Jumamosi, 25 Mei 2019

VIONGOZI WA WADI HADI WILAYA ZA UWT MKOA WA MAGHARIB WAPEWA MAFUNZO.

 
 KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao(wa Pili kushoto anayezungumza) akitoa Mada ya Wanawake na Uongozi katika Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Viongozi wa UWT Ngazi za Wadi hadi Wilaya za UWT Mkoa wa Magharibi Unguja huko katika Ukumbi wa UWT Wilaya ya Dimani Kiembesamaki.
 BAADHI ya Viongozi wa UWT wa Ngazi za Wadi hadi Wilaya wakifuatilia kwa makini Mafunzo hayo ya Siku Moja ya kuwajengea uwezo juu ya masuala mbali mbali ya Uongozi na Siasa.



VIONGOZI wa Ngazi mbali mbali za Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Tanzania Mkoa wa Magharibi wametakiwa kueleza Changamoto zinazowakabili Wanachama wa CCM ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar Ndugu Catherine Peter Nao wakati akitoa Mada ya  Wanawake na Uongozi wakati akifungua Mafunzo ya kuwajengea Uwezo  Viongozi wa UWT ngazi za Wadi hadi Wilaya za UWT Mkoa wa Magharibi Unguja.

Ndugu Catherine amesema baadhi ya Viongozi wa Kamati hizo hawasemi changamoto zilizopo katika maeneo wanayoyaongoza hali inayosababisha kukwama kwa baadhi ya majukumu ya Kiutendaji.

Amesisitiza suala la ushirikiano katika masuala ya kiutendaji ili kazi mbali mbali za UWT ziweze kwenda sambamba na matakwa ya Katiba na Kanuzi za Umoja huo na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla.

Katika maelezo yake Bi.Catherine amewasihi  Viongozi hao kutojihusisha na masuala ya makundi yasiyofaa ya kusaka Wagombea Urais,Ubunge,Uwakilishi na Udiwani kabla ya muda uliopangwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la mwaka 2017,  pamoja na miongozo na Kanuni mbali mbali za Chama.

Amesema kazi kubwa iliyopo mbele ya Umoja huo kwa sasa ni kujipanga vizuri kwa  kuongeza Wanachama wapya ndani ya CCM ambao ndio Mtaji madhubuti wa Kisiasa utakaoweza kufanikisha Ushindi wa CCM mwaka 2020.

Kupitia Mafunzo hayo amesema mwaka 2019 ni muda wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara ambao utakuwa ni kipimo halisi cha maandalizi ya Ushindi wa 2020 ,hivyo kila Kiongozi wa Umoja huo ajipange kuwamasisha Wanawake wajitokeze kwa wingi wakati utakapofika kuwania nafasi za Uongozi na kuhakikisha Wagombea wa CCM wanashinda.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi Zainab Ali Maulid amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuwakumbusha Viongozi hao Majukumu yao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka Ujao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Viti Maalum kupitia Mkoa wa Magharib ambaye pia ni Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar  Mhe.Amina Idd Mabrouk amesema Mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuwajengea Uwezo wa Kisiasa na kuwaunganisha pamoja ili wanufaike na fursa za zilizopo za Kijamii na Kichumi.

Amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuwaamini Wanawake kwa kuwateuwa katika nafasi mbali mbali za Uongozi ambazo wamekuwa wakizitendea haki kwa kutekeleza majukumu wanayopewa kwa ufanisi.

Mafunzo hayo elekezi ya siku moja kwa Viongozi wa UWT kuanzia ngazi za Wadi hadi Wilaya za Umoja huo yameandaliwa na Wawakilishi na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Magharibi Unguja.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni