa pana za kutosheleza mahitaji ya ajira kutokana na wingi wa vijana.
Kupitia sekta binafsi
serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaimarisha sekta mbali mbali zikiwemo za
kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, kuboresha uvuvi wa bahari kuu na kuwa wa
kisasa wa kuwasaidia vijana kujiajiri wenyewe.
Pia serikali imetenga
zaidi ya shilingi bilioni tatu kutekeleza sera ya viwanda Zanzibar, sekta
ambayo endapo wananchi wataipokea kwa dhati itaweza kupunguza au kumaliza
kabisa changamoto za ajira nchini.
Pamoja na mikakati
hiyo Dkt. Khalid alibainisha kwamba serikali imekusudia kuwekeza zaidi katika
sekta ya utalii ili uwe sehemu mahsusi ya kuongeza pato la taifa, sambamba na kuimarisha
kwa vitendo dhana ya utalii kwa wote.
Alitoa wito kwa
vijana kuthamini, kutangaza na kuunga mkono hatua za maendeleo zinazofanywa na
serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, katika
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020.
Akizungumza
Mwenyekiti wa Baraza Vijana Zanzibar, Khamis Rashid Kheir amesema kongamano
hilo limefungua fursa mbali mbali za vijana ambao wengi wao wamepata kujua
sehemu sahihi za kuwasilisha changamoto zao na zikafanyiwa kazi kwa haraka.
Naye Makamu
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Maulid Mwita, akiwasilisha maazimio 14
yaliyotolewa na vijana 300 walioshiriki katika kongamano la kuelekea
maadhimisho ya siku ya vijana Duniani
yaliyofanyika August 9 mwaka 2018, alisema vijana wanatakiwa kuzitumia vyema
fursa za kilimo, ufugaji na uvuvi ili kujiajiri wenyewe.
Makamu Mwenyekiti wa
UVCCM Taifa Tabia, maazimio mengine aliyataja kuwa ni pamoja na kuiomba
serikali kuandaa sera na sheria shirikishi zitakazotoa kipaumbele cha
kuwanufaisha vijana wa Zanzibar kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Akizungumza katika
kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi
alizishauri taasisi za vijana zilizobuni kongamano hilo kuendeleza utamaduni
huo wa kukutana mara kwa mara kujadili masuala muhimu yanayogusa maendeleo ya
nchini na ustawi wa tasisi zao.
Alisema CCM
Zanzibar inaunga mkono harakati za
vijana wa makundi yote hasa wale wanaoanzisha vuguvugu la kujadili masuala
mbali mbali ya kuimarisha maendeleo, amani,utulivu na umoja wa kijamii kwa
maslahi ya nchini.
“Hatuwezi
kuizungumzia historia ya Zanzibar bila kutaja vijana kwani waasisi wa ASP
walianzisha harakati za kuikomboa Zanzibar kutoka katika utawala wa kibabe,
viongozi hao walikuwa ni vijana.”, alieleza Dk.Mabodi.
Wakichangia maazimio
hayo washiriki mbali mbali kutoka taasisi za Serikali, Vyuo vya elimu ya juu na
taasisi za kisiasa wamesema pamoja na mikakati mizuri ya serikali ya kuwajengea
mazingira mazuri vijana bado kundi hilo linatakiwa kujitathimini na kurudi
katika misingi ya uzalendo.
Walisema endapo
vijana hawatokuwa na misingi imara ya kuishi katika misingi ya uzalendo juu ya
nchi yao, kuna hatari ya Zanzibar huko miaka ijayo kushindwa kufikia malengo
yake ya kuwa nchi yenye nguvu kiuchumi na kimaendeleo kwani vijana wengi watatumia
elimu zao kuhujumu maendeleo badala ya kuyalinda na kuyaendeleza kwa maslahi ya
wote.
Akifunga Mkutano huo Mkuu wa Mkoa Mjini
Magharibi, Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud amewataka vijana kujiamini na kupanga
mikakati madhubuti ya kuimarisha taasisi zao ili ziwe chachu ya kutatua
changamoto zilizowazunguka.
Mhe. Ayoub
amezipongeza taasisi hizo za vijana kwa kuandaa kongamano lenye tija lililoweza
kujadili mambo mengi yanayohusu taifa kwa muda mfupi na kupata maazimio
madhubuti yanayolenga kumaliza changamoto zinazowakabili katika kazi zao za
kila siku.
Pamoja na hayo Mkuu
wa Mkoa huyo, Mhe. Ayoub alitoa rai kwa vijana kuacha tabia za kulalamika na
badala yake wafuatilie kwa karibu mambo mbali mbali yanayowahusu katika sehemu
husika ili yapatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Kongamano hilo
lililoendeshwa na taasisi mbali mbali zikiwemo Wizara ya Vijana,utamaduni,sanaa
na michezo Zanzibar, Baraza la vijana Zanzibar pamoja na UVCCM Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni