CHAMA Cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar kimewaonya baadhi ya viongozi na wanachama wanaowashutumu na
kuwadhalilisha viongozi wenzao katika vyombo vya habari na hadharani kinyume na
utaratibu wa taasisi hiyo.
Onyo hilo limetolewa na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akitoa mada ya Muelekeo
wa Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka 2017/2022 katika mafunzo maalum ya siku Moja ya
viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya
ya Kaskazini “B” Unguja kichama.
Alisema viongozi na wanachama
wenye tabia hiyo ndani ya CCM hawawezi kuvumiliwa na watachukuliwa hatua za
kinidhamu kupitia vikao vya maadili vya chama hicho endapo watathibitika
kukutwa na hatia ya kuwajibika.
Alifafanua kwamba Chama
hicho kikiwa ndio kinara wa Demokrasia katika mfumo wa vyama vingi Tanzania,
utamaduni wa kukosoana, kuelekezana , wajibishana na kufanya maamuzi mazito kwa
baadhi ya mambo yasiyokwenda sawa kimaadili na kiuongozi upo lakini kwa kufuata
utaratibu wa vikao rasmi vya kikanuni ndani ya chama na sio hadharani.
“ Kuna tabia imezuka
kwa baadhi ya viongozi na wanachama ndani ya CCM Zanzibar wamekuwa wababe kiasi
cha kuwashutumu viongozi wenzao shutuma nzito, tena hadharani na kupitia vyombo
vya Habari, wakati kuna fursa pana ya vikao vya chama ambayo ndio sehemu pekee
ya kuelekezana kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo.
Tabia hiyo hatuwezi
kuivumilia lazima tukate mizizi mapema kabla haijakomaa na kukiangamiza chama
chetu, na wote wanaohusika na tuhuma hizo kwa sasa tunawachunguza na kuwafuatilia
kwa kina ili kujiridhisha na yeyote atakayekutwa na hatia vikao vya Maadili vya
chama vitachukua hatua stahiki bila ya kumuonea mtu yeyote.” Alieleza Vuai huku
akiwataka wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja.
Vuai alisisitiza kauli yake na kuahidi
kuwa Chama hicho Zanzibar hakitomvumilia kiongozi yeyote
anayevunja maadili ya uongozi kwa makusudi badala yake kitamshughulikia bila kujali cheo na umaarufu wake kisiasa.
Aliziagiza Kamati za
Maadili kwa ngazi mbali mbali katika maeneo yaliyozuka migogoro hiyo kuanza
mara moja kutekeleza wajibu wao wa kuwaita viongozi hao katika vikao vya kikanuni ili kusuluhisha na
ikishindikana wafuate utaratibu na kuwapeleka katika ngazi zingine za maamuzi.
Alitoa wito kwa
viongozi na watendaji wa Chama na jumuiya zake pamoja na wanachama kwa ujumla
kusoma Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2012
inayoelekeza kuwa ni Mwiko kwa kiongozi “
Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa
upendeleo , au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa
madaraka hayo”., alinukuu kifungu hicho Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo akizungumzia
mulekeo wa CCM aliwataka viongozi,
watendaji na wafuasi wa Chama hicho kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko
ya muundo mpya wa Chama na Jumuiya zake.
Alisema mabadiliko hayo
yanatokana na kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokaa Disemba 13 mwaka
2016, kufikia maamuzi ya kupitisha mapendekezo ya Kamati Kuu ya kufanya
mabadiliko ya muundo wa Chama hicho.
Vuai alieleza kuwa lengo la kufanyika kwa mabadiliko ya muundo
wa chama ni kuimarisha uhai wa taasisi hiyo kiutendaji na kiuongozi ili iweze
kufanya kazi zake kwa ufanisi kulingana
na wakati uliopo sasa katika ushindani wa kisiasa.
Hata hivyo aliyataja
baadhi ya mapendekezo yaliyofikiwa katika Kikao hicho kuwa ni pamoja na
kupunguza idadi ya wajumbe na vikao ambayo kwa sasa ni kubwa na inafanya chama hicho kishindwe kutekeleza vizuri baadhi
ya majukumu yake.
“ Wajumbe tulitafakari
kwa kina muelekezo wa CCM, mienendo ya kiutendaji ya watumishi na viongozi pamoja na mahitaji halisi ya wanachama wetu
tukaona kuna haja ya kufanyika mabadiliko ili
tutabane matumizi kwa kupunguza baadhi ya gharama zisizokuwa za msingi
ndani ya chama.
Ili chama chetu
kiendelee kuwa mwalimu wa Demokrasia ndani na nje ya Tanzania lazima wanachama
wote tuwe wamoja na wenye mshikamano katika kuunga mkono juhudi za kuleta
mabadiliko yenye ufanisi kiutendaji
ndani ya chama hicho.”, alielza Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo
alifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kikao hicho kuwa yaliamua
kupunguza Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388 na kupendekezwa wawe
158 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Kwa upande wa ngazi ya
Kamati Kuu walipendekezwa wawe wajumbe 24 badala 34 ambapo kati ya hao wajumbe
watatu watachaguliwa na Halmashauri Kuu kutoka Tanzania bara na watatu wengine
watachaguliwa na Halmashauri kuu ya Zanzibar.
Alisema maandalizi ya kufanyika kwa muundo huo
ndani ya Chama yalianza zamani kwani yalikuwa yafanyike mwaka 2012, na
kuhairishwa kutokana na sababu zisizoweza kuepukika.
Alisema baada ya
kuhairishwa kufanyika kwa muundo
huo chama kiliendelea kujipanga kwa kuwashirikisha wataalamu wa masuala ya
kisiasa, kutoka Vyuo ili watathimini na
kutoa ushauri wa kitaalamu utakaozaa muundo unaokidhi mahitaji ya wanachama.
Alibainisha kuwa Mapendekezo
hayo yatapelekea kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Chama na kanuzi za
jumuiya na chama, na kuongeza kuwa vyeo ambavyo havitokuwemo katika Katiba hiyo
havitoruhusiwa ndani ya Chama jumuiya.
Vuai aliwataka viongozi wanaohusika na vikao vya kuchuja
waombaji wa nafasi za uongozi kufuata maadili ya kikanuni kwa kuhakikisha,
muombaji ametimiza masharti ya uanachama kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya
CCM.
Alitoa angalizo kwa
wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uwezo, waadilifu
na waumini wa kweli wa CCM watakaoweza
kusimamia maslahi ya Chama kwa vitendo.
“ Tutumie vizuri fursa
hii ya uchaguzi kwani ndio sehemu pekee ya kupata timu imara ya kuongoza jahazi
la CCM kwa ufanisi na mafanikio makubwa kwa miaka mitano ijayo.
Pia ngazi husika hasa
Kamati za siasa kwa ngazi mbali mbali lazima mtoe taarifa na matangazo mapema kwa wanachama ili waweze kujitokeza
kwa wingi kuwania nafasi za uongozi kwani ni haki ya kikatiba kwa kila
mwanachama kuchagua na kuchaguliwa ’’ Alisisitiza
kiongozi huyo.
Aidha aliwataka
wabunge, wawakilishi na madiwani kutengeneza mazingira rafiki ya upatikanaji kwa
urahisi fursa za Mikopo na mafunzo ya Ujasiriamali kutoka katika taasisi
zinazozihusika na masuala ili ziweze kuwasaidia vijana ambao hawapo katika
mfumo rasmi wa ajira na waweze kujiajiri wenyewe.
Nao Washiriki wa Mafunzo
hayo waliwashauri viongozi na Watumishi wa CCM na Jumuiya zake wa ngazi za Juu
kuonyesha mfano wa kiutendaji ili viongozi na wanachama wa ngazi za chini
waweze kufuata nyayo hizo kwa vitendo.
Walisema licha ya Mkoa
huo kuwa na fursa ya Hoteli nyingi za Kitalii na rasilimali ya bahari bado
kundi la vijana wanakabiliwa na tatizo
la upungufu wa ajira, jambo linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu na serikali kwa kushirikiana na Chama.
Mafunzo hayo ya siku
moja yamewashirikisha jumla ya viongozi
na watendaji 487 wa chama na jumuiya wa ngazi za matawi, wadi na majimbo ya
Wilaya ya Kaskazini “B” kichama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni