MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Julai 9, mwaka 2018 ameongoza Kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar.
Makamu wa Rais Mhe. Samia ameongoza kikao hicho baada ya kupendekezwa na wajumbe wa kikao kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Ibara ya 108 (4) ili aongoze kikao hicho kwa niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk. Ali Mohamed Shein aliyesafiri nje ya nchi kikazi.
Kikao hicho kimefanyika kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:30 mchana katika ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Kisiwanduzi Zanzibar.
Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya kujadili kwa kina majina 19 ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi waliojitokeza kugombea nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Jang’ombe Zanzibar.
Wanachama hao 19 walioomba nafasi hiyo na kupendekezwa katika ngazi za jimbo, wilaya na Mkoa, Kikao hicho kimeweka alama zinazostahiki kwa wagombea wote na kupendekeza kwa Kamati Kuu ya CCM Taifa ili irejeshe majina matatu au kama itakavyoona inafaa kwa ajili ya kura ya maoni kwa lengo la kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Kikao hicho ni maalum kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017, ibara ya 109 (1) na 7(b).
Mchakato huo unafanyika kutokana na Jimbo la Jang’ombe kuwa wazi baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Abdalla Diwani kufukuzwa uanachama wa CCM hivi karibuni baada ya kukiuka maadili na miongozo ya Chama.
BAADHI ya Wajumbe wa Kikao hicho |
WAGOMBEA 19 wa CCM wanaowania nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Jang'ombe wakiwa katika picha ya Pamoja. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni