Ijumaa, 20 Julai 2018

CCM Z'BAR YAWAPIGA MSASA VIONGOZI NA WATENDAJI WA JUMUIYA ZAKE.



 

Wakuu wa Idara za CCM Zanzibar pamoja na Makamu Wenyeviti wa Jumuiya za CCM Taifa wakiimba nyimbo za CCM  mara baada ya kuingia katika ukumbi wa Mkutano wa Afisi Kuu CCM Kisiwandui Zanzibar, kwa ajili ya kikao.

 

BAADHI ya viongozi na Watendaji hao wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi wakifuatilia kwa makini maelekezo yanayotolewa na viongozi wa CCM kupitia Kikao hicho, kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.


 Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mgeni Hassan Juma akitoa nasaha kwa viongozi na watendaji hao juu ya uimarishaji wa CCM na Jumuiya zake.

 
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Ndugu Catherine Peter Nao (aliyesimama katikati), akizungumza na viongozi na watendaji wa Jumuiya tatu za CCM Z’bar wakiwemo Wabunge na Wawakilishi wa Viti Maalum.

 BAADHI ya viongozi na watendaji mbali mbali wa Jumuiya tatu za CCM wakiimba nyimbo za Chama cha Mapinduzi baada ya viongozi wa Chama kufika ukumbini.




CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar kimewataka watendajii na viongozi wa Jumuiya zote za Chama kufanya kazi zao kwa ushirikiano ili taasisi hiyo iendelee kuwa kinara wa kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi sera na mikakati yake ya  maendeleo kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar  Ndugu Catherine Peter Nao wakati akizungumza na Viongozi mbali mbali wa Jumuiya tatu za Chama cha Mapinduzi wakiwemo Makamu Wenyeviti, Wabunge na Wawakilishi wa viti maalum pamoja na Makatibu wa Jumuiya hizo huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Katibu huyo  wa Kamati Maalum ya NEC, Catherine alisema uimara wa CCM unatokana na ushirikiano uliotukuka unaofanywa na viongozi na watendaji wa ngazi mbali mbali za Chama na Jumuiya zake, ambao kimsingi ndio nyenzo pekee ya kusimamia sera za Chama zitekelezwe kwa ufanisi.

Catherine ambaye toka ateuliwe kushika nafasi hiyo hicho ni Kikao chake cha mwanzo kuzungumza na viongozi hao, alisisitiza kuwa kila kiongozi kwa sasa anatakiwa kutekeleza wajibu wake katika kupanga na kubuni mikakati endelevu ya kufanikisha ushindi wa CCM mwaka 2020.

“ Kila tunapokutana tukiwa ni viongozi tuliaminiwa na Wana- CCM kuwa tunaweza kuongoza kwa uadilifu jahazi hili mpaka mwaka 2022 ni lazima tujadili kwa kina namna ya kutekeleza kwa vitendo Ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2012, inayoeleza kuwa ushindi wa CCM ni lazima katika uchaguzi Mkuu na wa serikali za mitaa.”, aliwakumbusha viongozi hao Catherine.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, aliwapongeza wabunge na wawakilishi wanaofuata nyayo za Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa CCM wanaotekeleza kwa kasi Ilani hiyo kwa kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia aliwataka wabunge na wawakilishi wa viti Maalum kwenda sambamba na kasi hiyo ya utekelezaji wa Ilani ili Chama Cha Mapinduzi kiweze kutatua kwa kiwango kikubwa kero zinazowakabilli wananchi kabla ya mwaka 2020.

Aidha Ndugu Catherine aliwambia viongozi hao kwamba pia wana jukumu la kushiriki ipasavyo katika mipango ya kukijenga Chama hasa katika mipango ya kuongeza wanachama wapya ambao ndio rasilimali ya kudumu ya kisiasa kwa Chama cha Mapinduzi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Taifa,  Ndugu Abdallah Haji Haidar alisema kila kiongozi aliyepewa dhamana ya uongozi anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa kufanya kazi za Chama kwa bidii ili taasisi hiyo iendelee kuongoza dola.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Ndugu Tabia Maulid Mwita alisema vijana wapo tayari kufanya kazi za Chama na za ujenzi wa Taifa muda wowote kwani wapo kwa ajili ya kulinda na kutetea mambo mema yaliyoasisiwa na Vijana wa ASP kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma alisema maelekezo yaliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi watayafanyia kazi ili kwenda sambamba na siasa za ushindani wa kisera na utatuzi wa changamoto za wananchi kwa wakati.

Nao Wawakilishi na Wabunge hao wa viti maalum, waliahidi kuendeleza ushirikiano na viongozi wenzao katika kutekeleza mambo mema yatakayoimarisha CCM katika nyanja za kisiasa na kiuchumi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni