UTANGULIZI.
Ndugu Waandishi wa Vyombo
mbalimbali vya Habari.
ASSALAM ALEYKUM.
Awali
ya yote, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi
na Vyote viliyomo Ndani yake, kwa kutujaalia uzima na afya njema. Aidha,
nachukua nafasi hii kwa mara nyengine tena kuwashukuru ninyi Waandishi wa
Vyombo mbali mbali kwa kukubali wito wetu na kuhudhuria kikao hiki pamoja na
majukumu kadhaa mliyonayo ya kulihabarisha Taifa.
Ndugu Wanahabari,
Bila
ya kupoteza muda, lengo kuu la kukuiteni hapa leo hii si jengine bali ni kutoa salamu za pongezi kwa Rais Mteule
wa Zanzibar Mhe. Daktari Ali Mohamed
Shein, kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na Wazanzibari hasa Wana CCM hapo
tarehe 20 Machi, mwaka huu na hatimaye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) Mhe. Jecha Salim Jecha, jana (21/03/2016) kumtangaza rasmi kuwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kipindi cha miaka
mitano ijayo (2015 - 2020).
Kwa
mnasaba huo basi, Chama Cha Mapinduzi kinampongeza kwa dhati kabisa aliyekuwa
mgombea wa Chama chetu Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kupata kura halali 299,982
(91.4%). Hakika ni ushindi
mkubwa ambao haujapata kutokea katika historia ya demokrasia ya vyama vingi kwa
upande wa Zanzibar.
Pia
ushindi huo umedhihirisha wazi kuwa bado wananchi wa Zanzibar wana imani kubwa
na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na utekelezaji mzuri wa ilani ya chama
hiki.
Aidha,
CCM inampongeza kwa mara nyengine tena kwa hotuba nzuri aliyoitoa katika hafla
ya kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Marudio, iliyofanyika jana, ambapo
Mhe. Dkt. Shein aliwaahidi Wananchi kuendeleza suala zima la Amani na utulivu wa
Taifa, ili kuwafanya watu waweze
kujiendeleza kimaisha.
Sambamba
na hilo, Mhe. Rais Shein Mteule huyo, alielezea nia yake ya kusimamia kwa nguvu
zote Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 - 2020 na kuinua
hali ya kiuchumi kutoka asilimia 7.0 (sasa) kufikia asilimia 10.
Ushindi
huo, aliopata Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, haukuja hivi hivi tu, bali umetokana
na juhudi na mashirikiano ya pamoja baina ya Viongozi na Wanachama wa CCM na
Jumuiya zake wa ngazi zote Unguja na Pemba.
Kama
hiyo haitoshi, Wazanzibari wameshawishika na maendeleo yaliyoletwa na CCM chini
ya Uongozi uliotukuka wa Rais wa Zanzibar mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, ikiwa ni
Utekelezaji wa kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 - 2015.
Ndugu Wanahabari,
Chama
Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwapongeza pia wana CCM na wananchi wa
Unguja na Pemba kwa kutumia kikamilifu haki yao ya demokrasia na hatimaye
kufanya maamuzi sahihi na kukichagua Chama Cha Mapinduzi na hivyo kuipa ridhaa
ya kuongoza dola Tanzania Bara na Zanzibar katika kipindi cha miaka 2015 -
2020.
CCM
pia, inawapongeza Viongozi, Watendaji na Wanachama wa Chama hicho (ngazi zote)
pamoja na wananchi kwa ujumla, kwa kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji kura na
hatimaye kufanya maamuzi sahihi katika Uchaguzi huo wa Marudio, uliofanyika
machi 20, mwaka huu, nchini kote.
Sambamba
na hilo, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, pia kinavipongeza kwa dhati Vyombo vya
Ulinzi na Usalama kwa kusimamia kikamilifu suala la ulinzi katika Mikoa yote ya
Zanzibar kabla na wakati wote wa zoezi la upigaji kura, hali iliyotoa fursa kwa
wananchi kuweza kutekeleza haki yao hiyo ya kidemokrasia.
Mwisho, nawapongeza kwa
dhati wadau mbali mbali waliofanikisha kwa namna moja ama nyingine uchuguzi mkuu huo wa Marudio kwa amani na utulivu.
‘KIDUMU
CHAMA CHA MAPINDUZI’
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni