Ijumaa, 27 Januari 2017

CCM Z'BAR YAWAPONGEZA WANANCHI WA JIMBO LA DIMANI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaahidi Wananchi wa Jimbo la Dimani na maeneo mengine nchini kuwa kitasimamia Serikali Kuu Kuhakikisha inatekeleza  kwa vitendo ahadi zote walizoahidiwa wananchi hao.

Ahadi hiyo imetolewa na  Katibu wa Idara Maalum ya NEC, Itikadi na Uenezi Zanzibar wakati akitoa Pongezi kwa Wafuasi wa CCM na Wananchi wa Jimbo la Dimani kupitia taarifa kwa vyombo vya habari hapo Ofisi kwake Kisiwandui Zanzibar.

Alisema Chama hicho kimejengwa katika misingi ya ukweli na uwazi katika utekelezaji wa ahadi zake kwa umma hivyo ni lazima kiisimamie serikali kwa kuikumbusha utekelezaji wa ahadi ambazo hazijafanyiwa kazi kwa baadhi ya maeneo.

Kupitia Taarifa hiyo aliwapongeza kwa dhati Wanachama wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla jimboni humo kwa kuonyesha imani na mapenzi makubwa juu ya CCM hatua iliyofanikisha ushindi kwa Juma Ali Juma aliyepata kura 4,860 na kumshinda mpinzani wake kutoka CUF, Abdulrazak Khatib Ramadhan aliepata kura 1,234.

 Katika Uchaguzi huo wapiga kura walikuwa 6, 172 kati ya wapiga kura 9,275 waliojiandikisha katika Daftari la Wapiga kura Jimboni humo.

Alisema ushindi wa mgombea wa Chama hicho katika uchaguzi huo umekuwa mkubwa kuliko ule wa uchaguzi wa mwaka 2015, ishara inayotoa matumaini ya kuwa wananchi wa jimbo hilo wanaendelea kuiunga mkono CCM.

Aliwapongeza viongozi na  watumishi wa CCM Zanzibar kwa ngazi mbali mbali waliosaidia kwa njia moja ama nyingine kufanikisha uchaguzi huo.

Pia alisifu juhudi zilizofanywa na vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kulinda Amani na Utulivu katika maeneo yaliyofanyika Uchaguzi ndani ya jimbo hilo kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo lakini wamesaidia kulinda  amani kwa ufanisi mkubwa.

Waride alisema ushindi huo umetokana na sera na mipango endelevu vinavyotekelezwa na chama hicho kwa vitendo katika maeneo mbali mbali nchini hasa katika Jimbo la Dimani.

“ Siri ya ushindi wetu ni ukweli, utu na kusimamia misingi ya haki bila ya ubaguzi vinavyofanywa na viongozi wa CCM kwa kuwatumikia wananchi wetu bila ubaguzi.

Pia Mgombea wetu alikuwa na vigezo vyote vya kuwa kiongozi wa jimbo hilo kutokana na sifa zake za utendaji unaoambatana uadilifu katika kutekeleza ahadi anazotoa kwa jamii.”, alifafanua Waride na kuwataka viongozi, watendaji na Wana CCM kuendelea kujipanga kikamilifu katika Chaguzi zingine zijazo.

Aidha aliahidi kuwa CCM itasimamia kikamilifu viongozi wake wanaotokana na ridhaa za Wananchi hasa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani ili waweze kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2015/2020  kwa mujibu wa mahitaji halisi ya wananchi.

Akizungumzia tathimini ya CCM katika Uchaguzi huo alisema umefanyika katika mazingira yaliyokuwa  huru na Kidemokrasia kwa kuzingatia maelekezo na masharti ya NEC yaliyotolewa kabla ya kuanza zoezi hilo.

Alisema licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo zilizoundwa na wafuasi wanaosadikiwa kuwa wa Chama Cha CUF kwa nia ya kuvuruga uchaguzi huo kwa baadhi ya maeneo lakini Vyombo vya ulinzi vimetekeleza wajibu bila kusababisha vurugu.

Uchaguzi huo uliofanyika Juzi kwa lengo la kuziba nafasi ya Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani marehemu Hafidh Ali Tahir aliyefariki akiwa mbungeni Dodoma mwaka jana, hatimaye limepata mrithi wake kutoka ndani ya CCM.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni