Jumapili, 20 Agosti 2017

Dkt. Shein " wazazi simamieni vizuri malezi ya watoto "


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein  amewataka wazazi na walezi nchini kusimamia vizuri malezi ya watoto wao kwa kuhakikisha wanapata elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao ya  baadae.

Rai hiyo ameitoa wakati akizindua shule ya msingi ya Kihinani huko Jimbo la Mfenesini  Wilaya ya Magharibi  ‘’A’’  Unguja, amesema serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu kwa kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanasoma katika majengo  yenye hadhi na wanapata elimu bora.

Dkt. Shein alifafanua kuwa mara baaada ya kufanyika mapinduzi ya mwaka 1964 aliyekuwa Rais wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume alitangaza rasmi mpango wa elimu bure ili watoto wa waafrika waweze kusoma kama walivyokuwa wakisoma watoto wa baadhi ya jamii zilizokuwa na uwezo.

Akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khadija Ali Khamis  alisema skuli hiyo yenye madarasa sita na wanafunzi 1307 imejengwa kwa nguvu za wananchi  wa Kihinani.

Katibu Mkuu huyo amesema kwa sasa Zanzibar ina jumla ya shule za msingi 288 zilizojengwa na wananchi na wamezikabidhi kwa serikali imalizie ujenzi huo ambapo tayari serikali kupitia bajeti ya mwaka huu zitamaliziwa ujenzi wake.

Aidha Dkt. Shein amekagua  mradi wa maji safi na salama uliopo katika kijiji cha Bumbwisudi una visima  tisa na kimoja kati ya hivyo ni kikubwa kina uwezo wa kuzalisha lita za maji 220,000 na utakaosambaza maji  katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja  unatarajia kugharimu shilingi bilioni 11.

Akizungumza Dkt. Shein katika mradi huo aliiagiza Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kusimamia ipasavyo mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

Dkt. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  ameweka jiwe la msingi katika Tawi la CCM Bumbwisudi na kuwataka viongozi waliochaguliwa na wananchi kutekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi ili waweze kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao.

Makamo Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa kwa nafasi alizokuwa nazo ndani ya Chama na serikali ni lazima asimamie na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa ufanisi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Mabodi amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kuthamini maendeleo yanayoletwa na serikali ya awamu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni