Ijumaa, 8 Juni 2018

KATIBU MKUU MPYA WA UWT MWL. QUEEN MLOZI AZUNGUMZA NA WENYEVITI NA MAKATIBU WA UWT Z'BAR

 KATIBU Mkuu wa UWT Taifa Ndugu Queen Mlozi akizungumza na viongozi na watendaji wa Umoja huo ngazi za Mikoa na Wilaya Zanzibar, Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar  katika ziara yake ya kujitambulisha.

 BAADHI ya Wenyeviti na Makatibu wa UWT wa Mikoa na Wilaya wakisikiliza hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja huo Taifa.

 VIONGOZI wakuu wa UWT Taifa wakiomba dua katika kaburi la Mwasisi wa Mapinduzi ya mwaka 1964 ambaye pia alikuwa ni Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Abeid Amani Karume.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza na viongozi wakuu wa UWT Taifa waliofika Ofisini kwake, Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akielezea historia ya eneo alilouawa na wapinga maendeleo aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Aman Karume.

 

  SPIKA  wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid(kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi. Gaudencia Kabaka(kulia) alipofika katika Baraza hilo kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza na Wawakilishi wanawake katika Baraza hilo.

  NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma (kulia) akimkabidhi Katiba ya Jumuiya ya wawakilishi wanawake katika Baraza hilo Katibu Mkuu wa UWT Taifa, Bi. Queen Mlozi (kushoto).KATIBU Mkuu wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT)Taifa, Ndugu Queen Mlozi ameahidi kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uzalendo uliotukuka ili CCM ishinde katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa ngazi mbali mbali za UWT Zanzibar  hapo Afisi Kuu CCM Kisiwandui  katika ziara yake ya kwanza kujitambulisha kwa viongozi na watendaji  hao.

Alisema atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa lengo la kuimarisha  taasisi hiyo ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ndani ya Umoja huo na Chama kwa ujumla.

Ameeleza kwamba wanawake wa UWT wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kulinda maslahi ya CCM ili ishinde kwa ngazi zote kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar katika uchaguzi Mkuu ujao.

Katibu Mkuu huyo amewashukuru viongozi viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi waliomuamini na kumteuwa kushika nafasi hiyo ya ngazi ya juu ya kiutendaji kupitia Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es saalam.

“ Viongozi na wanachama wote nakuahidini kwamba nitatumia weledi na uzoefu wangu wote kwa kuhakikisha UWT inaendelea kuwa imara na mkombozi na mtetezi mkubwa wa maslahi ya wanawake wote nchini”, alisema Queen.

Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndugu Gaudencia Kabaka alisema ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi mbali mbali wa Umoja huo na Chama unampa nguvu na imani ya kusimamia maslahi ya taasisi hiyo bila hofu.

Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, ndugu Thuwayba Kisasi alisema lengo la ziara hiyo ni Katibu Mkuu huyo mpya  ujitambulisha kwa viongozi wa umoja huo pamoja na kuzungumza na Wawakilishi wanawake wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi alizungumza na msafara wa viongozi hao wa UWT Taifa aliwaeleza kuwa CCM Zanzibar inajivunia uwepo wa umoja huo kwani unafanya kazi kubwa ya kusimamia na kutekeleza kikamilifu sera za Chama kwa makundi yote yaliyopo katika jamii.

Viongozi hao walitembelea Baraza la Wawakilishi Zanzibar  wakazungumza na viongozi mbali mbali wakiwemo Spika wa Baraza hilo Mhe. Zubeir Ali Maulid pamoja na Naibu Spika Mhe. Mgeni Hassan Juma na wakaelezwa masuala mbali mbali ya kiutendaji yanayofanyika katika Baraza hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni