Jumatano, 16 Agosti 2017

Unguja kuongeza juhudi katika kilimo cha zao la ndimu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa vijiji vya Ukongoroni na Charawe Wilaya ya Kati Unguja kuongeza juhudi katika kilimo cha zao la ndimu ili liwakomboe kiuchumi. Wito huo ameutoa katika ziara yake ya kikazi inayoendelea katika Mkoa wa Kusini Unguja ndani ya Wilaya ya Kati ambapo amezungumza na wananchi wa vijiji hivyo na kuwasihi waendelee kukienzi kilimo hicho huku serikali ikiendelea na mikakati ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kusindika zao hilo. Mapema baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo waliwasilisha Changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na upungufu wa madaktari katika vituo vya afya, ukosefu wa barabara ya kiwango cha lami pamoja na upungufu wa walimu. Dkt. Shein katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizowasilishwa na wananchi hao aliwaagiza mawaziri wanaohusika na sekta hizo kutatua kwa haraka kero hizo. Aidha Dkt. Shein ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliweka jiwe la msingi Tawi la CCM Unguja Ukuu Kaibona na kuwambia wanachama wa chama hicho na wananchi kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi ya maendeleo ya serikali na chama ili kwenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020. Katika ziara hiyo aliweka jiwe la msingi katika jengo la ghala la kuhifadhi Chakula la Jeshi la kujenga Uchumi (JKU) kambi ya Cheju Unguja, ambapo alisifu juhudi za jeshi hilo katika shughuli za kilimo kinachoongeza uzalishaji wa chakula nchini. Amewambia wapiganaji wa jeshi hilo kuwa wanatakiwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa kufanya kilimo cha kisasa. Hata hivyo Dkt. Shein alikagua mradi wa maji safi na salama unaoendelea ujenzi wake katika Shehia ya Mitakawani Wilaya ya Kati Unguja na kuagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) imalize ujenzi wa kituo hicho kwa kipindi cha Mwezi mmoja ili wananchi wapate huduma hiyo kwa wakati. Akimalizia ziara yake katika Kijiji cha Dunga aliweka jiwe la msingi katika jengo jipya la Wilaya ya Kati na kuzitaka mamlaka zinazohusika na ujenzi huo kukamilisha jengo hilo litoe huduma kwa wananchi wa Wilaya hiyo. Wakati huo huo Dkt. Shein alikagua vikundi vya miradi ya ujasiria mali ya Mabaraza ya Vijana Wilaya ya Kati Unguja na kusisitiza vijana hao watumie vizuri fursa hiyo kwani ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kujikwamua katika wimbi la umasikini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni