Jumamosi, 21 Januari 2017

NICHAGUENI NI WALETEE MAENDELEO DIMANI - NDG, JUMA ALI JUMA


NA CHRISTOPHER LISSA, ZANZIBAR
MGOMBEA wa Ubunge, katika uchaguzi mdogo wa marudio, jimbo la Dimani, mkoa wa Magharibi,  Unguja, Juma Ali Juma, amewaomba wananchi wa jimbo hilo  kuto kufanya makosa  hapo kesho (jumapili)  kwani anania ya dhati ya kusimamia maendeleo katika jimbo hilo.
Wananchi wa  jimbo hilo,  wanatarajia kupiga kura kesho ( Jumapili), kumpata Mbunge   atakayechukua nafasi ya  aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo  Hafidhi Ali Twahil, aliyefariki dunia mwishoni mwa mwaka jana, akihudhuria vikao vya Bunge, mjini Dodoma.

Juma, alisema  miongoni mwa changamoto ambazo  anatarajia kukabiliana nazo eendapo atachaguliwa ni  uboreshaji wa  miundombinu hasa ya  maji, barabara, elimu na afya.
"Najua kuna changamoto mbalimbali ndani ya jimbo langu, hususan uhaba wa maji ingawa yapo lakini hayatoshelezi kwa sababu ya ongezeko kubwa la watu. Pia wananchi wanahitaji barabara bora ili  jimbo hili liweze kufikiwa na fursa nyingi muhimu za maendeleo. Tutaboresha  sekta ya elimu na afya,"alisema Juma.
Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutokufanya ajizi hapo kesho, kwa kumchagua  kwani yeye ni zao la CCM, Chama chenye nguvu, kilichopo madarakani na chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi.
"Ninaamini mkinichagua mimi  ambaye ni zao bora la CCM basi mmechagua maendeleo ndani ya jimbo letu. Chama kinaongozwa kwa Ilani na sera zinazotekelezeka. Nitakuwa kiungo muhimu  katika kwaletea wananchi   maendeleo. Nawaomba Jumapili  wanichague ili niweze kuwatumikia,"alisema mgombea huyo  machachari.
Aidha, Juma ameelezea kuridhishwa na mchakato mzima  wa kampeni unaohitimishwa leo  na kukipongeza Chama kwa kumnadi  ipasavyo pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia kikamilifu kampeni.

"Hakukuwa na dosari zozote zilizotokea. Zilikuwa ni kampeni za kistaarabu  na tunaomba hali iendelee hivyo hata kesho wakati wa upigaji kura ili jimbo letu liwe na amani na wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida baada ya kupiga kura,"alisema Juma.

Mgombea huyo anatarajia kupiga kura yake  katika Kituo cha Fuoni Sekondari, mapema asubuhi na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura  mapema na kumchagua.

"Wasisubiri mchana au jione. Kura ni mapema jioni tunashangilia ushindi. Naomba wasifanye ajizi wachague CCM wananichague Juma,"Hakuna maoni:

Chapisha Maoni