CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka
wananchi, wanachama, viongozi na watumishi wa Chama na Jumuiya zake kufanya suala la Usafi wa Mazingira kuwa
utamaduni wa kudumu ili kuenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akifanya usafi wa Mazingira kupitia Tawi la
CCM la Afisi Kuu Zanzibar Kisiwa Ndui lililopo katika maeneo ya Ofisi hiyo, Mjini
hapa.
Alifafanua kwamba suala la usafi wa mazingira
nchini lifanyike kwa ushirikiano wa wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za
kidini, kisiasa na kikabila kwani panapotokea athari mbaya zinazotokana na
uchafu zinawakumba jamii nzima.
Alisema usafi wa mazingira ni miongoni mwa
mambo muhimu yaliyokuwa yakisisitizwa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964, kwa lengo la kuweka mazingira katika hali ya usafi na haiba nzuri
kwa kuepusha jamii na maradhi ya miripuko.
Alisema Chama Cha Mapinduzi Pamoja na kufanya kazi za
kisaiasa bado kina jukumu la kuhamasisha
wafuasi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuendeleza tabia ya kufanya usafi
wa mara kwa mara katika maeneo wanayoishi.
“ Nakuombeni viongozi, wanachama, na
watumishi pamoja na wananchi kwa ujumla suala la usafi lianzie katika mioyo
yetu hadi katika mazingira tunayoishi, ili kuweka nchi yetu katika muonekano na
haiba ya kuvutia wakati wote.
Pia leo tunafanya usafi kuungana na wananchi
wengine katika maeneo mbali mbali wanaofanya shughuli mbali mbali za
kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.”, alisema Vuai.
Hata hivyo alisema kuwa Chama hicho kwa sasa
kina majukumu makubwa matano yanayotakiwa kutekelezwa kwa ufanisi yakiwemo
Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduza za kutimiza miaka 53 pamoja na kuadhimisha
miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM ambazo kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika
Gombani Pemba.
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliyataja majukumu
mengine kuwa ni kufanikisha Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na kuhakikisha
CCM inashinda, kufanyika Uchaguzi wa Chama mwaka 2017 na kupatikana viongozi
bora wanaoendana na kasi za kiutendaji za chama hicho pamoja Uimarishaji wa
Chama katika kutekeleza shughuli zake kuelekea mwaka 2020.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake
wa CCM Tanzania( UWT), Salama Aboud Talib aliwasihi wanawake nchini kuwa mstari
wa mbele katika kufanikisha shughuli za usafi kwani wao ndio waathirika wakubwa pindi panapotokea
majanga yanayotokana na athari za uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tawi hilo,
Nadra Juma Mohamed aliwapongeza Watendaji wa Afisi Kuu Zanzibar pamoja na
viongozi wengine walioungana na watendaji hao kufanya usafi huo.
Alisema kufanyika kwa usafi huo ni miongoni
mwa harakati za kuunga mkono Waasisi wa Mapinduzi walitoa sadaka maisha yao kwa
ajili ya kupigania uhuru na kuondosha dhuruma zilizokuwa zikifanywa na wakoloni
dhidi ya waafrika nchini.
“ Tawi la CCM Afisi Kuu Kisiwandui tumekuwa
tukifanya usafi na shughuli zingine za kijamii mara kwa mara katika maeneo yetu
kwa lengo la kuhamasisha wanachama wenzetu kuiga mambo mema tuyayoyafanya
katika maadhimisho haya.”, alieleza Nadra.
Akizungumza Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini, Mohamed
Nyawenga alisema suala la usafi wa mazingira liendane na kampeni ya kupiga vita
uharibifu wa mazingira na miondombinu ya maji na barabara nchini.
Usafi huo uliofanyika katika maeneo ya Afisi
Kuu Zanzibar chini ya maafisa wa Afisi hiyo wakishirikiana na viongozi na
watendaji kutoka katika ngazi mbali mbali za Chama na Jumuiya zake ni miongoni
mwa maadhimisho ya kutimiza miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yatakayofikia kilele chake mwaka
January 12, mwaka 2017.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni