Jumamosi, 15 Juni 2019

DK.MABODI: ATOA MAAGIZO CCM MFENESINI.



 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi,akiwahutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mfenesini na Wageni Waalikwa katika Mkutano wa kawaida wa Halmashauri hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.



NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amewataka Wanachama,Viongozi na Watendaji wa CCM Wilaya ya Mfenesini kuhakikisha Taasisi hiyo inashinda Majimbo yote ya Uchaguzi ndani ya Wilaya hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi 'A' Unguja.

 Amesema Viongozi na Watendaji hao kwa kushirikiana na Wanachama na Makada  mbali mbali wanatakiwa kuendelea kufanya kazi mbali mbali zikiwemo za kuelezea kwa kina namna Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 inavyotekelezwa katika maeneo yao.

Amesema Viongozi hao wanatakiwa kuwahamasisha Vijana na Makundi mengine yaliyomo katika jamii wajiunge na CCM ikiwa ni sehemu ya kuongeza Wanachama wapya waliotimiza umri wa kupiga kura kwa mujibu wa Sheria za Nchi, ambao ndio Mtaji wa kudumu wa CCM watakaoleta ushindi wa Chama katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi,amefafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amekuwa ni Muadilifu na kinara wa kuenzi na kudumisha Amani na Utulivu wa Nchi hali inayochochea Maendeleo Endelevu ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa Tunu hiyo ya Amani inatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote na kila Mwananchi bila kujali tofauti za Kidini,Kisiasa na Kikabila kwani ndio chimbuko la mafanikio katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi,Kijamii na Kisiasa.

Dk.Mabodi amesema Chama Cha Mapinduzi kinawathamini Wananchi Wote bila kujali tofauti zao za Kisiasa ndio maana kinasimamia Sera zake zitekelezwe kila eneo linalohitaji huduma za Kijamii na Kiuchumi.

Sambamba na hayo amewasihi Viongozi hao kuendeleza Utamaduni wa kufanya Vikao vya Kikatiba kwa Wakati husika ili kutoa fursa pana ya ngazi mbali mbali za Uongozi kujadili na kufanya Maamuzi ya kuimarisha Chama.

Amekumbusha kuwa CCM haitovumilia Mwanachama yeyote atayetumika kufanya ama kufanyiwa kampeni za kugombea nafasi za Uongozi mwaka 2020,kabla ya Chama kutangaza kufanyika kwa mchakato huo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud,amesema kufanyika kwa Mkutano huo kunatoa nafasi pana kwa Ngazi ya Mkoa ya Kichama kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Mohamed amesema kuwa Hali ya Kisiasa ndani ya Mkoa huo kwa sasa ipo vizuri na inaimarika zaidi kutoka na juhudi za Viongozi wa Majimbo ambao ni Wabunge na Wawakilishi kutekeleza Wajibu wao kwa Jamii.

Awali akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mfenesini Ndugu Kesi Mashaka Ngusa,amesema kuwa  Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo imeendelea kutekeleza kwa ufanisi masuala mbali mbali ya kuleta Maendeleo ndani ya Wilaya sambamba na kuwajenga Kiitikadi na Kiuongozi Wanachama wa CCM hasa Vijana na Wanawake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni