ALIYEKUWA Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan Abdallah Shaaban Enzi za Uhai wake. |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Idd, leo ameongoza Maelfu ya Wananchi katika Mazishi ya Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan Abdallah Shaaban aliyefariki jana May 16,2019 akiwa katika Matibabu Hospitali ya Agakhan Jijini Dar es saalam na
amezikwa leo kijijini kwao Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Mazishi hayo yameudhuriwa na
Viongozi na Watendaji mbali mbali wa CCM na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla,Spika wa Baraza
la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeir Ali Maulid na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamy
wa Pili wa Rais Aboud Mohamed Aboud.
Viongozi wengine ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya
CCM Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mawaziri na Manaibu
Mawaziri, Wabunge na Wawakilishi,Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za
SMZ,Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa ngazi mbali mbali pamoja na Wana CCM na
Wananchi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja
Suleiman Mzee Suleiman, akisoma wasifu wa marehemu amesema CCM
imepokea kwa mshtuko na huzuni mkubwa taarifa ya Kifo cha Ramadhan
Abdallah Shaaban ambaye alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka
Mkoa wa Kusini Unguja na Mkurugenzo wa Uratibu wa Uchaguzi Afisi Kuu ya CCM
Zanzibar.
Amesema Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban
alizaliwa mwaka 1948 katika Mkoa wa Kusini Unguja Wilaya ya Kati katika Kijiji
cha Uzini na kupata Elimu yake ya Msingi kuanzia mwaka 1964 hadi 1967 katika
Skuli ya Msingi Ndijani Wilayani humo.
Pia alieleza kwamba Marehemu aliendelea na
Elimu yake ya Sekondari katika Skuli ya Sekondari ya Lumumba mwaka 1968 hadi
1976 alipomaliza Kidato cha Nne na kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Nkuruma na
kuhitimu Diploma ya Ualimu, na kujiendeleza kielimu katika Vyuo Vikuu mbali
mbali vya ndani na nje ya Nchi.
Kupitia risala hiyo imeeleza kuwa Marehemu
enzi za uhai wake alikuwa Mwanachama na Kiongozi Mtiifu wa kuaminika lakini pia
alikuwa Mshauri ,Mkufunzi na mpiganaji na kamanda mzuri aliyelinda maslahi ya
CCM na Muumini mzuri wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Katika maelezo yake Katibu huyo, ameeleza kuwa
Marehemu Enzi za Uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Chama na
Serikali ambapo alikuwa ni miongoni mwa Makada Watiifu wa Afro-Shirazi Party
Yourth Legue na Mwanachama wa ASP.
Alisema mwaka 1977 alikuwa ni Balozi na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM Tawi la Uzini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Wilaya ya Kati na mwaka 1980 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
na kuwa Waziri wa Biashara Zanzibar.
Nyadhifa nyingine alizowahi kushika Marehemu
Ramadhan enzi za uhai wake mwaka 1980 hadi 1985 alikuwa Mbunge na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Muungano katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
mwaka 1988 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la JUWATA Tanzania.
Mnamo mwaka 2005 hadi 2015 tena kuwa Mjumbe wa
Baraza la Wawakilishi na Waziri katika Wizara mbali mbali za SMZ zikiwemo
Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na
Waziri wa Ardhi, Nyumba,Maji na Nishati na hadi kifo chake alikuwa Mjumbe wa
NEC CCM Taifa na Mkurugenzi wa Uratibu wa Uchaguzi wa Afisi Kuu ya CCM
Zanzibar.
Sambamba na hayo Katibu huyo alieleza kuwa
Marehemu Ramadhan ataendelea kukumbukwa kwa Mchango wake Mkubwa katika uhai
wake ndani ya CCM na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Fikra zake zitaenziwa kwa Vitendo katika mapambano ya Siasa za
Ujamaa na Kujitegemea.
Marehemu ameacha Vizuka wawili na Watoto Tisa.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala
Pema Peponi Amin.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni