Jumamosi, 19 Agosti 2017

DR.SHEIN AANZA ZIARA YAKE KATIKA MKOA WA MJINI MAGHARIBI UNGUJA


MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amewambia viongozi na wanachama wa chama hicho kuwa huu ndio wakati wa kutumia ipasavyo Matawi ya chama kujadili kwa kina mipango itakayoimarisha taasisi hiyo kisisasa na kiuchumi.

Wito huo ameutoa katika ziara yake mara baada ya kuzindua Tawi la CCM la Mwembe Matarumbeta huko Jimbo la Jang’ombe Unguja. 

Amesema kuna baadhi ya maeneo viongozi wamekuwa hawafungui Matawi mara kwa mara hadi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kusababisha kutofanyika kwa wakati vikao vya chama hicho.

Dkt. Shein ameelezea kuridhishwa kwake na ujenzi wa Tawi hilo ambalo limekuwa la kisasa linaloendana na hadhi ya chama cha mapinduzi. Kupitia hafla hiyo Dkt. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amewataka viongozi wa chama hicho waliomba ridhaa ya uongozi kupitia majimboni kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao kwa wakati.

 Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Mabodi amesema ziara za uzinduzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo inayofanywa hivi sasa na Dkt. Shein nchini ni kipimo tosha cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo. 

 Mapema Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alipokea taarifa ya utekelezaji ya Mkoa wa mjini magharibi iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed iliyozungumzia mafanikio yaliyopatikana katika Nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa. 

 Baada ya kupokea taarifa hiyo Dkt. Shein alianza ziara yake kwa kukagua ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa Mao Tse Tung wenye viwanja vidogo vidogo vya mpira wa kikapu, mpira wa mikono na sehemu ya mazoezi ya kunyanyua vyuma vizito unaojengwa kwa msaada wa serikali ya China ambao utagharimu dola bilioni 11.

Akizungumza Dkt. Shein mara baada ya kukagua uwanja huo amesema dhamira ya serikali ni kuimarisha sekta ya michezo nchini kwa kujenga viwanja vya kisasa ili vijana wapate sehemu za uhakika za kuinua vipaji vyao. 

Dkt. Shein amekagua mradi wa kuzuia mawimbi ya Bahari katika eneo la Kilimani Unguja na kupokea taarifa ya mradi huo ambayo imeeleza kuwa maji ya bahari yameathiri eneo la hekta nne ambazo tayari wamepanda miti aina ya mikoko 35,000 kwa ajili ya kuzuia athari za kimazingira katika eneo hilo. 

 Aidha ametembelea na kukagua ujenzi wa jengo la ghorofa mbili la Chuo cha maendeleo ya Utalii Zanzibar na kuona harakati mbali mbali za ujenzi wa jengo hilo linalotarajiwa kukamilika Disemba 15, mwaka huu. 

 Picha mbali mbali za matukio ya Ziara ya Mkoa wa Mjini















































Hakuna maoni:

Chapisha Maoni