Jumapili, 16 Juni 2019

NDG.THUWAYBA NA MHE.ANGELINA WAWAPIGA MSASA WANAWAKE WA KASKAKAZINI UNGUJA.

 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Edington Kisasi akifungua mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura na suala la mikopo kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini Unguja. Kulia ni Mbunge wa viti maalumu wa mkoa huo, Angelina Adam Malembekakushoto ni Mwenyekiti wa UWT Mkoani humo Maryam Muharami Shomari


 MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Kaskazini Unguja, Angelina Adam Malembeka (kulia) akihamasisha jambo kwenye mkutano mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura na suala la mikopo kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini Unguja. 




 VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuwasaidia viongozi waliochaguliwa kuteleleza ilani na ahadi walizozitoa wakati wa uchaguzi uliopita badala ya kukumbatia wagombea wa uchaguzi ujao.

Akifungua mafunzo ya siku moja yaliyoshirikisha viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM mkoani humo, Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Eddington Kisasi alieleza kuwa kufanya hivyo kunapelekea viongozi waliopo madarakani kushindwa kusimamia ahadi zao.

Alisema wapo baadhi ya viongozi wa chama lkatika ngazi mbali mbali wameanza kuwakumbatia wanachama 'wanaojipitishapitisha' kwa lengo la kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao watambue kuwa kufanya hivyo wakati huu ni kukiuka kanuni za uchaguzi za chama hicho.

Mafunzo hayo yaliyolenga kuhamasisha ujasiriamali na mikopo kwa wanawake na uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yaliandaliwa kwa pamoja kati ya mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka na UWT Mkoa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi iliyoagiza kuinuliwa kwa hali za kiuchumi za wanawake katika ngazi zote.

Alisema kanuni za uchaguzi za CCM zinakataza mtu kufanya kampeni kabla ya wakati hivyo viongozi wanaoandaa wagombea na kupanga nao mikakati wanapaswa kujua kuwa wanachochea vurugu ambazo zinakwaza kasi ya utekelezaji wa ilani na kuchelewesha upatikanaji wa maendeleo ya jamii.

"Chama kiliweka muongozo na ndio maana Mwenyekiti wetu (Dk. John Magufuli) alikataza Mambo ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ili tupate kuteleleza ahadi tulizoweka kwa wananchi wetu na nyinyi no mashahidi kwamba kabla ya 2020 tumeshatekeleza ilani kwa zaidi ya asilimia 90 Tanzania bara na Zanzibar", alieleza Kisasi.

Aidha aliwataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri na kuisambaza elimu waliyopatiwa kwa wanachama wenzao kwani yana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii na siasa za Tanzania.

"Tuliahidi kuinua uchumi wa wanawake katika ilani ya uchaguzi kupitia njia mbali mbali zikiwemo za ujasiriamali na uanzishwaji wa viwanda hivyo mafunzo haya yana mchango mkubwa katika kuendeleza vikundi vya kiuchumi tulivyonavyo katika shehia, wadi, wilaya na mikoa yetu", alisema Makamu huyo wa Mwenyekiti.

Aidha aliwataka wajasiriamali nchini kutumia fursa ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki iliyoanza Juni mosi mwaka huu Tanzania bara, kutengeneza mifuko mbadala ya kubebea bidhaa na kuipeleka huko ili kujiendeleza kiuchumi.

Akizungumzia uimarishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Kisasi aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kwenda kuhakikisha taarifa zao na kuwasaidia vijana wenye sifa waweze kujiandikisha.

"Utekelezaji wa ibara ya 5 ya katiba ya chama chetu wa kushinda uchaguzi haupo wakati wa uchaguzi pekee bali huanza mapema na huu ndio wakati wake ili kuzichungachunga kura za ushindi wetu ifikapo 2020", alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.

Akiwasilisha mada juu ya ujasiriamali na mikopo Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na elimu ya ujasiriamali na utoaji wa mikopo ya jijini Dar es salam Nickson Martin alisema ili kuwa na uzalishaji wenye tija ipo haja ya wajasiriamali kuzingatia elimu na uwekaji kumbukumbu za biashara zao kujua maendeleo ya shughuli zao.

"Ni lazima mkubali kubadilika na kuweka mikakati kuzifikisha ndoto zenu na za serikali yetu ya kuimarisha uchumi wa watu wake kupitia uchumi wa viwanda", alisema Nickson.

Nae Katibu Msaidizi wa CCM mkoani humo Shafi Hamad Ali akiwasilisha mada ya umuhimu wa daftari la kudumu alisema viongozi wa ngazi zote za chama hicho wanapaswa kujidhatiti na kuhakikisha wanatekeleza maagizo na maelekezo ya chama kama inavyoelekezwa na katiba ya CCM na ya jumuiya zake.

"Msingi wa ushindi katika uchaguzi wa chama chetu ni umoja na mshikamano na ndio maana sote tunawajibika kuhakikisha chama kinashinda katika chaguzi za kutafuta dola na daftari ndio chanzo cha ushindi siku zote", alisema Shafi.

Akitoa shukran za washiriki wa mafunzo hayo Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka alieleza kuwa ataendelea kuwatafutia wanawake wa mkoa huo fursa za kujikomboa kiuchumi ili waweze kujitegemea na kusaidia maendeleo ya familia zao.

Alisema iwapo wanawake hao watatumia kikamilifu fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za serikali na za binafsi wanaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda.

Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo aliyowahi kuwapatia wananchi wa mkoa huo kwsa kushirikiana na wadau mbali mbali ambapo hapo awali makundi mbali mbali ya wanawake yalipatiwa mafunzo ya utengenezaji chaki na mishumaa ili kujiongezea kipato.

"Baada ya kupata mafunzo yale nimeona nije na haya ya kuwaonesha fursa za kuendeleza miradi yetu ili siku moja tuwe na viwanda vidogo vidogo na vya Kati, hapo tutakuwa tumejikomboa kiuchumi kweli kweli", alisema Malembeka.

Alizungumzia mafunzo hayo mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo ambae ni Katibu wa UWT jimbo la Kijini Maryam Rashid Mussa alisema yamewasidia kuziona na kutambua fursa za misaada na kwamba watayatumia kuimarisha mitaji yao na chama kwa ujumla.

Mafunzo hayo yalishirikisha jumla ya viongozi wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa  huo 120 yalifungwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa anaetokea jumuiya ya wazazi Tanzania Suleiman Juma Kimea ambae aliwasisitiza washiriki mafunzo hayo kusimamamia misingi na maadili ya chama hicho ili kuepuka mizozo isiyo ya lazima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni