Jumanne, 28 Mei 2019

CCM WILAYA YA KUSINI UNGUJA YAKAGUA VITUO VYA AFYA MAKUNDUCHI.

  MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Abdulaziz Hamad Ibrahim(wa Tatu kushoto) akizungumza na Uongozi wa Kituo cha Afya cha Kajengwa katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ya Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Vituo vya Afya vilivyopo katika Jimbo la Makunduchi.

 Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Ndg. Hafidh Hamad Mkadam(wa kwanza  kushoto aliyesimama) akifafanua lengo la ziara hiyo kuwa ni ya Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kusini Unguja wakiongozwa na  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Abdulaziz Hamad Ibrahim akikagua  Ujenzi wa Nyumba ya Madaktari katika Hosapitali ya Kajengwa. 

 MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Abdulaziz Hamad Ibrahim akiwa na Kamati ya Siasa wakikagua Sehemu ya Kuchomea Takataka (Kinu Moshi) za Kituo cha Afya Kibuteni katika ziara hiyo ya kukagua Utekelezaji wa Ilani.

 KAMATI ya Siasa Wilaya ya Kusini Unguja wakipatiwa maelezo kutoka kwa Uongozi wa Kituo cha Afya cha Kizimkazi Mkunguni.

 BAADHI ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kusini Unguja wakisikiliza kwa makini maelezo  Afisa Utabibu Kituo cha Afya Mtende.


 KAMATI ya Siasa Wilaya ya Kusini Unguja wakikagua Shimo la Kuchomea Taka za Kituo cha Afya cha Kizimkazi Mkunguni linalohitaji matengenezo ya kujengewa kutokana na kuwa wazi.



MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Abdulaziz Hamad Ibrahim, ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kutatua Changamoto zinazovikabili Vituo vya Afya katika Jimbo la Makunduchi ili kwenda sambamba na Matakwa ya Ugatuzi  katika Sekta ya Afya Nchi.

Maelekezo hayo ameyatoa leo katika Ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2015/2020 katika Vituo vya Afya Vilivyomo ndani ya Jimbo la Makunduchi Unguja.

Amesema Serikali imefikia uamuzi wa kufanya Ugatuzi katika Sekta ya Afya kwa kuzipatia Mamlaka ya usimamizi Halmashauri za Wilaya kwa lengo la kuimarisha Huduma za Afya ili Wananchi wapate huduma bora na kwa wakati mwafaka.

Mwenyekiti huyo ameipongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kuimarisha upatikanaji wa Vifaa Tiba na huduma mbali mbali za msingi za Afya licha ya kuwepo kwa baadhi ya Vituo vinavyokabiliwa na Changamoto ya Miundombinu Duni ya Majengo hali inayosababisha usumbufu kwa Wananchi na Watumishi wa Afya.

Abdulaziz ameusisitiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kufanya ziara za mara kwa mara katika Vituo vya Afya kwa lengo la kuratibu changamoto zinazovikabili Vituo hivyo na kuzitatua  ili viendelee kutoa Huduma Bora za Afya.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo kwa niaba ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, amemshukru  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kusimamia ipasavyo Mfumo wa Utoaji wa Huduma za Afya Bure kwa Wananchi.

"Tumetembelea Vituo vya Afya mbali mbali vilivyopo katika Jimbo la Makunduchi na kujionea namna vinavyotoa Huduma za Afya kwa Wananchi lakini pia tumebaini uwepo wa Changamoto ndogo ndogo na tumetoa maelekezo kwa wahusika zitatuliwe kabla ya Mwaka 2020."amesema Mwenyekiti huyo wa CCM Abdulaziz.

Aidha amesema Chama Cha Mapinduzi Wilayani humo kitaendea kuisimamia Serikali itekeleze kwa ufanisi Ilani ya Uchaguzi hasa katika masusla ya utoaji wa Huduma za Afya ili kila Mwananchi apate fursa hiyo bila vikwazo.

Wakizungumza kwa Wakati tofauti Maafisa Utabibu wa Vituo vya Afya katika Jimbo hilo wameipongeza Serikali Kuu kwa kufanya Ugatuzi ambao  umeongeza upatikanaji wa Huduma Bora za Afya kwa Wananchi wa Vijijini.

Maafisa hao walizitaja Changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na Uchakavu wa Majengo ya Vituo, Ukosefu wa Uzio, Ukosefu wa Huduma za Usafiri kwa Watumishi wanaoishi mbali na Vituo hivyo, ukosefu wa Walinzi kwa baadhi ya Vituo pamoja na upungufu wa Watumishi kwa baadhi ya Vituo.

Ziara hiyo imefanyika katika Vituo vya Afya vya Mtende,Kibuteni,Kizimkazi Mkunguni, Kizimkazi Dimbani pamoja na Muyuni.















































































































































Hakuna maoni:

Chapisha Maoni